kimetayarishwa na kuchapishwa na kikundi cha sheria na haki za

32
1 Kimetayarishwa na kuchapishwa na Kikundi cha Sheria na Haki za Binadamu cha TIFPA kwa niaba ya wana TIFPA kwa msaada wa FORD FOUNDATION

Upload: lehanh

Post on 01-Feb-2017

291 views

Category:

Documents


11 download

TRANSCRIPT

1Kimetayarishwa na kuchapishwa na Kikundi cha Sheria na Haki za Binadamu cha TIFPA kwa niaba ya wana TIFPA kwa msaada wa Ford FoundATIon

2 32 3

YaliyomoShukrani ................................................................................ 3

Utangulizi.............................................................................. 4

1. Katiba ni Kitu Gani? .................................................. 6

2. Kwanini taifa linahitaji Katiba? ............................... 7

3. Ili Tuweze Kupata Katiba Nzuri Ipi ni Misingi ya

Katiba katika Nchi ya Kidemokrasia

(Constitutional Principles)? ........................................ 9

4. Je, ni wajibu wa nani kushiriki katika kutunga

Katiba? ........................................................................ 11

5. Je, ni mambo yapi yanapaswa yawemo kwenye

Katiba? ........................................................................ 11

6. Je, ni mambo yapi yanapaswa kujadiliwa ili

yawemo au yasiwemo katika Katiba Ijayo? ......... 19

7. Je, upi mwongozo bora wa kufuata katika

utungaji wa Katiba? .................................................. 29

Hitimisho ................................................................................ 31

2 32 3

Shukrani

Tunapenda kutoa shukrani zetu za pekee kwa taasisi ya Ford Foundation International iliyopo nchini Marekani kupitia mradi wa taasisi ya International Fellowship Program (IFP) kwa kuwezesha shirika la Tanzania IFP Alumni Assosiciation (TIFPA), pamoja na malengo mengine ya shirika, kuratibu shughuli zote za uandaaji, uchapaji na usambazaji wa uchambuzi huu kwa wananchi wa Tanzania.

Kwa mantiki hiyohiyo, TIFPA inapenda kumshukuru Bwana Kaleb Lameck Gamaya, kwa juhudi zake za kipee kuweza kutayarisha kijarida hiki kwa ajili ya kuwezesha umma wa watanzania wenzetu kuelewa mambo ya kikatiba na ushiriki wao katika mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya. TIFPA pia inawashukuru Bwana Harold Sungusia, Charles Mkude, na Bi. Butamo Kasuka Philip kwa juhudi zao za kuweza kufanyia uhakiki kijarida hiki ili kitumike kama chombo kimojawapo cha kuielimisha jamii katika utungwaji wa Katiba mpya ya Tanzania. Pia TIFPA inapenda kuwashukuru Ndugu Stephen Magoiga, Kassim Gilla, Zuberi Ngoda, Rehema Kerefu na Deus Kibamba kwa mchango wao wa kimawazo. Kwa kifupi, tunasema ahsanteni sana.

Winnie TerryMwenyekitiTIFPA

4 54 5

utangulizi

Kijarida hiki kimetayarishwa ili kutoa mwanga kwa wana jamii wa kitanzania juu ya maana halisi ya Katiba, kazi ya Katiba, misingi ya Katiba na vitu gani haswa vinapaswa kuwemo kwenye Katiba. Sio tu kwamba kijarida hiki ni bora kwa mwananchi wa rika lolote bali pia kwa watu wenye taaluma zozote zile na viwango vyovyote vile.

Kwa kutambua umuhimu wa uandikwaji upya wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa kuelewa kwamba hivi sasa kuna mchakato wa kutungwa kwa katiba mpya, tumeamua kuandaa kijarida hiki kwa makusudi kabisa ili kuweza kwanza kuielimisha jamii ya watanzania kuhusu Katiba kwa ujumla na pili kushiriki kwa njia ya chapisho hili ili kuweza kusaidia kuanzishwa kwa mjadala wa Katiba ambayo watanzania wanaihitaji.

Tumeanzisha mchakato huu tukiwa tunatambua kwamba Tanzania ina Katiba ambayo imefanyiwa marekebisho takribani mara 14 yaliyotokana na mabadiliko mbali mbali ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Pamoja na kuliongoza taifa kwa kipindi chote cha Katiba ya zamani, na pamoja na mabadiliko yote 14 ili kukidhi mabadiliko mbalimbali, bado Katiba ya sasa haijaweza kuendana na wakati na

4 54 5

hivyo matakwa ya uandikwaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sio tu ni swala la msingi bali pia la lazima.

Ni rai yetu kwamba kijarida hiki kitatumika kama sehemu ya mjadala unaoendelea wa Katiba mpya na hivyo kutoa fursa kwa jamii ya kitanzania kuelewa maana halisi ya Katiba ikiwa ni pamoja na mambo yake muhimu katika utungwaji na uandishi wa Katiba mpya ya sasa.

