waraka wa sera za uchumi jumla 2011 swahili - tanzania...6. pamoja na mfumuko wa bei kuendelea kuwa...

23
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MUHTASARI WA MFUMO WA SERA ZA JUMLA ZA UCHUMI NA MAENDELEO YA JAMII KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2011/12-2015/16 Imetolewa na Wizara ya Fedha Mei, 2011

Upload: others

Post on 01-Feb-2021

4 views

Category:

Documents


0 download

TRANSCRIPT

  • JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

    MUHTASARI WA MFUMO WA SERA ZA JUMLA ZA UCHUMI NA MAENDELEO YA

    JAMII KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2011/12-2015/16

    Imetolewa na Wizara ya Fedha

    Mei, 2011

  • 2

    MUHTASARI WA MFUMO WA SERA ZA JUMLA ZA UCHUMI NA MAENDELEO YA

    JAMII KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2011/12-2015/16

  • 3

    YALIYOMO

    UTANGULIZI ........................................................................................................................................ 1 MAPITIO YA MWENENDO WA UCHUMI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA 2010 .............................. 1 Mwenendo wa Uchumi wa Dunia .................................................................................................. 1 Ukuaji wa Pato la Taifa ................................................................................................................... 2 Mwenendo wa Bei ........................................................................................................................... 2 Mapato na Matumizi ya Serikali ..................................................................................................... 4 Deni la Taifa .................................................................................................................................... 5 Ujazi wa Fedha na Karadha ........................................................................................................... 6 Maboresho ya Sekta ya Fedha ....................................................................................................... 7 Sekta ya Nje .................................................................................................................................... 9 Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kikanda ............................................................................................ 9 Uendelezaji wa Sekta Binafsi ......................................................................................................... 9 Tathmini ya Dira na Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati na Mrefu ............................... 10 MKUKUTA na Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ......................................................... 10 Utafiti wa Afya na Demografía 2010-TDHS ................................................................................ 11

    MASUALA MUHIMU YA KISERA YALIYOJITOKEZA MWAKA 2010/11 ........................................... 12 Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) .............................................. 13

    Vipaumbele Vya Kisekta ................................................................................................................... 14 MISINGI NA MALENGO YA UCHUMI JUMLA NA MAENDELEO YA JAMII 2011/12-2015/16 ...... 19 HITIMISHO ........................................................................................................................................ 20

  • 1

    UTANGULIZI

    1. Taarifa hii inatokana na uchambuzi wa mwenendo wa viashiria muhimu katika

    maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na unyambuaji wa masuala muhimu

    yaliyojitokeza nchini, kikanda na duniani katika mwaka 2009/10 hususan suala la

    ukame uliojitokeza nchini mwishoni mwa mwaka 2010 na athari zake kwa sekta

    mbalimbali za kiuchumi kama vile katika kilimo, nishati na uzalishaji viwandani na

    kupanda kwa kasi bei za mafuta katika soko la dunia. Aidha, taarifa hii imezingatia

    maamuzi ya msingi ya Serikali hasa suala la kuandaa mpango kwa kuzingatia mfumo

    wa miaka mitano. Pia inalenga katika kukabiliana na athari za upatikanaji wa

    umeme wa uhakika; kutengemaza na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi;

    kuboresha maendeleo ya jamii; na kupunguza umaskini katika miaka mitano ijayo.

    Vile vile, taarifa hii inazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo imefanyiwa

    mapitio hivi karibuni, Malengo ya Maendeleo ya Milenia, Awamu ya Pili ya Mkakati

    wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA II), na vipaumbele

    vya uwekezaji vilivyoainishwa katika Mwongozo wa Mpango na Bajeti 2011/12

    _2015/16.

    MAPITIO YA MWENENDO WA UCHUMI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA

    2010

    Mwenendo wa Uchumi wa Dunia

    2. Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha Duniani, uchumi wa dunia umekua

    kwa asilimia 5 mwaka 2010 ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 0.6 uliotokea

    mwaka 2009 kutokana na msukosuko wa masoko ya fedha na mitaji uliotokea

    mwaka huo. Kiwango kikubwa cha ukuaji wa uchumi mwaka 2010 kilitokana na

    kuongezeka kwa kiasi kikubwa kwa mahitaji ya walaji katika nchi za Marekani na

    Japan, pamoja na hatua za makusudi zilizochukuliwa na nchi mbalimbali kuweka

    vichocheo vya kibajeti na kifedha vya kukuza uchumi (“stimulus package”). Kiwango

    cha ukuaji wa uchumi katika bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kilikuwa

    asilimia 5 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 2.8 mwaka 2009 kutokana na

    kuanza kuimarika kwa bei za bidhaa zinazouzwa nje na kuongezeka kwa mahitaji

  • 2

    katika soko la ndani. Changamoto bado ipo hususan ikizingatia kuwa nchi nyingi

    katika ukanda huu zinatemegea misaada na mikopo kutoka nchi zilizoendelea

    ambazo zimepunguza bajeti zao ili kuziba nakisi iliyopatikana wakati wa msukosuko.

    Hali kadhalika, tetemeko la ardhi lililotokea nchini Japan linatarajia kuathiri uchumi

    wa dunia na upatikanaji wa mikopo na misaada kwa nchi zinazoendelea ingawa

    taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa Japan itaendelea kutoa misaada yake kama

    ilivyopangwa licha ya matatizo iliyoyapata.

    Ukuaji wa Pato la Taifa

    3. Ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulikuwa asilimia 7.0 mwaka 2010 sawa na

    ilivyokadiriwa ikilinganishwa na asilimia 6.0 mwaka 2009. Ukuaji huu ulitokana na

    kuongezeka kwa viwango vya ukuaji katika kilimo kufuatia kuwepo kwa hali nzuri ya

    hewa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2009/10, na hatua za serikali za kutoa

    ruzuku ya pambejeo za kilimo na kuimarika kwa miundombinu ya umwagiliaji na ya

    barabara na utekelezaji wa mpango wa dharura wa kunusuru uchumi (rescue

    package). Sekta zilizochangia ukuaji huu ni pamoja na biashara na matengenezo,

    kilimo na ufugaji, usafirishaji na mawasiliano na uzalishaji viwandani.

    Mwenendo wa Bei

    4. Ofisi ya Taifa ya Takwimu ilibadilisha mwaka wa kizio wa Fahirisi za Bei za

    Taifa kutoka mwaka 2001 kuwa mwaka 2007 kwa kutumia matokeo ya Utafiti wa

    Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi wa mwaka 2007. Mabadiliko haya yalifanywa

    kwa kutumia makundi yaliyokubalika Kimataifa yanayoitwa Mchanganuo wa Matumizi

    Binafsi “Classification of Individual Consumption by Purpose (COICOP)” na maeneo

    ambayo mara nyingi jamii hununua bidhaa au hupata huduma mbalimbali (Outlets).

