biashara ndani ya ajira. - jamiiforums · ambacho wanakuwa hawajakijua ni kwamba hii ni hatari...
TRANSCRIPT
1
2
BIASHARA NDANI YA AJIRA. Anzisha Na Kuza Biashara Yako Ukiwa Bado Umeajiriwa.
MAKIRITA AMANI
+255 717 396 253
www.amkamtanzania.com
MAY 2016
3
Kitabu hiki kimeandikwa na;
Makirita Amani,
Simu; +255 717396253/ +255 755953887
Barua pepe; [email protected] au [email protected]
Blogu; www.kisimachamaarifa.co.tz
www.amkamtanzania.com
Toleo la kwanza May 2016.
Hatimiliki
Haki zote za kitaaluma zimehifadhiwa haipendezi na ni kinyume na sheria
kunakili au kuchukua chochote kilichoandikwa katika kitabu hiki bila idhini
kutoka kwa Mwandishi wa kitabu hiki; Lakini kinaruhusiwa kutumiwa popote
palipo na mafundisho yanayohusiana na yaliyoandikwa humu kwa ruhusa ya
mwandishi.
Kwa matumizi ya kitabu hiki katika mafundisho tafadhali wasiliana na
mwandishi kwa mawasiliano yaliyopo hapo juu.
OMBI MAALUMU;
HONGERA KWA KUPATA KITABU HIKI KIZURI CHA BIASHARA NDANI YA
AJIRA. KISOME NA TUMIA MAFUNDISHO HAYA KWENYE SAFARI YAKO YA
MAFANIKIO.
KAMA UMEPOKEA KITABU HIKI KAMA NAKALA TETE (SOFTCOPY) TAFADHALI
USIMTUMIE MTU YEYOTE KITABU HIKI HATA KAMA NI WA KARIBU SANA
KWAKO. KAMA KUNA YEYOTE ATAKAYEKIHITAJI TAFADHALI MWELEKEZE
JINSI ULIVYOKIPATA WEWE, ITAMSAIDIA SANA KUPATA MAFUNZO HAYA
TOFAUTI NA WEWE UKIMTUMIA TU.
KILA LA KHERI NA TUPO PAMOJA KATIKA SAFARI HII YA KUHAKIKISHA
MAISHA YETU YANAKUWA BORA ZAIDI.
ASANTE SANA.
4
YALIYOMO UTANGULIZI. ...................................................................................................... 6
AJIRA NI SEHEMU NZURI YA KUANZIA BIASHARA............................................... 7
HATARI YA KUCHOMA MELI MOTO. ................................................................. 11
UNA MUDA WA KUTOSHA. .............................................................................. 17
CHANZO KIMOJA CHA KIPATO NI UTUMWA. ................................................... 22
BIASHARA INAHITAJI MUDA KUKUA. ............................................................... 26
TENGENEZA MPANGO BORA KWAKO. ............................................................. 29
KUBALI KUPOTEZA. .......................................................................................... 33
BIASHARA UNAZOWEZA KUFANYA UKIWA BADO UMEAJIRIWA. ..................... 36
KIPAJI ULICHONACHO .................................................................................. 36
UTAALAMU NA UZOEFU WAKO ................................................................... 39
BIASHARA ZA KAWAIDA ............................................................................... 41
BIASHARA YA MTANDAO ............................................................................. 42
KILIMO CHA KIBIASHARA ............................................................................. 43
UWEKEZAJI UNAOWEZA KUFANYA UKIWA BADO UMEAJIRIWA ...................... 45
UWEKEZAJI KWENYE MFUKO WA UMOJA .................................................... 45
UWEKEZAJI KWEYE SOKO LA HISA ................................................................ 47
UWEKEZAJI KWENYE MALI ........................................................................... 47
MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOANZA BIASHARA UKIWA KWENYE AJIRA. ..... 50
HATARI ZA KUEPUKA ILI BIASHARA YAKO IFANIKIWE. ...................................... 56
KUWA NA MSHIRIKA. ....................................................................................... 60
USIFANYE KILA KITU PEKE YAKO. ...................................................................... 63
FAIDA NYINGINE ZA KUENDELEA KUBAKI KWENYE AJIRA. ............................... 65
NIDHAMU .................................................................................................... 65
MTANDAO ................................................................................................... 66
RASILIMALI ................................................................................................... 67
MIFEREJI NANE YA KIPATO UNAYOHITAJI KUWA NAYO. .................................. 69
TENGENEZA MFUMO. ...................................................................................... 74
LINDA KAZI YAKO. ............................................................................................ 77
5
WAKATI SAHIHI WA KUONDOKA KWENYE AJIRA. ............................................ 81
KITU MUHIMU KUFANYA MUDA WOTE. .......................................................... 87
ANZA SASA, NUNUA UHURU WAKO. ................................................................ 90
6
UTANGULIZI. BIASHARA NDANI YA AJIRA ni kitabu ambacho kinakupa mbinu za kuanzisha na
kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa. Ni kitabu ambacho kila
mwajiriwa anapaswa kukisoma kwa sababu kina maarifa muhimu ya
kumwezesha mwajiriwa kujikomboa kiuchumi.
