naomba kutoa hoja mheshimiwa spika, · 2019 linatarajiwa kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 7.8....
TRANSCRIPT
1
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja
kwamba Baraza lako Tukufu lipokee, lijadili na
hatimae likae kama Kamati ya Mapato na
Matumizi ili liidhinishe Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
2. Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nachukuwa
nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu
Mtukufu kwa kutujaalia afya njema na
kuniwezesha kuwasilisha hotuba hii katika
kikao hiki cha Baraza la Wawakilishi.
Namuomba kwa uwezo wake akijaalie kikao hiki
tukiendeshe na kukimaliza kwa maelewano
makubwa ili tufikie lengo tulilojiwekea.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru
kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein kwa umakini na hekima zake
za kuiongoza nchi yetu. Uongozi wake umekuwa
ni dira kwetu sote na hakika umetuletea
2
maendeleo na faraja katika nchi yetu. Bila
shaka sisi wasaidizi wake tutaendelea
kumuunga mkono katika juhudi zake hizo ili
kwa pamoja tufikie azma yetu ya maendeleo ya
nchi kwa wote.
4. Mheshimiwa Spika, naomba sasa nikushukuru
na kukupongeza wewe binafsi Mheshimiwa
Spika pamoja na wasaidizi wako Mheshimiwa
Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa
Baraza kwa kuliongoza Baraza hili Tukufu kwa
umahiri mkubwa. Naomba vile vile
niwashukuru na kuwapongeza Wenyeviti na
Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Baraza la
Wawakilishi kwa kufuatilia kwa karibu utendaji
wa Wizara na Taasisi za Serikali ili kuhakikisha
zinatoa huduma bora kwa wananchi.
5. Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa
namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Kusimamia Ofisi za Viongozi
Wakuu wa Kitaifa, Mheshimiwa Panya Ali
Abdalla, Mwakilishi wa Viti Maalum, Makamu
3
Mwenyekiti, Mheshimiwa Ali Suleiman Ali
(Shihata), Mwakilishi wa Wananchi wa Jimbo la
Kijitoupele na Wajumbe wote wa Kamati hiyo
kwa kuyapitia Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ya
mwaka 2019/2020 na kuyakubali na leo hii
tunayawasilisha katika kikao chako hiki
kitukufu.
HALI YA UCHUMI WA ZANZIBAR:
Ukuaji wa Uchumi:
6. Mheshimiwa Spika, uchumi wa Zanzibar
umeendelea kuwa imara katika kipindi cha
mwaka mmoja uliopita ambapo kwa mwaka
2018 kasi ya ukuaji wa uchumi imefikia
wastani wa asilimia 7.1. Pamoja na mambo
mengine ukuaji huu wa uchumi kwa mwaka
2018 umetokana na kuongezeka kwa asilimia
20.1 ya idadi ya watalii waliofika nchini na
kufikia watalii 520,809 mwaka 2018 kutoka
watalii 433,474 mwaka 2017. Aidha, kumekuwa
na ongezeko la usafirishaji wa zao la mwani
4
ambalo kwa mwaka 2018 limefikia tani 18,215
ikilinganishwa na tani 12,017 mwaka 2017
sawa na ongezeko la asilimia 66. Sambamba
na hilo kumekuwepo na ongezeko la uzalishaji
wa mazao ya chakula hadi kufikia tani 323,170
mwaka 2018 ikilinganishwa na tani 306,190
mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia
11.6.
7. Mheshimiwa Spika, sababu nyengine ni
kuongezeka kwa shughuli za sekta ndogo ya
usafirishaji na uhifadhi sambamba na ongezeko
la idadi ya abiria waliopitia bandarini kufikia
abiria 2,700,000 mwaka 2018 ikilinganishwa na
abiria 2,600,000 mwaka 2017 sawa na
ongezeko la asilimia 3.8. Aidha, idadi ya abiria
waliopitia viwanja vya ndege nayo imeongezeka
na kufikia abiria 1,400,000 mwaka 2018
kutoka abiria 1,200,000 kwa mwaka 2017 sawa
na ongezeko la asilimia 16.7. Vile vile,
kumekuwa na kuongezeka kwa shughuli za
utalii pamoja na muda wa kukaa kwa mgeni
5
ambapo mwaka 2017 watalii 5,046 walikaa kwa
siku 31 ikilinganishwa na watalii 5,920
waliokaa kwa siku kama hizo kwa mwaka 2018
ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.3.
8. Mheshimiwa Spika, mafanikio yote hayo
yanatokana na kuendelea kuwepo kwa hali ya
amani na utulivu nchini jambo ambalo ni
muhimu kwa ustawi wa Taifa letu.
PATO LA TAIFA NA PATO LA MWANANCHI:
9. Mheshimiwa Spika, hali ya Pato la Taifa
imeendelea kuwa nzuri ambapo kwa mwaka
2018 lilifikia thamani ya Shilingi
2,874,000,000 ikilinganishwa na thamani ya
Shilingi 2,684,000,000 mwaka 2017. Aidha,
Pato la Taifa kwa bei za soko limefikia thamani
ya Shilingi 3,663,000,000 mwaka 2018
kutoka thamani ya Shilingi 3,228,000,000
mwaka 2017. Hali hii imesababisha pia
kuongezeka kwa Pato la Mwananchi kutoka
Shilingi 2,104,000 sawa na Dola 944 na
kufikia Shilingi 2,323,000 sawa na Dola
6
1,026. Tayari Zanzibar imekaribia kufikia
kiwango cha nchi ya kipato cha kati cha Dola
1,030 kwa mujibu wa vigezo vya Kimataifa.
MFUMKO WA BEI:
10. Mheshimiwa Spika, kasi ya mfumko wa bei
umeshuka hadi kufikia wastani wa asilimia 3.9
mwaka 2018 ikilinganishwa na wastani wa
asilimia 5.6 mwaka 2017. Kushuka huko
kumesababishwa na kushuka kwa bei za
bidhaa za chakula na zisizo za chakula. Bidhaa
za chakula zilitoka asilimia 5.5 mwaka 2017
hadi kufikia asilimia 1.4 mwaka 2018 na
bidhaa zisizo za chakula zimeshuka kwa
kiwango kidogo kutoka asilimia 5.8 mwaka
2017 na kufikia asilimia 5.7 mwaka 2018.
11. Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa
katika kudhibiti mfumko wa bei ni kuongezeka
kwa uzalishaji wa mazao ya chakula ambapo
tani 323,170.2 zilivunwa kwa mwaka 2018
7
ikilinganishwa na tani 302,190.4 mwaka 2017
sawa na ongezeko la asilimia 5.5.
12. Mheshimiwa Spika, hali hii inatokana
kuwawezesha wakulima kwa kutoa pembejeo na
mafunzo ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia
teknolojia ya gharama nafuu, kuendeleza tafiti
katika sekta ya kilimo na kutokomeza maradhi
yanayokabili mazao ya matunda na mboga za
majani, kuendelea kutoa nafuu maalum ya
ushuru kwa baadhi ya bidhaa muhimu za
chakula, dawa na pembejeo za kilimo.
MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI WA
ZANZIBAR KWA MWAKA 2019:
13. Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa hali ya
uchumi wa Zanzibar kwa mwaka 2019
unategemea kwenda sambamba na utekelezaji
wa Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA III na
Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya
mwaka 2015 - 2020.
8
14. Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa kwa mwaka
2019 linatarajiwa kukua kwa kasi ya wastani
wa asilimia 7.8. Aidha, uchumi unatarajiwa
kuzidi kukua kutokana na kuongezeka na
kuimarika kwa uwekezaji wa Serikali na sekta
binafsi katika sekta ndogo ya usafirishaji na
sekta ya uvuvi. Kumekuwa na ongezeko la meli
za mizigo pamoja na abiria na kuongezeka kwa
uzalishaji wa vifaranga vya samaki na ufugaji
wa samaki, kuanza kwa uvuvi wa bahari kuu
baada ya kununua boti nne za uvuvi; kuimarika
sekta ndogo ya ufugaji ambapo Serikali imezidi
kukiimarisha Kituo cha Utafiti wa Mifugo ili
kusaidia uzalishaji bora na uendelezaji wa
mifugo na mazao yanayotokana na mifugo hiyo.