    Mfumo huu mpya wa ukokotoaji wa fahirisi za bei unatumia wastani wa kijiometria

    (geometric mean) badala ya wastani wa kawaida (arithmetic mean) katika

    kutengeneza Fahirisi za Bei katika ngazi za mwanzo kama inavyokubalika kimataifa

    kwa ulinganisho. Mizania mpya zinajumuisha matumizi ya kaya zote binafsi kutoka

    mijini na vijijini wakati mizania iliyokuwa inatumika zamani ilijumuisha kaya binafsi

    za maeneo ya mijini tu. Bidhaa na huduma mbalimbali za jamii zimeboreshwa kwa

  • 3

    kujumuisha bidhaa na huduma mpya na kuondoa zile ambazo zimeonesha

    kutotumiwa sana na walaji kwa sasa.

    .

    5. Mfumo huu wa kutumia wastani wa kijiometria ulianza kutumika Oktoba 2009,

    kwa kipindi cha miezi 12 ulitoa mfumuko wa bei wa asilimia 4.2 kwa mwezi Oktoba

    2010. Hii ilikuwa ni badiliko la asilimia 0.3 ikilinganishwa na mfumuko wa bei

    uliotumia wastani wa kawaida wa mwezi Septemba 2010 ambao ulikuwa asilimia

    4.5. Aidha, kama wastani wa kawaida ungetumika, mfumuko wa bei ungekuwa

    asilimia 4.1 kwa mwezi Oktoba 2010 ikilinganishwa na asilimia 4.2 kwa kutumia

    wastani wa kijiometria. Kwa wastani, mfumo wa awali unaonesha kutoa mfumuko

    wa bei ambao hautofautiani sana na unaotolewa kwa kutumia mfumo mpya.

    6. Pamoja na mfumuko wa bei kuendelea kuwa tarakimu moja, umekuwa na

    mwelekeo wa kupanda hususan katika robo ya kwanza ya mwaka 2011. Mfumuko

    wa bei umeongezeka kutoka asilimia 5.6 kwa kipindi kilichoishia Desemba 2010 hadi

    asilimia 6.4 Januari 2011 na kuendelea kupanda hadi asilimia 8.6 mwezi Aprili 2011.

    Kasi hiyo ya ongezeko la bei ilitokana hasa na kuongezeka kwa wastani wa fahirisi ya

    bei za umeme, gesi, chakula na vinywaji visivyo na kilevi.

    7. Mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa mwaka ulioishia

    Aprili 2011 ulipungua kufikia asilimia 5.7 kutoka asilimia 6.3 Machi 2011. Aina hii ya

    Fahirisi haijumuishi vyakula vilivyoliwa majumbani na hotelini, vinywaji baridi, petroli,

    dizeli, gesi, mafuta ya taa, mkaa na umeme. Vyakula na nishati vina sifa ya kuwa na

    bei ambazo hubadilika mara kwa mara na kisera inakuwa vigumu kusimamia bei hizi.

    Hivyo vikiondolewa kwenye Fahirisi ya bidhaa na huduma zote hubakia Fahirisi

    ambayo ina mwelekeo imara kisera hususan kwa kutumia sera za fedha na mapato

    na matumizi kusimamia mwenendo wa bei. Mfumuko wa bei wa nishati uliongezeka

    kufikia asilimia 22.1 na wa vyakula ulifikia asilimia 9.2 Aprili 2011 ikilinganishwa na

    asilimia 17.2 na 8.3 Machi 2011 kwa mtiririko huo.

  • 4

    Mapato na Matumizi ya Serikali

    8. Mapato ya ndani yaliongezeka kwa asilimia 8.2 mwaka 2009/10 kufikia

    shilingi bilioni 4,661.540 kutoka shilingi 4,293.074 bilioni mwaka 2008/09. Hata

    hivyo, kiasi hicho kilichokusanywa ni pungufu ya makadirio kwa asilimia 8.8 kwa

    mwaka 2009/10. Wastani wa makusanyo kwa mwezi unaonesha kuwa mapato ya

    ndani yalikuwa yakiongezeka mfululizo kutoka wastani wa shilingi bilioni 174.8 kwa

    mwezi mwaka 2005/06 hadi shilingi bilioni 388.5 kwa mwezi mwaka 2009/10.

    Misaada ya nje katika mwaka 2009/10 ilikuwa shilingi bilioni 1,405.3, mikopo ya nje

    ilikuwa shilingi bilioni 1,379.6 na mikopo ya ndani ilikuwa shilingi bilioni 568.5. Katika

    kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2010/11 (Julai – Disemba 2010), mapato ya

    ndani yakijumuisha mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 2,778.9, ikiwa ni

    asilimia 10 chini ya makisio ya shilingi bilioni 3,079.1 kwa kipindi hicho. Upungufu

    huu ulitokana hasa na athari za msukosuko wa kiuchumi duniani. Pamoja na

    kupungua kwa mapato ikilinganishwa na makisio, mapato yaliyopatikana katika

    kipindi hicho yalikuwa asilimia 17.6 zaidi ya mapato yaliyokusanywa katika kipindi

    kama hicho mwaka 2009/10.

    9. Matumizi ya Serikali yalifikia shilingi bilioni 8,173.7 mwaka 2009/10 sawa na

    asilimia 90.0 ya makadirio. Matumizi ya maendeleo yalikuwa asilimia 8.0 chini ya

    lengo hasa kutokana na kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi kulikosababishwa na

    baadhi ya Wizara, Idara, Mikoa na Halmashauri kuchelewa kukamilisha taratibu za

    ununuzi na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za miradi. Matumizi ya kawaida pia

    yalikuwa asilimia 8.0 chini ya malengo. Katika kipindi cha Julai - Desemba 2010,

    matumizi ya Serikali yalifikia shilingi bilioni 5,052.7 ikiwa ni asilimia 83.4 ya makisio

    ya matumizi ya shilingi bilioni 6,058.0. Matumizi ya maendeleo na ya kawaida

    yalikuwa asilimia 19.0 na 15.8 chini ya makadirio kwa kipindi hicho kwa mtiririko

    huo. Kupungua kwa matumizi hayo kunatokana na upungufu wa mapato katika

    kipindi hicho.