6 76 7

1. Katiba ni Kitu Gani?

Katiba ni sheria mama inayoandikwa au kuwekwa na wananchi kutoka katika taifa huru ili kuainisha pamoja na mambo mengine, misingi mikuu ya utawala, madaraka na majukumu ya mihimili ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama, misingi ya haki za msingi za wananchi, msimamo na mwelekeo wa taifa, mwelekeo au chimbuko na mwongozo wa sheria zote zitakazotungwa katika nchi husika.

Kwa hiyo Katiba ni sheria mama kwa sababu misingi yake huwezesha kutungwa kwa sheria mbalimbali ambazo huwezesha kuwepo kwa vyombo mbalimbali vya kiutawala katika ngazi zote kuanzia Serikali, Bunge, Mahakama na vyombo vingine vyote vya kimaadili, kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na haki za binadamu.

Kwa kifupi, Katiba ni waraka ulio juu ya mambo yote ya kitaifa na sio chombo cha serikali iliyoko madarakani, wanasheria na wanazuoni wachache pekee bali ni chombo kinachoonyesha umiliki wa nchi na rasilimali zake zote wa wananchi, nafasi ya wananchi katika utawala na namna gani wangependa kuweka utawala wa nchi yao na hivyo kutengeneza muundo wa mihimili ya dola ikiwa ni serikali yao, bunge lao na mahakama zao.

6 76 7

Kwa hiyo Katiba ni waraka wa kitaifa unaoweka bayana, pamoja na mambo mengine, mfumo wa haki za msingi kwa wananchi wake, mihimili yake ya dola, namna ya kuweka utawala katika ngazi zote, muundo wa serikali yao na namna ya usimamizi na matumizi ya rasilimali yote ya kitaifa bila ukandamizaji wa aina yeyote kwa jinsia zote.

2. Kwanini taifa linahitaji Katiba?

Kama tulivyoeleza hapo juu, taifa linahitaji Katiba kwani Katiba huzaa muafaka wa kitaifa kwa kuweka misingi mikuu ambayo nchi inahitaji kuifuata. Misingi hiyo hutafsiriwa kupitia sheria, sera, matendo na maadili mbalimbali yanayowekwa na wananchi kupitia njia mbalimbali ikiwamo njia ya uwakilishi katika mihimili yake ya dola ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama.

Taifa linahitaji Katiba kupitia kwa wananchi wake pale kunapotokea mabadiliko au mageuzi makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo yanaifanya Katiba iliyopo au miongozo iliyopo kutokidhi utashi wa wananchi na muundo wa vyombo vyake vya dola.

Kwahali hiyo, kwa mtizamo wetu kama miongoni mwa wanazuoni tumeona kuwa yafuatayo ni mambo muhimu

8 98 9

yanayolazimu Tanzania kuandika Katiba Mpya;

1. Mabadiliko kutoka ukoloni kwenda uhuru mwaka 1961; na kutoka uhuru kuwa Jamhuri mwaka 1962;

2. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964;

3. Mageuzi makubwa ya kisiasa kutoka chama kimoja hadi mfumo wa vyama vingi ya mwaka 1992;

4. Mfumo wa kiuchumi unaorekebisha kwa kiasi kikubwa mfumo wetu wa kijamaa ulioingiza mambo ya utandawazi hivi sasa; ni miongoni mwa mambo makubwa ya kisiasa na kiuchumi yaliyohitaji kuandikwa kwa Katiba.

5. Ushiriki wa wananchi ni sababu nyingine kuu ya Tanzania ya leo kuandika Katiba mpya. Wananchi na wasomi mbalimbali wametanabahisha kuwa michakato yote ya siku za nyuma ya uandikaji wa Katiba mpya katika Tanganyika na hata Zanzibar iliwashirikisha wananchi wachache na kupelekea kutafasiliwa na wachambuzi wa mambo ya kikatiba kuwa haikuwashirikisha wananchi.

8 98 9

6. Muundo wa Muungano na mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya dola ni swala jingine linaloifanya Tanzania ihitaji kuandika Katiba mpya.

7. Ni wazi kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inajumuisha mambo ya Muungano na pia mambo yanayoihusu Tanzania na mambo ya Tanzania Zanzibar. Hivyo ni vyema kuandika Katiba upya ili kuyajadili na kuyaweka bayana mambo yanayohusu muungano na yale yasiyokuwa ya muungano.

Kwahiyo sababu kuu za kuandikwa kwa Katiba mpya ni kuakisi mabadiliko makubwa yaliyojitokeza kisiasa na kiuchumi katika miaka iliyopita na mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi na kiteknolojia yanayojikeza duniani kote katika nyakati za hivi karibuni.