15. Mheshimiwa Spika, sababu nyengine ni
kuongezeka kwa uzalishaji na usafirishaji wa
zao la karafuu kutokana na matarajio ya
msimu mkubwa kwa zao hilo katika mwaka
2019; kuongezeka kwa kiwango cha idadi ya
watalii wanaoingia nchini kutokana na
9
kupatikana kwa masoko mapya ya utalii,
kuimarika kwa vivutio vya kitalii na malazi na
utumiaji wa mbinu za kidijitali katika
kuutangaza utalii; Zanzibar kuzitumia ipasavyo
fursa za Uchumi wa Buluu na kuimarisha
mazingira ya kufanya biashara sambamba na
kutumika ipasavyo kwa dhana ya Sekta
Mjumuisho kwa sekta za uzalishaji (Twin
Engine Approach); kutumika kwa Sera ya
Viwanda ipasavyo kwa kuiwezesha Mamlaka ya
Viwanda vidogo vidogo na vya kati (SMIDA),
kuimarisha viwanda hivyo na kuwawezesha
vijana kupata fursa za ajira; na kuimarisha
ajira kwa vijana kupitia utekelezaji wa
programu ya ajira kwa vijana, Mfuko wa
Khalifa (Khalifa Fund) na uwezeshaji wa
wananchi kiuchumi.
16. Mheshimiwa Spika, yote haya ni matunda ya
jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi mahiri
wa Rais wa Awamu ya Saba Mheshimiwa Dkt.
10
Ali Mohamed Shein katika kuhakikisha kuwa
hali ya uchumi na kijamii ya nchi yetu na
wananchi kwa jumla inazidi kuimarika kila
kukicha.
17. Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha kuwa
inakamilisha miradi yote mikubwa ya
maendeleo kama ilivyoahidi katika Ilani ya
Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka
2015 – 2020. Miradi hiyo ni pamoja na Ujenzi
wa Jengo la Abiria (Terminal 3) katika Uwanja
wa Ndege wa Sheikh Abeid Amani Karume,
Ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri na Ujenzi wa
Hospitali ya Binguni. Serikali tayari imeandaa
mikakati maalum ya kutafuta fedha kwa nchi
na mashirika rafiki sambamba na kutenga
fedha kutoka katika vianzio vyake vya ndani ili
ikiwa itashindikana kupata msaada kutoka nje
Serikali iendelee na ujenzi huo.
11
18. Mheshimiwa Spika, Maelezo zaidi kuhusu
mpango huu wa Serikali yatatolewa kwa kina
katika hotuba ya bajeti kuu ya Serikali kupitia
Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
19. MIGOGORO YA ARDHI:
Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Ardhi
imekuwa ikichukua hatua za kutatua migogoro
inayowasilishwa hapo ambapo hadi mwishoni
mwa mwaka 2018 kati ya migogoro (mashauri)
522 iliyowasilishwa na kusikilizwa, mashauri
270 yametolewa hukumu. Jitihada nyengine
zinazochukuliwa na Serikali ni kufanya
utambuzi kwa mwenye haki ya matumizi ya
ardhi (Land Adjudication) hatua ambayo kwa
sasa inaendelea katika eneo la Kilimani na
linatarajiwa kuendelea kwa maeneo ya
Migombani, Mazizini na Mbweni.
UCHIMBAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA:
20. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2018/2019 Serikali imekamilisha majadiliano
12
na Kampuni ya RAKGAS kwa Kitalu cha Pemba-
Zanzibar na hatimae kuweza kusainiwa
Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta
na Gesi Asilia (Production Sharing Agreement -
PSA) baina ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na Kampuni ya RAKGAS kutoka Ras
Al Khaimah tarehe 23 Oktoba, 2018.
21. Mheshimiwa Spika, baada ya hatua ya kusaini
Mkataba wa Mgawanyo wa Uzalishaji wa Mafuta
na Gesi Asilia (Production Sharing Agreement -
PSA) baina ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na Kampuni ya RAKGAS, Serikali
kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Gesi
Asilia Zanzibar (ZPRA) imejipanga kufanya
mazungumzo na Kampuni nyengine zinazohitaji
kuwekeza katika Sekta ya Utafutaji wa Mafuta
na Gesi Asilia hapa Zanzibar baada ya
kukamilika kwa hatua za kuvigawa Vitalu
vyengine vilivyopo Zanzibar.
13
22. Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka
2018/2019 imeandaa rasimu tatu (3) za Kanuni
ambazo ni Kanuni ya uchimbaji (Drilling
regulation), Kanuni ya Ada na Vibali (Fees and
Permit Regulation) pamoja na Kanuni ya
Uwasilishaji wa Taarifa za Kila siku (Daily
Reporting Submission Regulation).
23. Mheshimiwa Spika, Serikali imesimamia zoezi la
utafiti wa utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa
njia ya mtetemo kwa maeneo ya nchi kavu
pamoja na maeneo ya kina kifupi cha maji. Kwa
upande wa mtetemo wa maeneo ya nchi kavu
(Onshore), Serikali ilisimamia kikamilifu zoezi
hili katika Kitalu cha Pemba – Zanzibar ambalo
lilifanywa na Kampuni ya BGP kutoka China.
Zoezi hilo lilianza tarehe 8 Februari 2018 na
kukamilika tarehe 25 Septemba 2018. Lengo
kuu la zoezi hilo ni kuangalia maumbile
(features) ya miamba yenye uwezo wa kuhifadhi
Mafuta na Gesi Asilia.
14
24. Mheshimiwa Spika, jumla ya mistari 25 yenye
urefu wa Kilomita 717.1 ilifanyiwa utafiti.
Mistari hiyo ni 11 kwa Unguja yenye urefu wa
kilomita 388.1 na Pemba mistari 14 yenye urefu
wa kilomita 329. Kazi ya uchambuzi/usafishaji
wa taarifa (Data Processing) na kutafsiri taarifa
hizo (Data Interpretation) inaendelea na
inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi
wa Septemba 2019. Aidha, katika mazoezi hayo,
wataalamu wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar wanashiriki kikamilifu.
25. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa zoezi la
mtetemo wa kina kifupi cha maji (Transition
Zones), zoezi hili lilianza tarehe 7 Disemba,
2018 na kumalizika tarehe12 Febuari, 2019
ambapo Kampuni ya BGP kutoka China ndio
iliyofanya kazi hiyo. Jumla ya mistari kumi
(10) yenye urefu wa Kilomita 244 ilifanyiwa
utafiti. Matokeo ya mazoezi yote mawili
itatolewa kwa wananchi baada ya kukamilika
na Serikali kwa upande wake kujiridhisha.
15
HALI YA UPATIKANAJI WA MCHANGA:
26. Mheshimiwa Spika, mchanga ni miongoni
mwa rasilimali muhimu hapa Zanzibar
kutokana na matumizi makubwa katika sekta
ya ujenzi. Kwa bahati mbaya eneo halisi
linaloweza kuchimbwa mchanga katika visiwa
vyetu ni dogo zaidi kwa kuwa baadhi ya
maeneo tayari yameshachimbwa, maeneo
mengine yanatumika kwa matumizi mengine ya
kibinaadamu ikiwemo makaazi, kilimo na
huduma za jamii.
27. Mheshimiwa Spika, Kutokana na hali hiyo,
tarehe 3 Machi 2017, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ilitangaza utaratibu mpya wa
usimamizi wa uchimbaji, usafirishaji na uuzaji
mchanga nchini ili kudhibiti uchimbaji na
usafirishaji wa rasilimali hiyo pamoja na
kudhibiti maeneo ya ardhi na kuweza kutumika
kwa shughuli nyengine hasa za kilimo.