  • 5

    Deni la Taifa

    10. Deni la Taifa liliongezeka kwa asilimia 6.1 hadi Dola za Kimarekani milioni

    11,380.2 katika kipindi kilichoishia Desemba 2010 kutoka Dola za Kimarekani milioni

    10,725.92 Desemba 2009. Kati ya deni hilo, Dola za Kimarekani milioni 8,363.3

    zilikuwa ni deni la nje, sawa na asilimia 73.5 ya deni lote na zilizobaki ni deni la

    ndani. Kati ya kiasi hicho cha deni la nje, Dola za Kimarekani milioni 7,699.6

    (asilimia 91.7) ni bakaa ya deni (Disbursed Outstanding Debt_DOD) na kiasi

    kilichobaki cha Dola za Kimarekani milioni 693.7 ni malimbikizo ya riba. Kati ya kiasi

    hicho cha deni la nje, Dola za Kimarekani milioni 1,863.4 (22.3%) ni deni la sekta

    binafsi na kiasi kilichobaki cha Dola za Kimarekani milioni 6,529.6 zilikuwa ni deni la

    sekta ya umma. Deni la ndani hadi kufikia Desemba 2010 lilikuwa shilingi bilioni

    4,385.4, ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.3 ikilinganishwa na kipindi kama hicho

    mwaka 2009. Asilimia 62 ya deni hili ilikuwa ni hati fungani za Serikali. Ongezeko la

    deni la Taifa limetokana na malimbikizo ya riba ya deni la nje hasa kwenye nchi

    zisizo wanachama wa kundi la Paris ambazo hazijatoa misamaha ya madeni

    kulingana na makubaliano, mikopo mipya ya ndani na nje kwa ajili ya kugharamia

    miradi mbalimbali ya maendeleo na kushuka kwa thamani ya shilingi. Malipo ya deni

    la nje katika kipindi cha nusu mwaka ulioishia Desemba 2010 yalikuwa shilingi

    bilioni 62.8, na kati ya hizo, shilingi bilioni 38.8 zikiwa ni malipo ya riba. Malipo ya

    deni la ndani kwa nusu mwaka ulioishia Desemba 2010 yalikuwa shilingi bilioni

    632.4. Kati ya hizo, shilingi bilioni 424.7 zilitumika kulipia dhamana za Serikali

    zilizoiva kwa utaratibu wa kukopa na kulipia dhamana zilizoiva (rollover) na shilingi

    bilioni 107.7 zilikuwa ni malipo ya riba. Katika kutekeleza Mkakati wa Deni la Taifa,

    Serikali imeendelea kusimamia kwa umakini deni la Taifa kwa kukopa zaidi kutoka

    vyanzo nafuu kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na kuchambua athari

    zinazotokana na mikopo mipya. Kwa mujibu wa tathmini ya kuangalia uhimilivu wa

    deni (Debt Sustainability Analysis) iliyofanyika mwezi Oktoba 2010 inaonesha kuwa

    viashiria muhimu vya madeni ni himilivu na linahimilika. Kwa maana nyingine ni

    kuwa, tunakopesheka kwa kuzingatia uwezo wetu wa kulipa na kufuata sheria ya

    Mikopo, Dhamana na Misaada ya mwaka 1974 (iliyorekebishwa mwaka 2004) na

    kanuni zake.

  • 6

    Ujazi wa Fedha na Karadha

    11. Katika kipindi cha mwaka 2010/11, sera ya fedha ililenga kuwa na kiwango

    cha ongezeko la ujazi wa fedha kinachoenda sambamba na mahitaji halisi ya

    uchumi, kasi ya upandaji bei, ongezeko la mikopo ya ndani lisiloathiri uzalishaji mali

    na ambalo linalingana na malengo ya ujazi wa fedha, na kuwa na akiba ya fedha za

    kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje

    kwa kipindi kisichopungua miezi mitano. Hadi Desemba 2010, ujazi wa fedha kwa

    tafsiri pana (M2)1 ulikua kwa asilimia 21.8 kiwango ambacho kilikuwa chini ya

    kiwango cha ukuaji cha asilimia 26.3 kwa mwaka ulioishia Juni, 2010. Hata hivyo,

    kiwango hicho kilikuwa juu kidogo, kikilinganishwa na makadirio ya kiwango cha

    asilimia 20.8 hadi Desemba 2010. Katika kipindi hicho, M3 ilikua kwa asilimia 25.4,

    ikilinganishwa na asilimia 25.1 kwa mwaka ulioishia Juni, 2010, na hali kadhalika

    ikilinganishwa na makadirio ya ukuaji wa asilimia 23.5 ifikapo Desemba 2010. Kasi

    ya ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi ilitokana na kasi ya ongezeko la

    amana katika fedha za kigeni, ambapo ziliongezeka kwa asilimia 23.3 kutoka dola za

    kimarekani milioni 1,657.3 mwezi Desemba 2009 hadi dola milioni 2,043.6 mwezi

    Desemba 2010, pamoja na kuimarika kwa dola ya kimarekani dhidi ya sarafu

    nyingine. Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuongezeka hadi kufikia Dola za

    Kimarekani milioni 3,948.0 Desemba 2010, kiasi ambacho kinatosha kuagiza bidhaa

    na huduma nje kwa muda wa miezi 6.3. Kiwango cha ukuaji wa mikopo inayotolewa

    kwa sekta binafsi kiliendelea kuongezeka na kufikia asilimia 20.0 Desemba 2010

    kutoka asilimia 16.3 Juni 2010. Hii inatokana na kuanza kujengeka kwa imani ya

    mabenki dhidi ya sekta binafsi kufuatia kuanza kuimarika kwa hali ya uchumi wa

    dunia baada ya kupitia katika kipindi cha msukosuko wa Masoko ya Fedha na Mitaji.

    Tofauti kati ya viwango vya riba vinavyotozwa kwenye mikopo na vile vinavyotolewa

    kwenye amana kama faida vimeendelea kuwa juu, licha ya kuongezeka kwa

    ushindani katika sekta ya kibenki. Hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana

    kwa taarifa sahihi za wakopaji (credit reference data bank) na kutokuwepo kwa

    taasisi ya utoaji wa taarifa sahihi za waombaji mikopo (Credit Rerefence Bureau)

    1 M0 ni fedha zilizo kwenye mzunguko nje ya mabenki; M1=M0 + amana za hundi; M2 = M1 + amana za muda maalum + amana za

    akiba; M3 = M2 + amana za fedha za kigeni (foreign deposits)

  • 7

    nchini. Aidha, gharama kubwa za kufanya biashara kutokana na miundombinu

    hafifu, nazo zimechangia kuongeza viwango vya riba vinavyotozwa kwenye mikopo.