3. Ili Tuweze Kupata Katiba nzuri Ipi ni Misingi ya Katiba katika nchi ya Kidemokrasia (Constitutional Principles)?

Kama ilivyo kawaida katika chombo kikuu kama hiki katika nchi, Katiba huweka misingi mikuu ambayo ndio

10 1110 11

rejea kuu katika uwekaji, usimikaji au uandishi wa katiba. Kama tujuavyo na tunavyoamini watanzania, nchi yetu inaendeshwa kwa kufuata utawala wa kidemokrasia. Kwa hali hiyo, miongoni mwa misingi ifuatayo ndio misingi mikuu ya Katiba;

a) Katiba yoyote ni waraka na muafaka wa kitaifa uliokubaliwa na wananchi wote.

b) Katiba ni waraka wa kisiasa, kiutawala na ndio msingi wa sheria zote.

c) Ndio msingi mkuu wa mamlaka ya utawala wa nchi kuwa mikononi mwa wananchi na serikali kuwajibika kwa wananchi.

d) Katiba huweka mgawanyo mzuri wa madaraka na mamlaka ya nchi kati ya mihimili ya utawala wa nchi yaani – Bunge, Mahakama na Serikali.

Kwa misingi hii basi ni wazi kwamba wananchi ndio wenye uwezo wa kuhalalisha na kurasimisha Katiba yeyote ya Nchi na ni wao wenye madaraka na mamlaka ya kujiamulia jinsi ya kuongozwa. Ni rai yetu kuwa misingi hii itazingatiwa katika kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika utungwaji wa Katiba mpya.

10 1110 11

4. Je, ni wajibu wa nani kushiriki katika kutunga Katiba?

Wananchi ndio pekee wanaowezesha kuandikwa na kuwekwa kwa misingi mikuu ya utawala, madaraka na majukumu ya mihimili ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama, misingi ya haki za msingi za wananchi, msimamo na mwelekeo wa taifa. Hivyo ni wajibu wa kila mwananchi (wakiwamo watoto wa rika zote wanaoweza kujieleza, vijana, wanawake, watu wenye ulemavu, na wazee) kushiriki katika mchakato wa kutungwa na kuandikwa kwa Katiba mpya.

5. Je, ni mambo yapi yanapaswa yawemo kwenye Katiba?

Sio mambo yote au kero zote za wananchi zinapaswa kuwemo ndani ya Katiba. Mambo mengine ambayo husumbua wananchi kama vile wizi au rushwa kuwemo kwenye Katiba bila kuonekana moja kwa moja (indirectly) bali kupitia misingi au misimamo yaa Katiba katika haki ya kumiliki mali au maadili na kushughulikiwa na sheria kama matukio ya uvunjaji wa sheria ambayo iko chini ya Katiba.

Kwa kifupi mambo yote ambayo kimsingi hayawezi

12 1312 13

kutungwa na au kubadilishwa kupitia chombo cha utungaji wa sheria, ambacho ni Bunge, huwekwa kwenye Katiba. Na ni mambo ambayo kwahiyo, huwa ni vigezo vya kuwezesha kutunga sheria mbalimbali ili kutafsiri jambo.

Hata hivyo, msingi wa kuyazuia na kuyawekea sheria hutokana na misingi ambayo haswa ni lazima iwe ndani ya Katiba na ni miongoni mwa mambo ambayo yanatoa mwongozo thabiti kwa kufuata misingi ya katiba. Kwa hiyo, mambo yafuatayo ni miongoni mwa mambo yanayopaswa yawemo ndani ya Katiba;

a) utangulizi (Preamble) na mwelekeo wa taifaUtangulizi huonesha umiliki wa nchi kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliokubaliana kujenga taifa la aina ya misingi fulani fulani kama vile taifa la ujamaa na kujitegemea, na ni taifa lenye misingi ya haki sawa kwa wote.

b) Mipaka ya nchi Ni muhimu kwa Katiba kuonesha mipaka ya nchi kwa kutaja pande zote za nchi kwa kusema mipaka yake ikitumia nchi au maeneo inayopakana nayo ili kutambulisha taifa lake.

c) Haki za binadamu na wajibu wa kila mwananchi,Hili ni jambo muhimu na ni la lazima katika ulimwengu wa sasa kwa Katiba kuonesha na kuweka bayana haki na

12 1312 13

wajibu wa msingi wa kila raia katika taifa kama taifa la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Dhana hii ni vyema ikawekwa ndani ya Katiba bila ya kuiwekea vipingamizi katika vifungu vingine vya Katiba hiyo hiyo.

d) Muundo wa Mihimili ya dolaKatiba ni vyema ionyeshe muundo wa mihimili ya dola na namna inavyokutana na kutoingiliana. Hii ni muhimu katika Katiba ili kuondoa dhana ya mhimili mmoja wa dola, kama vile serikali, kuzidi au kuingilia mihimili mingine ya dola. Hata hivyo ni vyema, kujadili kwa kina ili kuweka misingi ya uwiano (checks and balance) kuepusha hatari ya migongano ya kila mara kiutendaji. Mihimili ya dola huwa ni Serikali, Bunge na Mahakama.