16
28. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia
Machi, 2017 hadi Disemba, 2018 chini ya
usimamizi wa Serikali, jumla ya Tani 1,690,122
za mchanga zilichimbwa hapa Zanzibar. Kati ya
tani hizo Unguja ilichimba na kusafirishaji tani
1,605,517 na Pemba tani 84,605. Kiwango
kilichochimbwa Pemba ni sawa na asilimia 5 tu
ya uchimbaji unaofanyika Unguja. Kwa
takwimu hizi ni wazi kuwa kuna kasi kubwa ya
uchimbaji wa mchanga katika kisiwa cha
Unguja ukilinganisha na Pemba.
29. Mheshimiwa Spika, tangu usimamizi wa moja
kwa moja unaofanywa na Serikali mafanikio
mbali mbali yamepatikana ikiwemo gari za
mchanga zilipimwa ili kupata malipo na
takwimu sahihi za mchanga uliochimbwa na
kutumika hapa nchini, kupunguza
msongamano wa gari machimboni, kuweka bei
elekezi itakayowazuia wafanya biashara
kupandisha bei ya mchanga kiholela ambayo
inawaumiza sana wananchi.
17
30. Mheshimiwa Spika, Vile vile wafanya biashara
ya mchanga kulipa kodi ya asilimia 3 ya
ushuru wa stempu ili kuchangia pato la Taifa,
kuweka kikomo cha “tripu” za kwenda shimoni
kuchukua mchanga, Serikali kuweka mgao wa
mapato ya mchanga yaliojumuisha gharama za
usimamizi, urejeshaji na mgao wa Halmashauri
ili kuchangia maendeleo ya jamii na malipo
yote ya fedha kulipwa benki ili kuzuia upotevu
na udokozi.
31. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa
changamoto zilizojitokeza wakati wa usimamizi
wa mchanga ni madereva kuuza mchanga kwa
bei kubwa kinyume na bei elekezi, ongezeko la
wizi wa mchanga katika maeneo yasio rasmi
ikiwemo Mangapwani, Nungwi (maeneo ya
fukwe), Mkwajuni, Donge, Bungi, Kinyasini, Uzi
na Maruhubi; kuongezeka kwa matumizi ya
mawe na kifusi kwa kuyasaga na kufanya unga
wa mawe kwa matumizi ya matofali hali
18
ambayo imeongeza kuhatarisha mazingira ya
nchi.
32. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha
2017-2019, Serikali imetayarisha Mpango
mpya wa usimamizi wa uchimbaji, usafirishaji
na uuzaji mchanga nchini kwa kipindi cha
2019 – 2021. Lengo kuu la mpango huu ni
usimamizi bora unaozingatia uhalisia wa
mahitaji, upatikanaji, usafirishaji na uuzaji wa
mchanga kwa uhifadhi wa mazingira, faida za
kiuchumi na kijamii.
33. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa
wananchi kwamba Serikali haitamvumilia
mwananchi yeyote yule ambaye atachimba na
kusafirisha mchanga kinyume na utaratibu
uliowekwa au kuuzwa mchanga kinyume na
bei elekezi iliyotolewa na Serikali.
19
MAENDELEO YA ELIMU:
34. Mheshimiwa Spika, Tumekuwa na
tutaendelea kuchukua hatua mbali mbali
kuhakikisha kuwa mazingira ya elimu
yanakuwa mazuri ili vijana wetu waweze
kupata haki hiyo ya msingi bila ya matatizo.
Kutokana na hatua hizo, hivi sasa asilimia ya
uandikishaji katika ngazi zote za elimu ya
lazima imeongezeka ikilinganishwa na mwaka
wa fedha wa 2017/18 ambapo ngazi ya
maandalizi uandikishaji umefikia asilimia 69.4
mwaka 2018 kutoka asilimia 66.1 mwaka
2017. Kwa upande ya elimu ya msingi imefikia
asilimia 116.5 mwaka 2018 ikilinganishwa na
asilimia 107 ya mwaka 2017 na kwa elimu ya
Sekondari uandikishaji ni asilimia 85.6
mwaka 2018 ambapo 2017 ilikuwa ni asilimia
77.2. Hii inatokana na upatikanaji wa nafasi,
mwamko wa jamii kuhusu elimu na ushiriki
mzuri wa jamii katika kuleta maendeleo ya
elimu.
20
35. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa mashirikiano
na OPEC tayari imekamilisha ujenzi wa skuli
tisa za ghorofa za Sekondari ambazo zipo
Mwembeshauri, Bububu, Kinuni, Fuoni na
Chumbuni kwa Unguja na Wara, Micheweni,
Kizimbani na Mwambe kwa upande wa Pemba.
Aidha, ujenzi wa Maabara, Maktaba, na
chumba cha kompyuta kwa Skuli 24 za
Sekondari kwa mashirikiano na Benki ya
Dunia; na uimarishaji na upanuzi wa
miundombinu ya Skuli ya Sekondari Donge
zinaendelea katika hatua ya mwisho ya ujenzi.
Vile vile, ujenzi wa skuli mbili mpya za Msingi
za Mbuyumaji na Mlilile Wilaya ya Kaskazini
“A” Unguja unatarajiwa kukamilika hivi punde.
Skuli hizi zote zinatarajiwa kuchukua
wanafunzi mwezi wa Januari, 2020 na hivyo
kusaidia sana katika kupunguza msongamano
wa wanafunzi madarasani na kuwawezesha
wanafunzi kujifunza vyema.
21
KADHIA YA UVUJAJI WA MITIHANI YA
KIDATO CHA PILI, ZANZIBAR
36. Mheshimiwa Spika, Itakumbukwa kuwa
mnamo mwezi wa Disemba mwaka 2018,
kulitokea uvujaji wa mitihani ya Kidato cha Pili
kwa Zanzibar. Kutokana na kadhia hiyo
isiyovumilika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
iliifuta mitihani hiyo mara moja.
Pia, Serikali iliiagiza Kamati ya Taifa ya Ulinzi
na Usalama kufanya uchunguzi wa kina na
kujua chanzo na waliosababisha uvujaji huo wa
mitihani.
37. Mheshimiwa Spika, Naomba kuwaarifu kuwa
Kamati hiyo imekamilisha kazi yake kama
ilivyoagizwa na kuwasilisha taarifa tayari
Serikali kwa utekelezaji.
22
Kufuatia taarifa ya uchunguzi imebaini
kwamba:-
i) Baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali pamoja na baadhi ya
watendaji wa Wizara ya Habari, Utalii na
Mambo ya Kale walihusika.
Hivyo, kufuatia uchunguzi huo, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua ya
kuwasimamisha kazi watendaji wote
waliohusika kutoka Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali na Wizara ya Habari, Utalii
na Mambo ya Kale kwa mujibu wa Sheria za
Utumishi wa Umma. Pia Serikali imelitaka
Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kwa
mujibu wa makossa waliyoyafanya.
23
38. KUPAMBANA NA MARADHI
YASIYOAMBUKIZA:
39. Mheshimiwa Spika, imebainika kuwa
wagonjwa wengi wanaokwenda katika vituo
vyetu vya afya na hospitali wamegundulika
kuwa na maradhi ya moyo, kisukari, saratani,
magonjwa sugu ya njia za hewa, ugonjwa wa
meno na magonjwa yanayotokana na ajali.
Miongoni mwa juhudi ambazo Serikali
inazichukua ni kufanya uchunguzi katika jamii
ili kuweza kuibua wagonjwa wa maradhi hayo
na kuwapatia huduma kwa wakati.
40. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa
kutoka Wizara Afya, kwa kipindi cha miezi tisa
iliyopita jumla wagonjwa 7,245 wa maradhi ya
kisukari walihudhuria katika kliniki za
maradhi hayo katika Hospitali za Wilaya na
rufaa, wagonjwa 20,463 walihudhuria katika
kliniki za meno na wagonjwa 702 wa maradhi
ya kansa/saratani walifika Hospitali ya Mnazi
Mmoja kwa ajili ya huduma.
24
41. Mheshimiwa Spika, Jumla ya wafanyakazi
115 wa Unguja na Pemba kutoka vituo na
kiliniki walipatiwa mafunzo ambayo
yalihusiana na namna ya kutumia muongozo
mpya wa kutibu ugonjwa wa Kisukari,
shinikizo la damu na pia kutambua hatua za
awali za maradhi ya saratani. Aidha,
wafanyakazi hao walifundishwa namna ya
kuwatambua wagonjwa wenye matatizo ya
msongo wa mawazo na magonjwa mengine ya
akili na kutakiwa kuwapatia rufaa wagonjwa
wenye matatizo makubwa kwenda hospitali
kubwa kwa hatua zaidi.
42. Mheshimiwa Spika, hatua kama hiyo pia
imechukuliwa kwa waganga wa tiba asili na
wasaidizi wao wapatao 50 kwa ajili ya
kuwawezesha kutambua maradhi ya shinikizo
la damu na kisukari ili wakiona dalili hizo kwa
wateja wao basi wawapatie rufaa katika kituo
cha afya.
25
43. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea
kuchukua hatua madhubuti katika kutoa
huduma za upambanaji wa maradhi
yasiyoambukiza ikiwemo uchunguzi wa
saratani ya shingo ya kizazi kwa akinamama
30,000 Unguja na Pemba, kufundisha
wafanyakazi wa afya ya jamii ili waweze kutoa
ushauri kwa wagonjwa wenye matatizo ya
kisukari na shinikizo la damu na kutoa elimu
kwa jamii juu ya vichocheo vya maradhi
yasioambukiza.
44. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa
Wajumbe wote wa Baraza lako Tukufu na jamii
kwa jumla tuwe na utamaduni na tabia ya
kupima afya zetu angalau mara moja kwa
mwaka.
MAPAMBANO DHIDI YA UDHALILISHAJI:
45. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa
ikichukua jitihada kubwa za kupinga na
kupambana na vitendo vya ukatili na
26
udhalilishaji kwa wanawake na watoto hapa
nchini. Hata hivyo, bado matukio haya
yanaendelea kuripotwa siku hadi siku
ijapokuwa takwimu za mwaka 2017/2018
kutoka Jeshi la Polisi zinaonesha kuwa
matukio haya yamepungua.
46. Mheshimiwa Spika, Uhalifu mwingine wa
kiudhalilishaji ni ule uliojitokeza kwa takriban
kipindi cha mwaka sasa ambapo wimbi la
kuibiwa watoto pamoja na masuala ya ubakaji
yamekuwa yakiripotiwa. Jumla ya matukio 466
yameripotiwa yakiwemo ubakaji 257, kulawiti
64, kutorosha 70 pamoja na shambulio la aibu
75.
47. Mheshimiwa Spika, Tunaliomba Jeshi la Polisi
liimarishe doria na kuwachukulia hatua kali
wale wote watakaobainika kufanya vitendo hivi.
Aidha, napenda kuwaasa wazazi, walezi na
jamii kwa ujumla tuwe karibu na kufuatilia
mienendo ya watoto wetu ili kujua wako wapi,
wapo na nani na wanafanya nini. Vile vile,
27
Masheha na wananchi wanapogundua kuwa
kuna mtu ambaye haeleweki katika maeneo
yao watoe taarifa kwenye vyombo
vinavyohusika haraka.
48. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi
hii kuwataka wafanyakazi wa bandari na
uwanja wa ndege watusaidie kufuatilia kwa
karibu watoto wanaposafirishwa hasa
bandarini kwani ni njia kuu inayotumika
kusafirisha watoto nje ya Zanzibar.
KUKABILIANA NA MAAFA:
49. Mheshimiwa Spika, kama tunavyoelewa
kwamba katika kipindi cha mwezi wa Machi
hadi Juni, nchi yetu huwa katika msimu wa
Mvua za Masika. Kwa mujibu wa taarifa kutoka
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya
Zanzibar muelekeo wa Mvua za Masika kwa
sasa huenda zikapunguwa tukilinganisha na
utabiri uliotolewa hapo awali. Hali hii
inatokana na athari za vimbunga
vilivyoambatana na mvua kubwa zilizotokea
28
nchini Msumbiji, Zimbabwe na Malawi na
kupelekea vifo vya mamia ya wananchi na
uharibifu wa miundombinu ya aina mbali
mbali. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape
subra ndugu zetu hao katika kipindi hiki
kigumu kutokana na maafa hayo.
50. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande wake
wa kukabiliana na maafa inaendelea
kuimarisha miundombinu ili kupunguza athari
za mvua kubwa. Tunawataka wananchi
kuepuka kujenga katika maeneo hatarishi
ambayo mazingira yake yanaweza kuathiriwa
na mabadiliko ya hali ya hewa. Kamisheni ya
Kukabiliana na Maafa kwa kushirikiana na
Taasisi mbali mbali itaendelea kutoa elimu na
tahadhari za mapema kwa wananchi na Taasisi
zetu ili kupunguza athari zinazoweza
kujitokeza.
29
UTEKELEZAJI WA KAZI ZA KAWAIDA NA
MIRADI YA MAENDELEO KWA KIPINDI CHA
MIEZI TISA (JULAI-MACHI) 2018/2019:
51. Mheshimiwa Spika, kazi za kawaida na miradi
ya maendeleo katika Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais zinatekelezwa kupitia Programu Kuu
11 na Programu Ndogo 25. Kwa kipindi cha
miezi tisa (Julai- Machi) cha mwaka wa fedha
2018/2019, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
na Taasisi zake kupitia Programu hizo zilizomo
katika Mafungu matano ya C01, C02, C03 C04
na C05 imetekeleza majukumu yake kama
ifuatavyo:-
OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS (C01)
PROGRAMU KUU (C0101): URATIBU WA
SHUGHULI ZA MAKAMU WA PILI WA
RAIS:
52. Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa na
Programu hii zimeainishwa ukurasa wa 15–16
wa kitabu cha hotuba.
30
53. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2018/2019 Programu iliidhinishiwa kutumia
Shilingi 1,291,205,007 kwa kazi za kawaida
na hadi kufikia Machi, 2019 fedha
zilizoingizwa ni Shilingi 1,112,030,384
ambazo ni sawa na asilimia 86.
PROGRAMU KUU - (CO102): URATIBU WA
SHUGHULI ZA SERIKALI:
54. Mheshimiwa Spika, Programu hii ina Programu
Ndogo saba ambazo ni : -
Programu Ndogo – CO10201: Kukabiliana
na Maafa:
55. Mheshimiwa Spika, Programu hii ndogo kazi
ilizotekeleza zimeanishwa katika ukurasa wa
17 – 19 wa kitabu cha bajeti.
56. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2018/2019 Programu hii Ndogo iliidhinishiwa
kutumia Shilingi 769,800,000 kwa kazi za
kawaida na hadi kufikia Machi, 2019 fedha
31
zilizoingizwa ni Shilingi 668,601,125 ambazo
ni sawa na asilimia 87. Aidha, kupitia mradi
wake wa Kujenga Uwezo wa Kukabiliana na
Maafa ilipanga kutumia Shilingi 106,000,000
na hadi Machi 2019 ilipata Shilingi
88,345,000 ambazo ni sawa na asilimia 83
kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Programu Ndogo – CO10202: Sherehe na
Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na
Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa:
57. Mheshimiwa Spika, Programu hii ndogo kazi
zilizotekelezwa zimeainishwa katika ukurasa
wa 20 wa kitabu chetu.
58. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2018/2019 Programu hii ndogo iliidhinishiwa
kutumia Shilingi 3,021,636,268 kwa kazi za
kawaida na hadi kufikia Machi, 2019 fedha
zilizoingizwa ni Shilingi 3,081,872,537
ambazo ni sawa na asilimia 102.
32
Programu Ndogo – CO10203: Shughuli za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar:
59. Mheshimiwa Spika, Program Ndogo kazi
zilizotekelezwa zimeelezwa katika ukurasa wa
21 – 24 wa kitabu chetu cha hotuba.
60. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2018/2019 Programu hii Ndogo iliidhinishiwa
kutumia Shilingi 7,531,276,133 kwa kazi za
kawaida na hadi kufikia Machi, 2019 fedha
zilizoingizwa ni Shilingi 5,346,657,862 ambazo
ni sawa na asilimia 71. Aidha, Programu hii
Ndogo ilipanga kutumia Shilingi
12,740,000,000 kwa kazi za maendeleo na
hadi Machi, 2019 ilipata Shilingi
3,666,028,400 ambazo ni sawa na asilimia 29.
Programu Ndogo – CO10204: Shughuli za
SMZ Dar es Salaam:
61. Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa
zimeelezwa ukurasa wa 25 – 26 wa kitabu
chetu cha hotuba.
33
62. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2018/2019, Programu Ndogo ya Uratibu wa
Shughuli za SMZ, Dar-es-Salaam iliidhinishiwa
kutumia jumla ya Shilingi 717,604,441 kwa
kazi za kawaida, na hadi kufikia mwezi Machi,
2019 fedha zilizoingia Shilingi 500,499,586
sawa na asilimia 70.
Programu Ndogo – CO10205: Usimamizi wa
Masuala ya Watu wenye Ulemavu:
63. Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa
zimeainishwa ukurasa wa 26 – 29 wa kitabu
chetu cha hotuba.
64. Mheshimiwa Spika, Programu Ndogo ya
Usimamizi wa Masuala ya Watu wenye Ulemavu
kwa mwaka wa fedha 2018/2019 iliidhinishiwa
Shilingi 549,242,435 kwa matumizi ya
kawaida na hadi Machi, 2019 fedha
zilizoingizwa ni Shilingi 403,996,057 ambazo
ni sawa na asilimia 74.
34
Programu Ndogo – CO10206: Usimamizi wa
Mazingira:
65. Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa
zimeelezwa katika ukurasa wa 30 – 31 wa
kitabu chetu cha hotuba.
66. Mheshimiwa Spika, Programu Ndogo ya
Usimamizi wa Mazingira kwa mwaka wa fedha
2018/2019 iliidhinishiwa Shilingi
493,768,200 kwa matumizi ya kawaida na
hadi Machi, 2019 fedha zilizoingizwa ni
Shilingi 371,321,263 ambazo ni sawa na
asilimia 75.
Programu Ndogo – CO10207: Uratibu wa
Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi:
67. Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa
zinaonekana ukurasa wa 32 wa kitabu chetu.
35
68. Mheshimiwa Spika, Programu Ndogo ya
Uratibu wa Mazingira na Mabadiliko ya
Tabianchi kwa mwaka wa fedha 2018/2019
iliidhinishiwa Shilingi 353,456,800 kwa
matumizi ya kazi za kawaida na hadi Machi,
2019 fedha zilizoingizwa ni Shilingi
240,190,049 ambazo ni sawa na asilimia 68.
Aidha, Programu ndogo hii iliidhinishiwa
1,336,700,000 kwa Kazi za Maendeleo na hadi
Machi, 2019 iliingiziwa Shilingi 114,419,600.
PROGRAMU KUU - (CO103): UENDESHAJI
NA URATIBU WA OFISI YA MAKAMU WA
PILI WA RAIS:
69. Mheshimiwa Spika, Programu Kuu hii ya
Uendeshaji na Uratibu wa Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais ina Programu Ndogo tatu ambazo
ni Uongozi na Utawala, Mipango, Sera na
Utafiti na Ofisi Kuu Pemba.
36
Programu Ndogo – CO10301: Uongozi na
Utawala:
70. Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa
zinaonekana ukurasa 33 wa kitabu chetu cha
hotuba.
71. Mheshimiwa Spika, Programu Ndogo ya
Uongozi na Utawala kwa mwaka wa fedha
2018/2019 iliidhinishiwa Shilingi
1,632,537,773 kwa matumizi ya kawaida na
hadi Machi, 2019 fedha zilizoingizwa ni Shilingi
1,075,262,139 ambazo ni sawa na asilimia
66.
Programu Ndogo – CO10302: Mipango, Sera
na Utafiti:
72. Mheshimiwa Spika, kazi ilizotekeleza
zimeanishwa katika ukurasa wa 34 – 35 wa
kitabu chetu.
73. Mheshimiwa Spika, Programu Ndogo ya
Mipango, Sera na Utafiti kwa mwaka wa fedha
37
2018/2019 iliidhinishiwa Shilingi
358,484,205 kwa matumizi ya kawaida na
hadi Machi 2019 fedha zilizoingizwa ni Shilingi
252,497,712 ambazo ni sawa na asilimia 70.
Aidha, Program iliidhinishiwa Shilingi
850,000,000 kwa matumizi ya kazi za
maendeleo na hadi Machi, 2019 fedha
zilizoingizwa ni Shilingi 635,214,979 sawa na
asilimia 75.
Programu Ndogo – CO10303: Uratibu na
Utekelezaji wa Shughuli za Ofisi Pemba:
74. Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa
zimeainishwa katika ukurasa wa 36 wa kitabu
chetu.
75. Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya
Uratibu wa Utekelezaji wa Shughuli za Ofisi
Pemba kwa mwaka wa fedha 2018/2019
iliidhinishiwa Shilingi 916,688,738 kwa
matumizi ya kawaida na hadi kufikia Machi,
38
2019 Ofisi imeingiziwa Shilingi 685,560,260
sawa na asilimia 75.
BARAZA LA WAWAKILISHI (C02):
76. Mheshimiwa Spika, Baraza la Wawakilishi lina
jukumu la kutunga sheria, kufuatilia utendaji
wa Serikali na kuidhinisha na kusimamia
Mipango ya Maendeleo ya Serikali ili
kuhakikisha kuwa mahitaji ya wananchi
yanapatikana. Jukumu hili la Baraza
linatekelezwa kupitia Programu Kuu mbili
ambazo ni:-
PROGRAMU KUU - (CO201): KUTUNGA
SHERIA, KUPITISHA BAJETI NA
KUSIMAMIA TAASISI ZA SERIKALI:
NA
PROGRAMU KUU - (CO202): UONGOZI NA
UTAWALA WA BARAZA LA WAWAKILISHI:
39
77. Mheshimiwa Spika, kazi zinaonekana katika
ukurasa wa 37 wa kitabu chetu cha hotuba.
78. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Baraza la
Wawakilishi kupitia Programu zake mbili kwa
mwaka wa fedha 2018/2019 iliidhinishiwa
Shilingi 20,354,800,000 kwa matumizi ya
kawaida na hadi Machi 2019 fedha
zilizoingizwa ni Shilingi 15,069,399.012
ambazo ni sawa na asilimia 74.
TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR (C03):
79. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar ina Programu Kuu mbili ambazo ni :-
PROGRAMU KUU - (CO301): UENDESHAJI
WA SHUGHULI ZA UCHAGUZI:
NA
40
PROGRAMU KUU - (CO302): USIMAMMIZI
WA KAZI ZA UTAWALA ZA UENDESHAJI
WA SHUGHULI ZA TUME YA UCHAGUZI
YA ZANZIBAR:
80. Mheshimiwa Spika, zimeelezwa katika
ukurasa wa 38 - 40 wa kitabu chetu cha
hotuba.
81. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar kupitia Programu zake kuu mbili
iliidhinishiwa Shilingi 1,774,100,000 kwa kazi
za kawaida na hadi Machi, 2019 fedha
zilizopatikana ni Shilingi 1,374,918,228 sawa
na asilimia 77.
TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA
UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA (C04):
82. Mheshimiwa Spika, Tume ya Kitaifa ya Kuratibu
na Udhibiti wa Dawa za Kulevya ina Programu
kuu mbili ambazo ni:-
41
PROGRAMU KUU - (CO401): UDHIBITI WA
DAWA ZA KULEVYA:
NA
PROGRAMU KUU - (CO402): UENDESHAJI
NA UTAWALA WA TUME YA KITAIFA YA
KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA
KULEVYA:
83. Mheshimiwa Spika, kazi zinaonekana katika
ukurasa wa 40 – 42 wa kitabu chetu.
84. Mheshimiwa Spika, Tume ya Kitaifa ya
Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya
kupitia Programu zake mbili kwa mwaka wa
fedha 2018/2019 iliidhinishiwa Shilingi
941,400,000 kwa matumizi ya kawaida na
hadi Machi, 2019 fedha zilizoingizwa ni
Shilingi 599,734,835 ambazo ni sawa na
42
asilimia 64. Aidha, iliidhinishiwa Shilingi
500,000,000 kwa matumizi ya kazi za
maendeleo na hadi Machi 2019 fedha
zilizoingizwa ni Shilingi 166,000,000 sawa na
asilimia 33.
TUME YA UKIMWI ZANZIBAR (C05):
85. Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI ya
Zanzibar inatekeleza majukumu yake kupitia
Programu kuu mbili ambazo ni :-
PROGRAMU KUU - (CO501): KURATIBU
MUITIKO WA TAIFA WA UKIMWI:
NA
PROGRAMU KUU - (CO502): UENDESHAJI
NA UTAWALA WA TUME YA UKIMWI:
86. Mheshimiwa Spika, kazi zilizotekelezwa
zimeelezwa ukurasa wa 44 – 46 wa kitabu
chetu.
43
87. Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI kupitia
Programu zake mbili kwa mwaka wa fedha
2018/2019 iliidhinishiwa Shilingi
903,500,000 kwa matumizi ya kawaida na
hadi Machi, 2019 fedha zilizoingizwa ni
Shilingi 583,200,000 ambazo ni sawa na
asilimia 65.
UTEKELEZAJI KIFEDHA:
88. Mheshimiwa Spika, Kwa ujumla, Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka wa fedha
2018/2019 kupitia Programu zake 11
ilizokuwa nazo na Programu Ndogo 25
iliidhinishiwa kutumia jumla ya Shilingi
41,609,500,000 kwa kazi za kawaida na hadi
kufikia Machi, 2019 imetumia Shilingi
31,365,691,048 ambazo ni sawa na asilimia
75. Aidha, Ofisi iliidhinishiwa jumla ya
Shilingi 15,532,700,000 kwa Kazi za
Maendeleo na hadi kufika Machi, 2019
44
imepatiwa Shilingi 4,670,007,979 ambazo ni
sawa na asilimia 30 (Angalia Kiambatanisho
Nam. 3 na 4).
89. Mheshimiwa Spika, Ofisi vile vile imekusanya
Shilingi 104,428,000 ambayo ni asilimia 73
ya Shilingi 142,653,000 ilizopangiwa kwa
mwaka wa fedha 2018/2019.
MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA
MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA
FEDHA 2019/2020:
90. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais pamoja na Taasisi zake kwa
mwaka 2019/2020 itatekeleza na kusimamia
Programu kuu kumi na moja (11) na
Programu Ndogo ishirini na tano (25). Kupitia
Programu hizo, Ofisi imepanga kutekeleza kazi
kama ifuatavyo:-
45
PROGRAMU KUU - (C0101): URATIBU WA
SHUGHULI ZA MAKAMU WA PILI WA RAIS:
91. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2019/2020, Ofisi kupitia Programu ya Uratibu
wa Shughuli za Makamu wa Pili wa Rais
imepanga kutekeleza kazi ambazo
zimebainishwa katika ukurasa wa 48 wa
kitabu chetu.
92. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza kazi hizo
kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Programu
ya Uratibu wa Shughuli za Makamu wa Pili
wa Rais imepanga kutumia jumla ya Shilingi
1,262,085,507 kwa kazi za kawaida ambapo
Shilingi 722,530,007 ni kwa ajili ya malipo
ya mishahara na Shilingi 539,555,500 kwa
matumizi mengineyo ya kiutendaji.
46
PROGRAMU KUU - (C0102): URATIBU WA
SHUGHULI ZA SERIKALI:
93. Mheshimiwa Spika, Programu hii ina
programu ndogo saba ambazo ni:-
Programu Ndogo – CO10201: Kukabiliana
na Maafa:
94. Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya
Kukabiliana na Maafa kwa mwaka wa fedha
2019/2020 kazi zilizopangwa kutekelezwa
zimebainishwa katika ukurasa wa 49 – 50 wa
kitabu chetu cha bajeti.
95. Mheshimiwa Spika, Programu Ndogo ya
Kukabiliana na Maafa katika kutekeleza kazi
hizo imepanga kutumia jumla ya Shilingi
1,112,600,000 ambapo Shilingi
932,600,000 kwa kazi za kawaida na
Shilingi 180,000,000 ni kwa kazi za
47
maendeleo. Katika Shilingi 932,600,000 za
matumizi ya kazi za kawaida, Shilingi
376,100,000 ni za mishahara na Shilingi
556,500,000 za matumizi mengineyo.
Programu Ndogo – CO10202: Sherehe na
Maadhimisho ya Kitaifa pamoja na
Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa:
96. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa
fedha 2019/2020, imepanga kutekeleza kazi
zilizobainishwa katika ukurasa wa 50 wa
kitabu chetu.
97. Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya
Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa ili iweze
kutekeleza hayo, kwa mwaka wa fedha
2019/2020, tunaomba Baraza lako ukufu
kuidhinisha jumla ya Shilingi 1,228,836,268
ambapo Shilingi 168,636,268 kwa malipo ya
mishahara ya wafanyakazi na Shilingi
1,060,200,000 kwa matumizi mengineyo.
48
Programu Ndogo – CO10203: Shughuli za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar:
98. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2019/2020 imepanga kutekeleza kazi
zilizoelezwa katika ukurasa wa 51 – 52 wa
kitabu chetu.
99. Mheshimiwa Spika, Ili Programu ndogo ya
Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
iweze kutekeleza hayo kwa mwaka
2019/2020, naliomba Baraza lako Tukufu
liidhinishe jumla ya Shilingi 687,858,033
kwa kazi za kawaida ambapo Shilingi
406,291,133 zitatumika kwa malipo ya
mshahara na Shilingi 281,566,900 kwa
matumizi mengineyo. Aidha, naliomba Baraza
lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi
7,341,349,000 kwa matumizi ya Kazi za
Maendeleo ambapo Shilingi 39,730,000 ni
mchango wa Serikali kwa Mradi/Mpango wa
49
Maendeleo wa Kunusuru Kaya Masikini
(TASAF III) na Shilingi 7,301,619,000 ni
mchango wa washirika wa maendeleo.
100. Mheshimiwa Spika, kupitia Programu hii vile
vile naomba Baraza lako Tukufu liidhinishe
matumizi ya Shilingi 13,900,000,000 ikiwa
ni ruzuku kwa Idara ya Uhamiaji, Zanzibar.
Programu Ndogo – CO10204: Shughuli za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar- Dar es
Salaam:
101. Mheshimiwa Spika, Programu hii imepanga
kutekeleza kazi zilizoainishwa katika ukurasa
wa 53 – 54 wa kitabu chetu cha bajeti.
102. Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Programu ndogo
ya Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Dar es Salaam itekeleze kazi hizo,
naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe
50
jumla ya Shilingi 616,204,441 kwa kazi za
kawaida ambapo Shilingi 342,604,441 kwa
malipo ya mishahara na Shilingi
273,600,000 kwa matumizi mengineyo.
Programu Ndogo – CO10205: Usimamizi wa
Masuala ya Watu Wenye Ulemavu:
103. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha
2019/2020, kazi zilizopangwa kutekelezwa
zimeainishwa katika ukurasa wa 54 – 55 wa
kitabu chetu.
104. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa
fedha 2019/2020, Programu ya Usimamizi wa
Masuala ya Watu Wenye Ulemavu imepanga
kutumia jumla ya Shilingi 616,211,915 kwa
kazi za kawaida ambapo Shilingi
234,460,435 kwa malipo ya mishahara na
Shilingi 381,751,480 kwa matumizi ya
mengineyo.
51
Programu Ndogo – CO10206: Usimamizi wa
Mazingira:
105. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha
2019/2020 imepanga kutekeleza kazi
zinazoonekana ukurasa wa 56 wa kitabu
chetu.
106. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2019/2020, naliomba Baraza lako Tukufu
liidhinishe Shilingi 518,768,200 kwa kazi za
kawaida kwa Mamlaka ya Usimamizi wa
Mazingira Zanzibar ambapo Shilingi
328,768,200 ni kwa ajili ya malipo ya
mishahara na Shilingi 190,000,000 ni kwa
matumizi mengineyo.
Programu Ndogo – CO10207: Uratibu wa
Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi:
52
107. Mheshimiwa Spika, Kazi zitakazotekelezwa
kupitia miradi hiyo zimeelezwa katika ukurasa
wa 57 wa kitabu cha bajeti.
108. Mheshimiwa Spika, Programu ndogo Uratibu
wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi
kupitia Idara ya Mazingira inaomba
kuidhinishiwa Shilingi 1,195,056,800
ambapo Shilingi 388,456,800 kwa kazi za
kawaida na Shilingi 806,600,000 kwa kazi za
maendeleo. Kati ya Shilingi 388,456,800,
Shilingi 238,456,800 ni malipo ya mishahara
na Shilingi 150,000,000 kwa matumizi
mengineyo ya kiofisi. Aidha, kwa upande wa
fedha za maendeleo, Shilingi 350,000,000 ni
kutoka Serikalini na Shilingi 456,600,000 ni
kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
PROGRAMU KUU - (CO103): UENDESHAJI
NA URATIBU WA OFISI YA MAKAMU WA
PILI WA RAIS:
53
109. Mheshimiwa Spika, lengo la Programu hii ni
kuimarisha mazingira bora ya wafanyakazi,
usimamizi wa mipango na shughuli za Ofisi ili
kutoa huduma bora kwa jamii. Programu hii
kuu ina Programu ndogo tatu ambazo ni
Uongozi na Utawala; Mipango, Sera na Utafiti
na Uratibu na Utekelezaji wa Shughuli za Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais, Pemba.
Programu Ndogo – CO10301: Uongozi na
Utawala:
110. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2019/2020 imepanga kutekeleza kazi zake
zilizoainishwa katika ukurasa wa 58 – 59 wa
kitabu cha bajeti.
111. Mheshimiwa Spika, Program Ndogo ya
Uongozi na Utawala ya Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais kwa mwaka wa fedha 2019/2020
inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi
1,651,917,773 kwa kazi za kawaida ambapo
54
Shilingi 912,537,773 ni kwa malipo ya
mishahara na Shilingi 739,380,000 kwa
matumizi mengineyo ya uendeshaji.
Programu Ndogo – CO10302: Mipango, Sera
na Utafiti:
112. Mheshimiwa Spika, Programu ndogo ya
Mipango, Sera na Utafiti kwa mwaka wa fedha
2019/2020 imepanga kutekeleza kazi
zilizoainishwa katika ukurasa wa 59 – 60 wa
kitabu chetu cha bajeti.
113. Mheshimiwa Spika, Programu ndogo
Mipango, Sera na Utafiti imepanga kutumia
jumla ya Shilingi 795,829,373 ambapo
Shilingi 445,829,373 kwa kazi za kawaida na
Shilingi 350,000,000 ni kwa kazi za
maendeleo. Katika Shilingi 445,829,373 za
matumizi ya kazi za kawaida, Shilingi
162,683,253 ni za mishahara na Shilingi
283,146,120 ni za matumizi mengineyo.
55
Programu Ndogo – CO10303: Uratibu na
Utekelezaji wa Shughuli za Ofisi Pemba:
114. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2019/2020 imepanga kutekeleza kazi
zilizobainishwa katika ukurasa wa 60 – 61 wa
kitabu chetu.
115. Mheshimiwa Spika, ili Programu ndogo ya
Uratibu na Utekelezaji wa Shughuli za Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais Pemba itekeleze kazi
hizo kwa mwaka 2019/2020, naliomba Baraza
lako Tukufu liidhinishe Shilingi 927,531,690
kwa matumizi ya kawaida, kati ya fedha hizo
Shilingi 666,731,690 kwa ajili ya malipo ya
mishahara na Shilingi 260,800,000 kwa
matumizi mengineyo.
116. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais vile vile inaratibu shughuli za Baraza
la Wawakilishi, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,
56
Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa
Dawa za Kulevya na Tume ya UKIMWI
Zanzibar, ambazo zina programu kuu na
programu ndogo kama ifuatavyo:-
BARAZA LA WAWAKILISHI (C02):
117. Mheshimiwa Spika, Baraza la Wawakilishi
linatekeleza Program kuu mbili ambazo ni:-
PROGRAMU KUU - (CO201): KUTUNGA
SHERIA, KUPITISHA BAJETI NA
KUSIMAMIA TAASISI ZA SERIKALI:
NA
PROGRAMU KUU - (CO202): UONGOZI NA
UTAWALA WA BARAZA LA WAWAKILISHI:
118. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
wa 2019/2020 kazi zilizopangwa kutekelezwa
na Baraza la Wawakilishi kupitia Programu
hizi zinaonekana katika ukurasa wa 62 – 63
wa kitabu chetu cha bajeti.
57
119. Mheshimiwa Spika, ili Ofisi ya Baraza la
Wawakilishi iweze kutekeleza malengo yake
hayo kwa ufanisi zaidi, naliomba Baraza lako
Tukufu liidhinishe Shilingi 21,009,400,000
kwa kazi za kawaida ambapo Shilingi
9,156,353,922 ni kwa ajili ya malipo ya
mishahara na Shilingi 11,853,046,078 ni
kwa kazi nyenginezo.
TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR (C03):
120. Mheshimiwa Spika, Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar inasimamia Programu Kuu mbili
ambazo ni:-
PROGRAMU KUU - (CO301): UENDESHAJI
WA SHUGHULI ZA UCHAGUZI:
NA
58
PROGRAMU KUU - (CO302): USIMAMIZI WA
KAZI ZA UTAWALA NA UENDESHAJI WA
SHUGHULI ZA TUME YA UCHAGUZI YA
ZANZIBAR:
121. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2019/2020 kazi zilizopangwa kutekelezwa na
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kupitia
Programu hizi zinaonekana katika ukurasa wa
63 – 65 wa kitabu cha bajeti.
122. Mheshimiwa Spika, Ili Programu ya
Usimamizi wa Kazi za Utawala na Uendeshaji
wa Shughuli za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
iweze kutekeleza kazi zake, naomba Baraza
lako Tukufu liidhinishe Shilingi
1,934,400,000 kwa kazi za kawaida ambapo
Shilingi 1,227,900,000 ni kwa ajili ya malipo
ya mishahara na Shilingi 706,500,000 ni
kwa kazi nyenginezo.
59
123. Mheshimiwa Spika, fedha kwa ajili ya
matumizi ya Programu ya Uendeshaji wa
Shughuli za Uchaguzi zinatoka katika Mfuko
Mkuu wa Serikali.
TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA
UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA (C04):
124. Mheshimiwa Spika, Taasisi hii inasimamia
Program Kuu mbili ambazo ni:-
PROGRAMU KUU - (CO401): UDHIBITI WA
DAWA ZA KULEVYA
NA
PROGRAMU KUU - (CO402): UTAWALA NA
UENDESHAJI WA TUME YA KITAIFA YA
KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA
KULEVYA:
125. Mheshimiwa Spika, Tume ya Kitaifa ya
Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya
60
kupitia programu hizi imepanga kutekeleza
shughuli zilizoainishwa katika ukurasa wa
66.
126. Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha
2019/2020, naliomba Baraza lako Tukufu
liidhinishe Shilingi 973,200,000 kwa kazi za
kawaida ambapo Shilingi 220,200,000 ni kwa
ajili ya malipo ya mishahara na Shilingi
753,000,000 kwa kazi nyenginezo za
uendeshaji. Aidha, naomba liidhinishe
Shilingi 680,000,000 kwa Kazi za Maendeleo.
TUME YA UKIMWI (C05):
127. Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI
Zanzibar ina jukumu la kuratibu na kuongoza
mapambano ya kitaifa dhidi ya UKIMWI hapa
Zanzibar kupitia Programu Kuu mbili ambazo
ni:-
61
PROGRAMU KUU - (CO501): URATIBU WA
MUITIKO WA TAIFA WA UKIMWI:
NA
PROGRAMU KUU - (CO502): UTAWALA NA
UENDESHAJI WA TUME YA UKIMWI:
128. Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa
kutekelezwa na Tume ya UKIMWI Zanzibar
kupitia Programu hizi zinaonekana katika
ukurasa wa 67 – 68 wa kitabu chetu cha
bajeti.
129. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza kazi hizo,
nailiomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha
Shilingi 220,619,000 kwa Kazi za Kawaida na
Shilingi 540,000,000 kwa Kazi za Maendeleo
kwa Programu ya Kuratibu Muitiko wa Taifa
wa UKIMWI na Shilingi 699,481,000 kwa
Kazi za Kawaida kwa Programu ya Utawala na
Uendeshaji wa Tume ya UKIMWI ambapo
62
Shilingi 359,700,000 ni kwa ajili ya malipo ya
mishahara na Shilingi 339,781,000 ni kwa
kazi nyenginezo.
130. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, makisio
kwa Programu zote 11 za Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais na Taasisi zake kwa mwaka wa
fedha 2019/2020 ni Shilingi 57,911,349,000
ambapo Shilingi 48,013,400,000 ni kwa kazi
za kawaida na Shilingi 9,897,949,000 ni kwa
kazi za maendeleo (Angalia Kiambatisho
Nam. 5 na 6).
UKUSANYAJI MAPATO
131. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha
2019/2020, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
na Taasisi zake imepangiwa kukusanya
mapato ya jumla ya Shilingi 304,410,000 na
mchanganuo wake unaoonekana katika
ukurasa wa 69 wa kitabu chetu cha hotuba.
HITIMISHO:
63
132. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena
naomba nitoe shukurani zangu za dhati kwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed
Shein kwa kuendelea kuiongoza vyema nchi
yetu na namuomba Mwenyezi Mungu
amuongezee hekima na busara Kiongozi wetu
huyu. Nawashukuru sana Wasaidizi wangu
katika kuiongoza Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais, Mheshimiwa Mohamed Aboud
Mohamed, Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais na Mheshimiwa Mihayo Juma
N’hunga. Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais kwa kuendelea kuzifanya kazi
zao kwa bidii na kuleta mafanikio makubwa.
Aidha, natoa shukurani kwa Watendaji na
wafanyakazi wote wa Ofisi Makamu wa Pili wa
Rais na Taasisi zake wakiongozwa na Katibu
Mkuu Ndugu Shaaban Seif Mohamed na
Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Abdallah Hassan
Mitawi kwa kazi nzuri wanayoifanya
kuhakikisha Ofisi yetu inatoa huduma kwa
64
ufanisi mkubwa. Nawapongeza na
nawashukuru sana.
133. Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia
kuendelea kuwashukuru Waheshimiwa
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kwa
namna walivyoshirikiana na Ofisi yangu
katika mwaka 2018/2019, na kwa namna ya
pekee kwa Mwenyekiti na Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Ofisi za
Viongozi Wakuu wa Kitaifa ambayo
imetupatia ushauri na maelekezo mbali mbali
ambayo kwa sehemu kubwa yametusaidia
katika utoaji wetu wa huduma kwa wananchi.
Vile vile nazishukuru sana Ofisi ya Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Ofisi ya Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo
tumeshirikiana nazo katika masuala mbali
mbali ya Kitaifa.
65
134. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru
sana Washirika wetu wa Maendeleo kwa
kuendelea kushirikiana na Serikali katika
kuwaletea maendeleo wananchi kupitia
miradi mbali mbali. Miongoni mwa Washirika
hao ni:-
Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya
Afrika, Mashirika ya Umoja wa Kimataifa
ikiwemo UNDP, UNICEF, UNFPA, WHO, WFP,
UNAIDS, USAID, FAO na WIPO, Mfuko wa
Dunia wa Kupambana na Kifua Kikuu
Malaria na UKIMWI, Nchi za China, India,
Finland, Norway, Japan, Marekani, Oman,
Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu (UAE),
Cuba na nyenginezo.
135. Mheshimiwa Spika, nazishukuru Taasisi,
Mashirika na Jumuiya zisizo za Kiserikali kwa
kuendelea kutumia uwezo, taaluma na
rasilimali zao kusaidiana na Serikali katika
kuwaletea maendeleo wananchi. Navipongeza
66
sana vyombo vyetu vya habari kwa
kuwaelimisha wananchi juu ya masuala
mbali mbali yanayohusu Mikutano ya Baraza
letu Tukufu pamoja na matukio ya ndani na
nje ya nchi yetu.
136. Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, napenda
kukutakia wewe, Mhe. Spika, Wasaidizi wako
wote pamoja na Wajumbe wote wa Baraza
lako Tukufu Mfungo mwema Mtukufu wa
Ramadhan, mwezi ambao una chumo kubwa
kwetu.
137. Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia kwa
kuwashukuru sana wananchi wote wa
Zanzibar kwa kuendelea kuiunga mkono na
kuilinda Serikali yao ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Aidha, nawashukuru wananchi wa
Jimbo la Mahonda kwa kuendelea kuniunga
mkono katika kutekeleza kazi zangu za
Uwakilishi Jimboni humo sambamba na kazi
yangu ya Makamu wa Pili wa Rais wa
67
Zanzibar. Nawashukuru sana kwa
ushirikiano wanaonipa.
138. Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa napenda
kukutakia wewe Mheshimiwa Spika, wasaidizi
wako wote na pamoja na Wajumbe wa Baraza
lako Tukufu Mfungo mwema wa Mwezi
Mtukufu wa Ramadhan, mwezi ambao una
chumo kubwa kwetu.
139. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo,
sasa naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe
jumla ya Shilingi 57,911,349,000 kwa Ofisi
ya Makamu wa Pili wa Rais na Taasisi zake
kwa ajili ya kutekeleza Programu 11
nilizozielezea hapo awali. Mchanganuo wa
fedha hizo kupitia mafungu yao ni kama
ifuatavyo: -
68
Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais (C01)
Shilingi 31,854,249,000
Ofisi ya Baraza la
Wawakilishi (C02)
Shilingi 21,009,400,000
Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (C03)
Shilingi 1,934,400,000
Tume ya Kitaifa ya
Kuratibu na Udhibiti
wa Dawa za Kulevya
(C04)
Shilingi 1,653,200,000
Tume ya UKIMWI
Zanzibar (C05)
Shilingi 1,460,100,000
JUMLA KUU Shilingi 57,911,349,000
140. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.