    Maboresho ya Sekta ya Fedha

    12. Serikali ilianza kutekeleza Awamu ya Pili ya Mageuzi katika Sekta ya fedha

    mwaka 2006/07. Mageuzi haya ni pamoja na kuimarisha sekta ya mabenki kwa

    lengo la kuimarisha mazingira ya ushindani katika utoaji wa huduma, kuimarisha

    masoko ya fedha, mageuzi katika usimamizi wa uwekezaji rasilimali kwa Mifuko ya

    Hifadhi za Jamii, kuboresha utoaji wa mikopo ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na

    mikopo kwa ajili ya kilimo,mikopo ya makazi (Mortgage Finance) na Mikopo ya

    karadha (Finance Leasing) na kuboresha taarifa za wakopaji kwa kuanzisha chombo

    cha kutoa taarifa hizo (Credit Reference Bureau). Hadi sasa mafanikio makubwa

    yamekwisha patikana ikiwa ni pamoja na Sekta ya fedha nchini kuendelea kukua

    kwa kasi nzuri. Kulingana na vigezo na viashiria vya uimara wa sekta ya fedha,

    mabenki yote nchini yanakidhi viwango vya mtaji unaoweza kuhimili madai (capital

    adequacy ratio), yana ukwasi wa kutosha kukidhi malipo kwa wateja (liquidity ratio)

    na ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi wa kuridhisha. Aidha, mfumo wa malipo

    nchini umeboreshwa na kuleta ufanisi katika kutekeleza sera za kiuchumi na fedha.

    Mfumo wa malipo baina ya mabenki nchini ulioanza kutumika rasmi mwaka 2004

    umeendelea kuboreshwa kwa kuhakikisha kwamba unatumika kurahisisha

    ukusanyaji wa mapato ya Serikali na baadhi ya malipo yanayofanywa na serikali. Hali

    kadhalika, mfumo wa malipo ya hundi umeendelea kuboreshwa (kwa kutumia TISS2)

    na kupunguza muda wa malipo ya hundi.

    13. Katika mwaka 2010, Serikali iliendelea na maboresho ya sekta ya fedha

    ambapo Kanuni zitakazotumika katika masuala ya taarifa za mikopo zilichapishwa

    kupitia Tangazo la Serikali namba 177 na 178 la mwaka 2010 na kuanza kutumika

    rasmi mwezi Oktoba 2010. Hali kadhalika, Serikali ilihitimisha mchakato wa

    uanzishwaji wa Mamlaka ya Kusimamia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (Social Security

    Regulatory Authority - SSRA) ambayo jukumu lake ni kukuza ufanisi na kuongeza

    2 TISS ni Tanzania Interbank Settlement System

  • 8

    ushindani katika mifuko ya pensheni na hivyo kuchangia zaidi kwenye ustawi wa

    uchumi. Aidha, serikali inaendelea na mchakato wa kuboresha taratibu za mafao ya

    mifuko yote ya hifadhi ya jamii ili ilingane na iwe endelevu. Aidha, maboresho

    mengine ni pamoja na kuiwezesha Benki ya Rasilimali Tanzania kutoa mikopo ya

    muda mrefu. Serikali pia inandaa mfumo kabambe wa kisera na kisheria wa

    utaratibu wa upatikanaji na utoaji wa mikopo ya muda mrefu.

    14. Licha ya mafanikio yaliyopatikana chini ya programu ya uboreshaji wa sekta

    ya fedha, zipo changamoto ambazo Serikali itaendelea kutafuta ufumbuzi wake.

    Changamoto kubwa ni viwango vikubwa vya riba kwenye mikopo ambavyo

    vimeendelea kutozwa na benki zetu ikilinganishwa na faida ndogo inayolipwa kwa

    amana (interest rate spread). Serikali inaendelea na mkakati wa kuimarisha soko la

    dhamana za serikali ili kufikia viwango halisi vya riba vinavyotokana na nguvu za

    soko na visivyobadilika mara kwa mara. Hali kadhalika, Serikali inaendelea kubuni

    mikakati yenye lengo la kuimarisha miundombinu katika sekta ya fedha pamoja na

    kuimarisha mazingira ya ushindani katika sekta hiyo. Vile vile, changamoto nyingine

    ni ufinyu wa mikopo ya muda mrefu pamoja na wananchi wengi, hasa wa vijijini,

    kutofikiwa na huduma za kibenki. Hata hivyo, wananchi wengi zaidi hasa wa vijijini

    ambako huduma za kawaida za kibenki zilikuwa hazipatikani wameanza kunufaika

    kutokana na ongezeko la matumizi ya simu za mkononi katika kupata huduma za

    kifedha. Hadi mwezi Mei mwaka 2010, kulikuwa na zaidi ya watumiaji milioni 6 wa

    huduma hizi. Baadhi ya huduma zinazopatikana ni pamoja na kutuma fedha kwa

    ndugu na jamaa, kulipa ankara za maji (DAWASCO), umeme (LUKU), bima, na

    kulipa madeni. Changamoto kuu kwa sasa ni juu ya suala la usimamizi kwani

    makampuni ya simu yanayotoa huduma hizi yanasimamiwa na chombo (TCRA)

    ambacho hakihusiki na masuala ya kifedha bali ya mawasiliano. Hata hivyo, Benki

    Kuu inakamilisha mazungumzo na TRCA kuiwezesha kushiriki katika kusimamia

    masuala ya huduma za kifedha zinazofanywa na makampuni ya simu.

  • 9

    Sekta ya Nje

    15. Katika mwaka 2010 thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje iliongezeka

    kwa asilimia 21.9 kutoka Dola za Kimarekani milioni 4,780.4 mwaka 2009 hadi Dola

    za Kimarekani milioni 5,828.2. Hii ilichangiwa na kuongezeka kwa thamani ya mauzo

    ya bidhaa zisizo asilia ambayo iliongezeka kwa asilimia 33.7 na mapato ya huduma

    (asilimia 12.8). Kwa upande mwingine, thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa

    toka nje mwaka 2010 ziliongezeka kwa asilimia 18.8 kufikia Dola za Kimarekani

    milioni 8,974.7 kutoka Dola za Kimarekani milioni 7,543.2 mwaka 2009. Hii ilitokana

    na kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa hususan zitakazowezesha kuongeza

    uzalishaji.

    Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kikanda

    16. Katika kuongeza juhudi za kuimarisha mtangamano wa Jumuiya ya Afrika

    Mashariki (EAC) nchi wanachama wa Jumuiya zimeridhia uanzishwaji wa, na

    zimeanza utekelezaji wa Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika

    Mashariki. Kuhusu Jumuiya ya Uchumi Kusini Mwa Afrika (SADC), nchi wanachama

    zinaendelea na jitihada za kuimarisha utekelezaji wa makubaliano ya “Eneo Huru la

    Biashara: (Free Trade Area) ili ifikapo mwaka 2012 nchi zote ziwe zimeingia katika

    makubaliano na ushuru kwa bidhaa nyingi ufikie sifuri. Hadi sasa nchi za Demokrasia

    ya Kongo, Angola na Seychelles hazijarithia mpango huo wa eneo huru la biashara.