i) SerikaliMhimili wa Serikali (executive) huundwa na viongozi mbalimbali akiwamo Rais na ambao upatikanaji wake huwekwa kwenye

Tunataka Katiba ieleze wazi

kuhusu mipaka ya serikali zinazounda muungano

14 1514 15

Katiba na kutafsiriwa na sheria mbalimbali zikiwamo sheria za uchaguzi na teuzi mbalimbali za viongozi wakuu waliokasimiwa madaraka ya kufanya hivyo na Katiba na au sheria za nchi. Katika utamaduni uliozoeleka, kiongozi wa mhimili huu huwa ndiye kiongozi wa nchi.

Kazi kubwa ya mhimili huu ni kusimamia utekelezaji wa Katiba, sheria, sera na taratibu mbalimbali za nchi ili kuongoza taifa na wananchi kwa ujumla katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kidemokrasia, kijamii na kiutamaduni.

ii) BungeMhimili wa Bunge huundwa na wabunge ambao upatikanaji wake uwekwa kwenye Katiba na kutafsiriwa na sheria mbalimbali za uchaguzi. Vivyo hivyo, mhimili huu huongozwa na kiongozi wa Bunge ambaye utaratibu wa upatikanaji wake uwekwa kwenye Katiba na kwa utamaduni uliozoeleka huitwa Spika.

Kazi kubwa ya mhimili huu ni kutunga, kurekebisha na au kufuta sheria za nchi. Hali kadhalika, Bunge hufanya kazi ya kujadili mikataba mbalimbali ya kimataifa ili kuridhia au kutoridhia utumikaji wake.

14 1514 15

iii) MahakamaMhimili wa mahakama huundwa na majaji, mahakimu ama wenyeviti mbalimbali wa mabaraza ya utoaji haki ambao upatikanaji wake huwekwa kwenye Katiba na kutafsiriwa na sheria mbalimbali za nchi. Vivyo hivyo, mhimili huu huongozwa na kiongozi wa mahakama ambaye utaratibu wa upatikanaji wake huwekwa kwenye Katiba na kwa utamaduni uliozoeleka huitwa Jaji Mkuu.

Kazi kubwa ya mhimili huu ni kutafsiri sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge pale zinapooneka kukiukwa dhidi ya mtu yeyote ikiwamo serikali na kutoa haki kwa mtu yeyote ambaye haki yake huonekana kuvunjwa, kurekebisha na au kufuta sheria za nchi. Kwa lugha nyingine hiki ndicho chombo pekee cha utoaji haki kwa wananchi.

e) Haki za Binadamu na Misingi yakeHaki za Binadamu na Misingi yake ni mambo muhimu kuwemo ndani ya katiba ili kuelezea ni haki zipi raia wote wa marika yote katika nchi ya Tanzania wanazo. Hali kadhalika huonesha ni wajibu upi katika kutekeleza haki raia wa Tanzania wanayo. Haki za binadamu na misingi yake huwa ni kielelezo tosha kwa wananchi kuonesha taifa lao linawajali kwa kadri gani dhidi ya uvunjanji wa haki za msingi za binadamu.

16 1716 17

f) usimamizi wa Haki za Binadamu na Maadili ya Taifa

Hivi ni vyombo muhimu kuwemo kwenye Katiba ili kutoa, kulinda na kutafsiri haki na misingi ya haki za binadamu pale inapoonekana kuelekea kuvunjwa au kukiukwa. Mfano wa vyombo kama hivyo ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Tume ya Maadili ya Viongozi. Hali kadhalika mahakama huingizwa katika sehemu hii kwani ndicho chombo cha juu cha usimamizi wa Haki za binadamu na maadili ya taifa.

g) ulinzi na usalama wa nchi na Mali za WananchiIli kulinda mipaka na usalama wa nchi yetu ni vyema vyombo vya ulinzi na usalama na namna ya uwepo wake, namna vitakavyoongozwa na ni nani amiri jeshi mkuu wa majeshi, viwemo ndani ya Katiba.

h) MuunganoKwa sababu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar unahusisha nchi mbili basi ni vyema swala la Muungano wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar likawepo kwenye Katiba. Na kwa sababu swala hili limeibua hisia tofauti na mjadala mrefu katika Nchi hii basi ni vyema pande zote za muungano zikaweka namna ya muonekano na utekelezaji wa muungano wetu.