    Kufuatia hatua zilizochukuliwa za kuimarisha biashara miongoni mwa nchi

    wanachama, biashara kati ya Tanzania na nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki

    na Jumuiya ya Uchumi Kusini Mwa Afrika iliendelea kukua ambapo mauzo ya bidhaa

    za Tanzania katika nchi hizi kwa pamoja yaliongezeka kwa Dola milioni 437.1

    mwaka 2010, sawa na asilimia 68.5 wakati ambapo uagizaji wa bidhaa uliongezeka

    kwa Dola milioni 69.2 sawa na asilimia 6.6.

    Uendelezaji wa Sekta Binafsi

    17. Katika mwaka 2010, Serikali iliendelea kuchukua hatua za makusudi katika

    kuimarisha na kuendeleza sekta binafsi. Mwezi Agosti 2010, Bunge lilipitisha sheria

  • 10

    ya Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Binafsi - PPP No. 19 ya mwaka 2010. Vitengo

    vya PPP tayari vimeshanzishwa katika Wizara ya Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu ili

    kuratibu masuala yanayohusiana na PPP. Kupitia vitengo hivyo, Serikali inaandaa

    mkakati na mwongozo wa utekelezaji wa sheria ya PPP, hususan katika miradi

    mikubwa ya miundombinu. Serikali inakamilisha maandalizi ya kanuni

    zitakazoongoza utekelezaji wa Sheria ya PPP.

    Tathmini ya Dira na Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati na Mrefu

    18. Tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ilibainisha

    kwamba dhana ya Dira ya Taifa ya Maendeleo bado ni sahihi na inatekelezeka iwapo

    kutaongezwa msukumo katika utekelezaji. Aidha, tathmini ilibainisha haja ya kuwa

    na mfumo linganishi wa utayarishaji na utekelezaji wa mipango ya muda wa kati na

    mrefu. Serikali iko katika mchakato wa kuandaa Mpango wa Muda Mrefu ambao

    utekelezaji wake utafanyika kuanzia mwaka 2011/12 kwa vipindi vya muda wa kati

    wa miaka mitano mitano hadi 2025. Mchakato huu ambao bado unaendelea ulianza

    kwa kupitia mifumo ya mipango iliyoko na kuangalia namna bora ya kuioanisha.

    Utekelezaji wa mpango huu unakusudia kwanza kufungua fursa za kijiografia tulizo

    nazo ili tuweze kufaidika na soko la nchi za Jumuiya ya Africa Mashariki, SADC na

    Maziwa Makuu na kuweza kuhudumia nchi majirani zisizokuwa na bahari. Aidha,

    Mpango unakusudia kuhakikisha tunafaidika na rasilimali asili tulizonazo kama vile

    ardhi yenye rutuba, madini, vivutio vya kitalii, n.k.

    MKUKUTA na Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs)

    19. Utekelezaji wa awamu ya kwanza ya MKUKUTA ulifikia kikomo Juni 2010.

    Mafanikio kadhaa yalipatikana kutokana na utekelezaji wake, kama vile ukuaji wa

    uchumi, ongezeko katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, usimamizi thabiti wa fedha

    za umma, uimarishaji wa barabara vijijini, pamoja na uboreshaji wa sekta za elimu,

    afya na maji. Hata hivyo, zipo changamoto zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na kasi

    ndogo ya kupungua kwa kiwango cha umaskini, upatikanaji na ubora wa huduma

    kwa viwango vilivyokusudiwa, ushiriki mdogo wa sekta binafsi, na ufinyu wa bajeti.

    Changamoto nyingine zilikuwa nje ya uwezo wa Serikali, zikiwemo ukame

    uliojitokeza nchini mwaka 2006 na kuyumba kwa uchumi wa dunia kulikoanza

  • 11

    mwishoni mwa mwaka 2008. Pamoja na ufinyu wa bajeti, Serikali ilikuwa ikiongeza

    mwaka hadi mwaka kiasi cha fedha kinachoenda katika utekelezaji wa MKUKUTA

    kutoka asilimia 54.1 ya bajeti yote mwaka 2005/06 wakati MKUKUTA ulipoanza hadi

    asimia 71.2 mwaka 2009/10. Katika kuongeza juhudi za kuondoa umaskini na

    kukuza uchumi, Serikali iliridhia uanzishwaji wa awamu ya pili ya MKUKUTA mwezi

    Oktoba 2010. Mchakato wa uandaaji wa awamu hii ya pili uliwashirikisha wadau

    wengi na ulizingatia zaidi mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika

    utekelzaji wa awamu ya kwanza ya MKUKUTA.

    20. Mapitio ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia, yanaonesha kuwa Tanzania

    inafanya vizuri katika baadhi ya viashiria kama vile vya elimu ya msingi na usawa wa

    jinsia. Hata hivyo, changamoto bado zipo katika viashiria vingine vya umaskini

    kama vile afya ya uzazi wa mama na kupunguza vifo vya watoto. Hivyo, kipaumbele

    sasa kimewekwa katika kuongeza ufanisi katika maeneo hayo ya changamoto na

    kuimarisha zaidi utekelezaji pale ambapo Tanzania imepata mafanikio kiasi. Hata

    hivyo, kuna haja ya kuchambua viashiria hivi kwa umakini zaidi kwani kuna baadhi

    ambavyo vimepitwa na wakati. Mfano, MDG inasisitiza zaidi juu ya uandikishaji

    katika elimu ya msingi na kusahau masuala ya msingi ya ubora wa elimu. Vile vile

    viashiria vingine havina namna ya kuvipima mfano vinavyohusiana na masuala ya

    mazingira.