16 1716 17

I) usawa wa JinsiaUsawa wa kijinsia ni swala nyeti katika maendeleo ya taifa lolote. Ni swala linaloingia katika sehemu zote kwa sababu wanawake na wanaume ni wabia sawa katika shughuli za maendeleo. Hivyo ni vyema suala hili likawemo kwenye Katiba ili kulinda usawa huu.

j) Tume ya uchaguziHii ni tume inayofanya kazi ya kusimamia chaguzi mbali mbali za kitaifa ili kuwezesha kuwepo kwa viongozi wa ngazi mbalimbali wanaochaguliwa kidemokrasia. Ili kuwezesha uchaguzi ulio huru na haki suala hili ni bora likawemo kwenye Katiba na kujadiliwa juu ya muundo wake uweje.

k) Ardhi na MipakaArdhi ndio rasilimali kuu inayo, pamoja na mambo mengine, wezesha taifa kuwepo kwa kutafsiri mipaka na namna ambayo raia wake wanaweza kuitumia rasilimali hiyo katika shughuli zao za kimaendeleo katika matabaka yote. Hivyo, matumizi sawa na umiliki wa rasilimali hii lazima uwepo ndani ya Katiba ili kutoa ulinzi kamili.

l) MazingiraSuala la uhifadhi na matumizi ya mazingira, ambayo kwa kiasi kikubwa hutoa taswira ya muonekano wa ardhi ya

18 1918 19

nchi, ni vyema likawemo ndani ya Katiba ili kutoa uhifadhi na matumizi ya mazingira kwa faida ya kizazi kijacho. Mazingira yakiharibika, ni wazi kuwa sura ya mazingira ikiharibika basi mipaka, ardhi na hali ya wananchi kimaisha ndani ya nchi itakuwa hatarini.

m) Mgombea BinafsiSuala la mgombea binafsi lilizuiliwa na Katiba iliyopo sasa japokuwa limezua mjadala mrefu mpaka sasa. Ili kuondoa mashaka yaliyopo ni vyema suala hili likajadiliwa kwa kina na kuwepo kwenye Katiba mpya ili kuonyesha sura ya ama kulikubali au kulikataa.

Ni maoni yetu kuwa Katiba mpya iruhusu mgombea binafsi ili kuendana sawia na haki ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa. Kitu cha kufanya ni kuweka vigezo vya hali ya juu na wazi ili kupata mtu muadilifu/muwajibikaji. Vigezo viwe vyenye nguvu ya kuhakikisha kuna udhibiti wa uadilifu na uwajibikaji kwa kila mgombea anayehitaji kugombea binafsi. Kwa mfano tunaweza kuwa na chombo huru cha kutathmini wagombea wote akiwamo mgombea binafsi.

n) Mamlaka ya Wananchi na ushiriki wao

Katika nchi nyingi za kidemokrasia katiba huonyesha mamlaka ya nchi kwa wananchi na kwamba madaraka yote

18 1918 19

ya umma, ikiwamo suala la uandishi na uwekaji wa Katiba, yanatokana na watu. Hivyo ni vyema suala hili likajadiliwa kwa kina ili kuonyesha nafasi ya wananchi katika utawala wa nchi.

Kwa mfano, ni mapendekezo yetu kuwa

o) usimamizi na utunzaji wa Mali na rasilimali ya Taifa

Suala la usimamizi na utunzaji wa mali ya taifa ni suala nyeti na ni vyema likawemo ndani ya Katiba ili kuondoa vishawishi vya aina yeyote vinavyoweza kufanywa na kundi dogo kwa nia binafsi bila kujali masilahi ya taifa.

6. Je, ni mambo yapi yanapaswa kujadiliwa ili yawemo au yasiwemo katika Katiba Ijayo?

a) Muundo wa Serikali na Mamlaka ya umma,

i) Rais na mfumo wa Urais

Katika muundo wa sasa huyu ndiye mkuu wa nchi na serikali na amiri jeshi mkuu na hupatikana kwa njia ya uchaguzi mkuu kupitia chama cha siasa. Ni muda muafaka kwa suala

20 2120 21

hili nyeti likajadiliwa na kuridhiwa kwa kina juu ya mfumo wake.

ii) Makamu wa Rais

Katika muundo wa sasa huyu ni msaidizi wa rais na anapatikana kupitia nafasi ya mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa kipindi cha miaka mitano mitano. Ni vyema suala hili nyeti likajadiliwa kwa kina juu ya muundo wake.

iii) Waziri Mkuu,

Katika muundo wa sasa huyu ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za serikali iliyomo madarakani na ni mteule wa rais ambaye hudhibitishwa na Bunge. Ni vyema suala hili nalo likajadiliwa kwa kina juu ya muundo wake ili kutoa mwelekeo uweje.

iv) Baraza la Mawaziri,

Katika muundo wa sasa hawa ni wasimamizi wa shughuli za serikali katika wizara na uteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kutoka miongoni mwa wabunge wa chama tawala. Ni vyema suala hili likajadiliwa muundo wake, kazi zake na uwezo wake uweje kikatiba.