    Utafiti wa Afya na Demografía 2010-TDHS

    21. Kulingana na ripoti ya Utafiti wa Afya na Demografía (Tanzania Demographic

    and Health Survey – (TDHS) ya mwaka 2010, kiwango cha udumavu wa watoto

    walio chini ya miaka mitano kilipungua kutoka asilimia 37.7 mwaka 2004/05 hadi

    asilimia 35.4 mwaka 2010; upungufu wa uzito kwa watoto walio chini ya miaka

    mitano ulipungua kutoka asilimia 22 mwaka 2004/05 hadi asilimia 21 mwaka 2010;

    na hali ya ukondefu iliongezeka kutoka asilimia 3 mwaka 2004/05 hadi asilimia 4

    mwaka 2010. Aidha, watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wenye uzito

    uliozidi au kiribatumbo walikuwa asilimia 5 . Hali kadhalika kwa mujibu wa ripoti

    hiyo, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka watoto

  • 12

    112 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai mwaka 2007 hadi watoto 81 mwaka

    2010 na vile vya watoto wachanga vimepungua kutoka watoto 68 hadi watoto 51

    kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai mwaka 2010. Vile vile, kiwango cha jumla

    cha uzazi (total fertility rate) kimepungua kutoka wastani wa watoto 6.3 mwaka

    1991/92 kwa mwanamke mmoja hadi wastani wa watoto 5.4 kwa mwanamke

    mmoja. Kiwango hiki kwa sasa ni kikubwa kwa maeneo ya vijijini (6.1)

    ikilinganyishwa na maeneo ya mijini (3.7). Pamoja na viashiria hivi vya afya

    kuonesha mwenendo mzuri, bado kuna haja ya kuongeza mikakati ya kuboresha

    zaidi huduma za afya hasa katika maeneo ya vijijini.

    MASUALA MUHIMU YA KISERA YALIYOJITOKEZA MWAKA 2010/11

    22. Mwaka 2010, uchumi wa dunia ulianza kuimarika na kurudi katika hali yake ya

    kawaida baada ya kuyumba katika mwaka 2008/09 kufuatia kuzorota kwa masoko

    ya fedha na mitaji katika masoko ya Ulaya na Marekani. Uchumi wa Tanzania nao

    ulianza kuimarika siyo tu kwa sababu ya kuimarika kwa uchumi wa dunia bali pia

    kutokana na mpango wa Serikali wa kuunusuru uchumi, pamoja na hatua

    zilizochukuliwa na serikali katika kuongeza ruzuku ya pembejeo za kilimo na

    utekelezaji wa ASDP kulikoenda sambamba na kuwepo kwa hali nzuri ya hewa . Hata

    hivyo, katika nusu ya pili ya mwaka 2010/11, matatizo ya ukame yalianza kuikumba

    nchi yetu ambapo sekta mbalimbali ziliathirika moja kwa moja kama vile kilimo na

    nishati ambazo hutegemea zaidi mvua. Kufuatia hali hiyo ya ukame, Serikali

    ililazimika kuanza mgao wa umeme mwishoni mwa mwaka 2010 kutokana na

    kupungua kwa kina cha maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme. Mgao huu

    uliathiri sekta nyingine zinazotegemea umeme kama vile viwanda na hivyo kuna

    hatari ya kutofikia malengo tuliyojiwekea na itapelekea pia kudumaza jitihada za

    kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2025 na MDG. Hali kadhalika, kuongezeka

    kwa bei za mafuta katika soko la dunia ambako kunachochewa pia na machafuko ya

    kisiasa katika nchi za kiarabu kunaweza kuathiri pia ukuaji wa uchumi wetu.

    Kutokana na hali hii, ni dhahiri kuwa pana haja ya kuongeza kasi ya ukuaji uchumi.

  • 13

    23. Masuala mengine ya kisera yaliyojitokeza mwaka 2010 ni pamoja na

    utekelezaji wa MKUKUTA II ambao ulipitishwa rasmi mwezi Oktoba 2010, maandalizi

    ya mpango wa “SAGCOT”, maendeleo ya rasilimali watu na maandalizi ya Mpango

    wa Maendeleo wa Miaka Mitano.Utekelezaji wa Mradi wa Ukanda wa Kilimo wa

    Kusini mwa Tanzania (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania_ SAGCOT)

    ambao ni sehemu ya Kilimo Kwanza utasaidia kupunguza umaskini miongoni mwa

    wananchi wanaoishi vijijini kwa kuwaongezea mavuno ya mazao yao na kukuza ajira

    miongoni mwa watanzania. SAGCOT ni mpango mkakati wa kuleta mapinduzi ya

    kilimo unaotekelezwa kwa pamoja kati ya serikali na kwa kushirikiana na wadau

    mbalimbali wa kilimo yakiwemo mashirika ya kimataifa.

    Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16)

    24. Mchakato wa kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 –

    2015/16) unaendelea kufanyika na kwa sasa uko katika ngazi za maamuzi, chini ya

    uongozi na usimamizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango. Mpango huu ni awamu ya

    kwanza ya mpango elekezi (roadmap) wa miaka 15 wa kutekeleza Dira ya Taifa ya

    Maendeleo 2025 kwa utaratibu maalum (systematically) ukiwa na viashiria vya

    kupima mafanikio ya utekelezaji. Mpango wa Miaka Mitano unajengwa juu ya na

    unazingatia malengo ya MKUKUTA II na pia unajumuisha malengo mapana zaidi.

    Dhana ya Mpango huu ni kufungulia fursa za ukuaji wa uchumi wa Taifa na

    unalenga kabadili mtazamo wa kupanga maendeleo ya Taifa kutoka kupanga

    kulingana na rasilimali zilizopo pekee kwenda kwenye kupanga ili kutumia kikamilifu

    fursa zinazojitokeza. Mpango pia umebainisha nguzo kuu nne ambazo zitakuwa

    vipaumbele vya kitaifa na utekelezaji wake utasaidia kufikia malengo ya Dira. Nguzo

    hizo ni kama zifuatazo:

    I. Kuendeleza Utengamavu wa Uchumi Jumla: Katika nguzo hii, Serikali

    itaimarisha viashiria vya uchumi jumla kwa kuimarisha sera ya mapato na

    matumizi ya Serikali, kudhibiti mfumuko wa bei, kuweka viwango sahihi vya

    ujazi wa fedha vinavyowiana na kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa na upandaji

    wa bei, kuimarisha usimamizi wa mabenki na mfumo wa malipo nchini. Vile

    vile utawala bora utaimarishwa katika sekta zote ili kuongeza kasi ya ukuaji

  • 14

    wa uchumi katika ngazi zote. Sambamba na hili, Serikali itaendeleza

    mafanikio yaliyopatikana katika huduma za jamii na msukumo utakuwa katika

    kuongeza ubora wa elimu, huduma za afya, maji na ustawi wa jamii katika

    ngazi zote;

    II. Kutumia fursa za rasilimali zilizopo katika kukuza uchumi: Eneo la

    msisitizo hapa ni kufanya mapinduzi ya kijani ili Tanzania ijitosheleze kwa

    chakula na kuuza ziada nje.;