20 2120 21

Ni maoni yetu kuwa, Baraza la Mawaziri liwe ni chombo kamili kinachosimamia utekelezaji wa sera na masuala yote ya mipango ya serikali na sio chombo cha kumshauri Rais ili kuongeza dhana ya uwajibikaji wa pamoja.

v) Viongozi wakuu waandamizi

Hawa ni viongozi mbalimbali wanaoteuliwa na Rais kwa mujibu wa sheria mbali mbali ili kushika nafasi mbalimbali za kitaifa kiuongozi wakiwamo makatibu wakuu, mabalozi, wasimamizi wa mashirika mbalimbali,

Wanakijiji wote tuna haki ya kutoa

maoni yetu juu ya Katiba mpya mheshimiwa

22 2322 23

wakurugenzi n.k. Suala hili ni vyema likajadiliwa kwa kina ili kutoa mwelekeo wa nanma ya upatikanaji wa viongozi waandamizi wa serikali.

vi) Wakuu wa Mikoa na Wilaya

Katika muundo wa sasa hawa ni wasimamizi wa shughuli za maendeleo na hali ya ulinzi na usalama katika mikoa na wilaya husika. Wakuu wa Mikoa na Wilaya ni wateule wa Rais na kimantiki humwakilisha Rais katika maeneo yao. Hivyo ni vyema nafasi hizi zikajadiliwa na wananchi ya namna zitakavyokuwa ili kuleta ufanisi katika maendeleo ya taifa.

Sisi tunapendekeza; Wakuu wa Mikoa na Wilaya wachaguliwe na wananchi kupitia uchaguzi mkuu ili kutoa fursa ya uwajibikaji kamili wa watendaji hawa katika ngazi zao na kusimamia kikamilifu uunganifu wa kazi za wabunge, madiwani na wakurugenzi katika mkoa au wilaya.

vii) Serikali za Mitaa

Katika muundo wa sasa tunazo serikali za mitaa ambazo dhana yake ni kurudisha utawala kwa wananchi. Wasimamizi wakuu wa serikali za mitaa ni wananchi kupitia wawakilishi wao katika ngazi za udiwani na watendaji wake

22 2322 23

huanzia ngazi ya wakurugenzi. Wakurugenzi wa ngazi hii ni wateule wa Rais. Tunatoa wito vile vile wa suala hili ni vyema likajadiliwa namna bora litakavyokuwa ili kutoa fursa kamili ya utendaji na madaraka kwa wananchi.

Ni maoni yetu kuwa dhana ya madaraka mikoani na serikali za mitaa iimarishwe zaidi kwa kuzipa nguvu Serikali za Mikoa, Wilaya na Mitaa/Vitongoji zinazowajibika moja kwa moja kwa wananchi.

b) Bunge na uhuru wake (Supremacy of Parliament)

Bunge ni chombo cha kutunga sheria kwa mujibu wa Katiba. Bunge ni chombo huru ambacho husimamia serikali katika utekelezaji wa sheria na kanuni mbalimbali zilizowekwa kuiongoza nchi. Kwa muundo wa sasa Bunge huongozwa na Spika, naibu Spika na Wenyeviti wake.

Katika hali hiyo hiyo, tunatoa wito kujadili namna ya upatikanaji wa watendaji wa Bunge wakiwemo wabunge wenyewe, Katibu wa Bunge na Wakurugenzi wa taasisi hiyo ili kutoa taswira halisi ya uhuru wa Bunge na kazi zake.

24 2524 25

c) Mahakama na uhuru wake (Independence of the Judiciary)

Huu pia ni mhimili mmojawapo wa dola ambao unasimamia utekelezwaji wa haki na wajibu kama ilivyo katika katiba ya nchi na sheria mbalimbali zinazotungwa na Bunge. Kama tujuavyo kazi kubwa ya mahakama ni kutoa tafsiri ya sheria bila kushurutishwa, upendeleo, na uoga wa aina yeyote. Ili kuhakikisha hilo linakuwepo basi ni vyema suala hili likajadiliwa hasa hasa ili kuwezesha uhuru kamili wa Mahakama.

Katika kuhakikisha uhuru kamili wa Mahakama, tunapendekeza kwamba, Rais asihusike na uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu bali wateuliwe na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa mfumo wa mashindano ya wazi na pia wathibitishwe na Bunge katika vikao ambavyo umma unahusika kikamilifu ‘public hearing’.

Ili kudumisha uhuru wa mahakama Rais asiwe mmoja wa wasimamizi wa utendaji wa mhimili wa Mahakama, isipokuwa awe tu na uwezo wa kutoa msamaha kwa baadhi ya makosa ‘executive prerogatives of mercy’ na uwezo huu pia wabidi kujadiliwa ili kuona njia bora ya ufanisi wake. Kwa hiyo hata Jaji Kiongozi au Jaji mwingine yeyote atashindwa kufanya kazi au anahitaji kuchukuliwa hatua

24 2524 25

za kinidhamu, maamuzi yote yafanywe na Jaji Mkuu kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi wa mahakama.

d) Madaraka ya raisNi maoni yetu kwa ujumla kuwa wananchi wa Tanzania wajadili namna ya kumpunguzia Rais mzigo ili kutekeleza dhana ya utawala wa pamoja na hivyo kupunguza lawama na utegemezi wa kuendesha taifa kupitia kwa taasisi moja. Kwa mfano kazi ya uteuzi wa majaji kama ilivyo sasa ingeweza kuachiwa Tume ya Mahakama ikifanya hivyo kupitia mapendekezo tuliyoyatoa juu ya upatikanaji wa majaji. Hali kadhalika upatikanaji wa wakuu wa mikoa na wilaya ungeweza kufanyika kupitia chaguzi kuu za kitaifa.

e) nafasi ya Wananchi Katika umiliki wa rasilimali za nchiSuala la nafasi ya wananchi katika kumiliki rasilimali limekuwa ni moja ya mambo yaliyozua mjadala mkubwa katika taifa kutokana na wananchi kukosa nafasi ya kujadili mambo muhimu yanayohusu mikataba ya madini na mikataba mingine mbalimbali katika mashirika ya umma. Hivyo ni wito wetu kuwa suala hili ni vyema likajadiliwa ili kupata msimamo wa kitaifa katika suala hili.

Hata hivyo ni pendekezo letu kuwa wananchi wapate nafasi ya kujadili umiliki wa rasilimali zao moja kwa moja au kwa

26 27

kupitia wawakilishi wao na sio kuiachia serikali peke yake kufanya maamuzi katika masuala nyeti ya rasilimali za kitaifa.

f) Vipindi vya Mbunge Kutumikia JimboKama ilivyo sasa, muda wa mbunge kutumikia wananchi wake hauna ukomo. Hali hii, pamoja na kutoa uwiano sawa wa kuchaguliwa muda wa uchaguzi unapofika, lakini unaminya fursa sawa kwa wananchi wengine waliokuwa nje ya bunge kufanya hivyo kutokana na mambo mengi likiwemo suala la vipato. Hivyo ni muhimu kujadili vipindi maalumu vya wawakilishi kama ilivyo hivi sasa kwa upande wa Rais ili kutoa mwanya na nafasi ya demokrasia kwa watu wengine zaidi.

g) nafasi ya Wabunge wa Viti MaalumuHali kadhalika ni vyema kujadili namna ya upatikanaji wa wabunge wa viti maalumu. Wito wetu, tunatoa rai kujadili kama bado tunahitaji nafasi ya wabunge wa viti maalumu bungeni na namna gani sahihi itumike ili kuwapata wabunge wa viti maalumu katika uwiano sawa wa kimchuano kwa wabunge wengine wanaopatikana kutoka majimboni.

h) uwajibikaji wa Wabunge kwa wapiga kuraHali ilivyo sasa mbunge hawezi kuwajibishwa na wananchi pindi anapochaguliwa mpaka nyakati za uchaguzi

26 27

mwingine. Badala yake, chama kilichomteua au Msajili wa vyama ndio wanaoweza kufanya hivyo. Hali hii sio tu inawanyima haki wananchi kumsimamia mwakilishi wao, bali pia inawafanya wawakilishi hawa wasijali shida za wananchi waliowachagua. Hivyo ni wito wetu kuwa suala hili lijadiliwe na kutoa mwelekeo wa namna gani wananchi wawajibishe wawakilishi wao bungeni kabla ya uchaguzi.

i) Muundo wa Tume wa uchaguziTume ya Uchaguzi imo ndani ya Katiba ya sasa, hata hivyo, ni maoni yetu kuwa muundo wa Tume ya uchaguzi uangaliwe upya ili kukiweka chombo hiki kuwa huru. Vile vile katika nyongeza zingine, ni maoni yetu ya jumla katika sehemu hii kuwa ni vizuri wapiga kura au wagombea au mwananchi awe na haki ya kupinga matokeo Mahakamani.

Ni maoni yetu pia kuwa Uwezo wa kufungua shauri Mahakamani (‘locus standi’) kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Rais au mwenendo wake uwe kwa mgombea au chama kilichosimamisha mgombea wa kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano tu ili kupunguza uwezekano wa mashauri mengi yasiyo na mashiko kisheria kufunguliwa Mahakamani.

j) nafasi ya Mgombea BinafsiKama tulivyotangulia kusema hapo awali, suala la mgombea binafsi limekuwa ni jambo kubwa lililoleta mijadala katika

28 2928 29

taifa. Ili kuondoa mashaka yaliyopo ni vyema suala hili likajadiliwa kwa kina na kuwepo kwenye Katiba mpya ili kuonyesha sura ya ama kulikubali au kulikataa.