    III. Kutumia Fursa za Kijiografia: Mwelekeo wa Mpango ni kutumia kimkakati

    fursa ya kupakana na bahari ya Hindi na Maziwa pamoja na nchi zisizokuwa

    na bahari inayoifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara na usafirishaji

    katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu. Hivyo, msukumo utaelekezwa katika

    kuboresha (kukarabati na kujenga) miundombinu ya bandari, reli, nishati,

    barabara na mkongo wa Taifa pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa

    huduma hizo na zile za Mamlaka ya Mapato; na

    IV. Kuboresha na kukuza matumizi ya TEKNOHAMA: Katika kipindi hiki cha

    Mpango, msukumo utawekwa katika kuboresha teknolojia ili kusaidia katika

    kuongeza thamani na tija hususan katika viwanda, madini, usindikaji wa

    mazao ya kilimo na matumizi ya TEKNOHAMA katika kuboresha huduma kama

    vile ‘e_Government”. Maeneo mengine yatakayopewa msisitizo ni katika

    kuongeza kiwango na ubora wa elimu hasa ya sayansi, na ufundi stadi.

    Vipaumbele Vya Kisekta

    25. Serikali imebainisha maeneo ya kipaumbele ya Kitaifa yatakayotekelezwa

    katika kipindi cha muda wa kati. Lengo ni kuwekeza katika shughuli za kiuchumi na

    kijamii zenye kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi kwa upana zaidi na kupunguza

    umaskini. Aidha, pamoja na maeneo yaliyobainishwa kama vipaumbele, maeneo ya

    kimkakati yatakayozingatiwa kwa mwaka wa mpito wa 2011/12 ni umeme, bandari,

    reli, maji na chakula cha hifadhi. Kila sekta itahakikisha kuwa inaweka msukumo

  • 15

    katika matumizi endelevu ya maliasili zilizopo kama vile ardhi, maji, madini, gesi

    asilia, wanyama pori, mazao ya misitu na vivutio vya utalii ili kuchangia katika ukuaji

    wa uchumi. Maeneo yaliyobainishwa na sekta husika kama vipaumbele vya muda wa

    kati ni kama ifuatavyo:

    I. Elimu

    a. Kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote ikiwemo ufundishaji na ujifunzaji

    kwa njia ya TEKNOHAMA;

    b. Kuboresha sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na mikakati ya

    utekelezaji, ikiwemo kutoa elimu inayoimarisha ujuzi wa wahitimu; na

    c. Kuimarisha ugharamiaji wa elimu ya juu.

    II. Kilimo, Mifugo na Uvuvi

    a. Kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na ujenzi wa

    mabwawa kwa ajili ya upatikanaji wa maji ya mifugo na umwagiliaji;

    b. Kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo, mifugo na uvuvi;

    c. Kuboresha huduma za ugani;

    d. Kuiwezesha sekta binafsi kuwekeza katika kilimo, mifugo na uvuvi; na

    e. Kuboresha upatikanaji wa masoko na usindikaji wa mazao ya kilimo,

    mifugo na uvuvi.

    III. Nishati

    a. Kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali;

    b. Kupanua na kuimarisha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na

    usambazaji wa nishati ya umeme, sawia na kuongeza uhakika wa

    upatikanaji na unafuu wa bei yake;

    c. Kuendeleza utafiti wa upatikanaji na utumiaji wa umeme wa gesi asilia na

    mafuta; na

    d. Kupanua miundombinu ya gesi asilia.

  • 16

    IV. Uendelezaji wa Miundombinu na Usafirishaji

    a. Ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja na vivuko na kupunguza

    msongamano wa magari mijini;

    b. Kuanzisha mfuko wa ujenzi wa barabara (Road Development Fund) na

    kupanua wigo wa mfuko wa matengenezo ya barabara;

    c. Ujenzi na ukarabati wa majengo/nyumba za Serikali;

    d. Ukarabati na ujenzi wa reli pamoja na viwanja vya ndege;

    e. Uimarishaji wa huduma za hali ya hewa;

    f. Ujenzi na ukarabati wa bandari pamoja na utengenezaji wa meli katika

    maziwa: na

    g. Kujenga uwezo wa kufanyia ukarabati mitambo, magari na vifaa vingine

    vya Serikali.

    V. Maendeleo ya Viwanda

    a. Kuendelea kuboresha mazingira ya viwanda, biashara na kuvutia

    uwekezaji nchini;

    b. Kukuza teknolojia sahihi kwa wajasiriamali wadogo na wa kati katika

    kuongeza thamani ya bidhaa hususan usindikaji wa bidhaa za kilimo;

    c. kuendeleza Kanda maalumu za uzalishaji kwa ajili ya kuuza nje kwa

    kushirikisha sekta ya umma na sekta binafsi; na

    d. Kuendeleza viwanda vya msingi na kuvipa kipaumbele viwanda

    vinavyotumia malighafi inayopatikana nchini.

    VI. Afya

    a. Kuimarisha huduma za tiba, kinga na utengamavu wa afya katika ngazi

    zote;

    b. Kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya; na

    c. Kuajiri madaktari wote wanaohitimu katika vyuo mbalimbali.

    VII. Maji

    a. Kuendeleza program ya maji na usafi wa mazingira vijijini;

  • 17

    b. Kutekeleza program maalumu ya maji safi na maji taka katika jiji la Dar es

    Salaam;

    c. Kutekeleza miradi inayoendelea kwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na

    salama; na

    d. Kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.

    VIII. Ardhi

    a. Kuboresha upatikanaji wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo ya

    mijini na vijijini na kuboresha uelewa wa wananchi kuhusu huduma za

    mikopo ya nyumba;

    b. Kuanzisha kituo cha kitaifa cha kupokea picha za anga ili kurahisisha

    upimaji wa ardhi na utayarishaji wa ramani;

    c. Kuimarisha na kupanua mfumo wa kisasa wa utunzaji wa kumbukumbu za

    ardhi ili kuboresha usimamizi wa ardhi na kurahisisha mfumo wa Taifa wa

    anuani za makazi;

    d. Kutekeleza Mpango wa taifa wa matumizi ya ardhi; na

    e. Utayarishaji wa mipango miji kukabiliana na changamoto za ukuaji wa

    miji.

    IX. Maendeleo ya Raslimali watu

    a. Kuimarisha ujuzi na utaalamu unaokidhi mahitaji ya soko kwa kuzingatia

    sekta ya umma, sekta binafsi na masoko ya kikanda;

    b. Kujenga uwezo wa sekta mbalimbali kuandaa mipango thabiti ya raslimali

    watu na kuchambua mahitaji ya ujuzi katika sekta husika;

    c. Kuimarisha uwajibikaji na uadilifu katika utendaji kazi;

    d. Kukamilisha mradi wa vitambulisho vya Taifa; na

    e. Kuwashirikisha watanzania wafanyao kazi nje ya nchi (diáspora) ili waweze

    kushiriki na kuchangia katika uchumi.