Hata hivyo, ni maoni yetu kuwa Katiba mpya iruhusu mgombea binafsi ili kuendana sawia na haki ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa. Kitu cha kufanya ni kuweka vigezo vya hali ya juu na wazi ili kupata mtu muadilifu/muwajibikaji. Vigezo viwe vyenye nguvu ya kuhakikisha kuna udhibiti wa uadilifu na uwajibikaji kwa kila mgombea anayehitaji kugombea binafsi. Kwa mfano tunaweza kuwa na chombo huru cha kutathmini wagombea wote akiwamo mgombea binafsi.

k) Masilahi na marupurupu ya ViongoziHili ni suala jingine nyeti ambalo pamoja na mambo mengine ya kujadili, ni vyema pia likajaliwa ili kuweka uwiano sawa kwa viongozi wakiwemo viongozi wa umma. Hali hii itaondoa misuguano iliyomo kati ya viongozi na wananchi. Kwa mfano, kunaweza kukaundwa Tume ya Masilahi ya viongozi itakayoshughulikia muundo na uwiano wa mishahara, posho, marupurupu na haki zingine za watumishi wa umma na binafsi.

28 2928 29

7. Je, upi mwongozo bora wa kufuata katika utungaji wa Katiba?

Kuna taratibu mbalimbali zinazotumika katika uandishi wa Katiba. Miongozo hiyo hutegemea sana aina ya utawala unaotumika katika nchi inayoandika Katiba kwa wakati huo. Nchi yetu, inafuata utawala wa kidemokrasia. Hivyo, katika uandishi wa Katiba katika nchi inayofuata utawala wa kidemokrasia hatua zifuatazo ni muhimu kufuatwa;

i) Kuundwa kwa Tume ya Katiba (Constitutional Commission)Hiki ni chombo huru ambacho, kutokana na uzoefu huundwa na Rais wa nchi. Tume hii uapishwa na kupewa hadidu za rejea zitakazotumika kuongoza shughuli zote za mchakato wa uundwaji wa Katiba ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mawazo kutoka kwa wananchi, uandikaji wa rasimu ya Katiba, kuwasilisha rasimu hiyo kwenye Bunge la Katiba, kuwasilisha rasimu kwa ajili ya upigaji kura ya maoni (referendum) ya kuunga au kukataa Rasimu ya Katiba.

ii) Mkutano Mkuu wa Wananchi (National Constitutional Convention)Huu ni mkutano ambao wajumbe wake huchaguliwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge ama kwa mujibu wa maelezo ya Katiba.

30 3130 31

Kazi kubwa ya mkutano huu ni kutengeneza, kurekebisha au kupitia Katiba na kutoa maoni ya jinsi ya kuiboresha. Lengo kuu la mkutano huu ni kuleta makubaliano na umoja wa kitaifa.

Hata hivyo ni bora kueleza wazi kwamba utaratibu huu haumo ndani ya Katiba yetu wala sheria mbalimbali za Bunge

iii) Bunge la Katiba (Constituent Assembly)

Hili ni Bunge linalochaguliwa na wananchi mahususi kwa ajili ya utungaji wa Katiba. Idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba huwa ni wengi ukilinganisha na Bunge la kawaida. Kwa maana nyingine wabunge wa Bunge la sasa pamoja na wengine kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii wanaweza kutengeneza Bunge Maalumu la Katiba.

iv) Kura ya Maoni (Referendum)

Kura ya maoni, yaani (referendum) ni kura ya udhibitisho na maamuzi ambayo hupigwa na wananchi kuamua kama Rasimu ya Katiba iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba itumike au isitumike. Kwa kawaida wananchi, kupitia mfumo wa Tume ya Uchaguzi hupiga kura ya “ndio” au “hapana”. Endapo kura ya “ndio” itashinda, Rais wa nchi atatia saini

30 3130 31

katika Katiba mpya na kusubiri kutangazwa kwa tarehe itakapoanza kutumika.

v) Tarehe ya kuzindua Katiba (Promulgation)

Hii ni tarehe ya uzinduzi au tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba mpya. Siku hii vyombo vyote vya zamani hukoma na kuashiria kuanza kutumika kwa vyombo vipya vilivyotajwa katika Katiba mpya.

Hitimisho

Kama viongozi wetu wa kitaifa wanavyoendelea kusisitiza, sisi pia tunatoa rai kwa jamii ya watanzania wa rika zote, fani zote, dini zote, makabila yote, wenye vyama vya siasa na wasio navyo na wale wote wenye mapenzi mema na nchi hii, kushiriki kikamilifu mjadala wa katiba mpya bila woga ili taifa hili lipate Katiba mpya kwa faida ya watanzania wote. Huu ni wajibu wetu wa kiraia na inapaswa tuutimize ili kuweza kujenga mustakabali wa taifa letu na vizazi vijavyo.

32

Kwa maelezo zaidi wasiliana na TIFPA:493 Regent Estate Mikocheni | Old Bagamoyo Road

P. O. Box 72650 | Dar es Salaam - Tanzania, Tel: +255 22 732 995375