    X. Sayansi na Teknolojia

    a. Kuendeleza miundombinu na huduma za TEKNOHAMA nchini ikiwa ni

    pamoja na kukamilisha ujenzi wa mkongo wa Taifa;

  • 18

    b. Kuboresha na kujenga taasisi za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu

    zinazojumuisha mafunzo ya ufundi stadi, (ikiwemo Taasisi ya sayansi na

    Teknologia ya Nelson Mandela) vituo mahiri vya utafiti wa kisayansi na

    viatamizi; na

    c. Kuimarisha utafiti na maendeleo (R&D) na kutumia matokeo yake

    kibiashara.

    XI. Mtangamano wa Kikanda

    a. Kuendeleza uwezo na ujuzi unaohitajika ili kuiwezesha Tanzania kutumia

    kikamilifu fursa zilizopo na zinazojitokeza katika mtangamano wa kikanda;

    b. Uendelezaji wa miundombinu ya kikanda inayojumuisha sekta za

    barabara, reli bandari, TEKNOHAMA na nishati;

    c. Kukamilisha Mkakati wa Utekelezaji wa Soko Huru la Pamoja; na

    d. Kukamilisha mkakati wa utekelezaji wa habari, mawasiliano na ufahamu

    unaolenga kuwafikia wadau wengi zaidi.

    XII. Mamlaka ya Serikali za Mitaa

    a. Kuendelea kutekeleza sera ya kupeleka madaraka mikoani (D by D);

    b. Kujenga na kukarabati miradi ya miundombinu na kutoa vivutio

    vitakavyowashawishi wataalamu kubaki na kuendelea kutoa huduma

    katika Serikali za mitaa hasa maeneo ya pembezoni;

    c. Kupanua wigo na kuimarisha usimamizi wa kodi;

    d. Kuboresha mfumo wa usimamizi wa fedha za umma na uwajibikaji katika

    ngazi zote;

    e. Kujenga ofisi za makao makuu ya mikoa, halmashauri na wilaya mpya; na

    f. Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa kwa wakati;

    XIII. Sekta ya Fedha

    a. Kuongeza mtaji wa Banki ya Rasilimali Tanzania na Benki ya Wanawake;

    b. Kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo;

  • 19

    c. Kuongeza na kuimarisha huduma za kifedha pamoja na uelewa wa

    masuala ya kifedha (financial education) kwa wakopaji na wakopeshaji

    hasa katika maeneo ya vijijini;

    d. Kuanzisha chombo cha kutoa taarifa za masuala ya mikopo (Credit

    Reference Bureau/Databank); na

    e. Kukuza ufanisi na kuongeza ushindani katika mifuko ya hifadhi ya jamii;

    MISINGI NA MALENGO YA UCHUMI JUMLA NA MAENDELEO YA JAMII

    2011/12-2015/16

    26. Malengo ya sera za uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2011/12 –

    2015/16 yatakuwa yafuatayo:

    (i) Pato halisi la Taifa litakua kwa asilimia 6.8 mwaka 2011, asilimia 7.5

    mwaka 2012, na kuendelea kuongezeka hadi asilimia 8.5 mwaka 2015;

    (ii) Kuendelea kudhibiti kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya

    tarakimu moja;

    (iii) Kuongezeka kwa mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la

    Taifa kwa asilimia 17.2 ya Pato la Taifa mwaka 2011/12 na kuendelea

    kuongezeka kwa wastani wa asilimia 17.5 karika kipindi cha muda wa

    kati;

    (iv) Kudhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi unatarajiwa

    kukua kwa asilimia 19.0 mwaka 2011/12; asilimia 18.6 mwaka 2012/13

    na asilimia 18.1 mwaka 2013/14. Ukuaji huu unalenga kuwiana na

    malengo ya ukuaji wa uchumi, na kasi ya upandaji bei;

    (v) Kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayoweza kukidhi mahitaji ya

    uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje kwa kipindi kisichopungua

    miezi 4.6;

    (vi) Kupunguza tofauti ya viwango vya riba; na

    (vii) Kuwa na kiwango imara cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na

    mwenendo wa soko la fedha.

  • 20

    27. Malengo tuliyokusudia ya Sera za uchumi jumla katika kipindi cha muda wa

    kati (2011/12-2015/16) yatafanikiwa kwa kuzingatia misingi ifuatayo:-

    (i) Kuendelea kuimarika kwa amani, utulivu na utengamano;

    (ii) Vyanzo vya maji vitaendelea kuhifadhiwa na kukidhi mahitaji;

    (iii) Kuendelea kuimarika kwa utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla

    na maendeleo ya jamii;

    (iv) Kuongezeka na kuboresha mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na kubuni

    vyanzo vipya vya kodi, kuimarisha ukusanyaji wa kodi ya majengo, na

    kupunguza misamaha ya kodi ili kuweza kugharamia vipaumbele

    vilivyoainishwa;

    (v) Kuimarisha usimamizi katika matumizi ya fedha za umma;

    (vi) Rasilimali zitaelekezwa kwenye maeneo yanayochochea ukuaji wa

    uchumi kwa haraka zaidi kama yalivyoainishwa hapo juu na katika

    Mwongozo wa Mpango na Bajeti wa mwaka 2011/12 – 2015/16;

    (vii) Kutekelezwa kwa MKUKUTA II kama ilivyopangwa;

    (viii) SAGCOT na Nguzo 10 za Kilimo Kwanza zitatekelezwa kama

    ilivyopangwa;

    (ix) Kuendeleza ushirikishwaji wa sekta binafsi na kuboresha mazingira ya

    biashara; na

    (x) Kuimarika kwa sera ya fedha (monetary policy) ili iendane na sera za

    bajeti (fiscal policies) zitakazosaidia kupunguza mfumuko wa bei na

    tofauti ya riba za kukopa na amana, na kuongeza mikopo kwa sekta

    binafsi;

    HITIMISHO

    Dhamira kuu ya Serikali ni kuhakikisha kuwa yote yaliyosemwa hapo juu

    yatatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu na asasi zisizo za kiserikali ikijumuisha

    sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kufikia malengo ya millenia, Dira na ya

    MKUKUTA II. Kama kila mmoja atatekeleza wajibu wake, inawezekana kabisa kufikia

    malengo yetu ya muda mfupi, kati na mrefu tuliyojiwekea kama yalivyoainishwa

    katika Mpango wa Maendeleo wa Muda wa Kati.