Wote ni mashahidi kwamba hali ya ajira kwa sasa imebadilika sana. Na kipato
cha ajira kimekuwa hakitoshelezi. Na hata zile njia ambazo watu walikuwa
wanatumia kujipatia kipato cha ziada kama posho, marupurupu na hata
rushwa kwa sasa vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Hivyo njia pekee kwa waajiriwa kuweza kujitengenezea uhuru wa kipato ni
kuwa na vyanzo mbadala vya mapato. Kupitia kitabu hiki itajifunza mbinu za
kuanzisha biashara na kuikuza. Pia itajifunza aina za biashara unazoweza
kufanya ukiwa bado kwenye ajira. Utajifunza uwekezaji unaoweza kuanza
kufanya ukiwa hapo kwenye ajira yako.
Kikubwa na muhimu zaidi utajifunza mifereji nane ya kipato unayotakiwa
kujijengea ili kuweza kufikia uhuru wa kifedha. Utajifunza changamoto na
hatari za kuepuka na pia kuweza kuilinda kazi yako pale unapofanya biashara.
Kitabu hiki ni mwongozo muhimu kwako kufikia uhuru wa kifedha kwa kuwa na
biashara ya pembeni wakati umeajiriwa.
Soma kitabu hiki na yatumie yale ambayo umejifunza kwenye kitabu hiki katika
kuboresha kazi yako na biashara yako pia. Na mwishowe utafikia uhuru wa
maisha yako na mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri kwenye usomaji wa kitabu hiki, nina imani utajifunza
mengi na utayatumia kwenye kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa
ujumla.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.amkamtanzania.com
www.kisimachamaarifa.co.tz
7
AJIRA NI SEHEMU NZURI YA KUANZIA BIASHARA. Tunaishi kwenye zama ambazo mabadiliko yanaendelea kutokea kwa kasi
kubwa sana. Hizi ni zama ambazo tunatoka kwenye ajira kuwa chanzo cha
uhakika cha kipato na tunaelekea kwenye biashara na ujasiriamali kama
chanzo cha uhakika cha kipato.
Miaka ya nyuma, hasa baada ya mapinduzi ya viwanda, kupata kazi ilikuwa
ndiyo ndoto kubwa ya kila mtu. Watu walisisitizwa kwenda shuleni, kusoma
kwa bidii sana ili wafaulu na kuweza kupata kazi nzuri. Kazi zilikuwa za uhakika
na wale waliokuwa wamesoma na kufaulu vizuri walikuwa na uhakika wa kazi.
Lakini kama ilivyo asili ya dunia kila kitu kinabadilika, na kila zama zina mambo
yake. Sasa hivi zama zile za kusoma ili upate kazi na uwe na uhakika wa maisha
mazuri hazipo tena. Ujio wa mapinduzi ya kiteknolojia umerahisisha sana
ufanyaji wa kazi. Mahali ambapo wangefanya kazi watu watano, anaweza
kufanya kazi mtu mmoja na kompyuta. Na pia zama hizi watu wengi sana
wameweza kupata elimu ya juu, wamesoma na kufaulu vizuri.
Kwa hali hii, ya nafasi za kazi kuwa chache, na wanaozitafuta nafasi hizo kuwa
wengi, thamani ya kazi imeshuka. Ule uhakika wa kwamba ukipata kazi nzuri
ndiyo uhakika wa kuwa na maisha mazuri haupo tena. Mtu anaweza kuwa
kwenye kazi leo na mwezi ujao kazi hiyo akawa hana tena.
Zamani ilikuwa kawaida kwa mtu kufanya kazi kwenye kampuni au taasisi moja
kuanzia ujana mpaka anazeeka, ila kwa sasa mpaka mtu anazeeka anakuwa
amefanya kazi sehemu tofauti zisizopungua tano. Hali hii inafanya kutegemea
ajira kama sehemu kuu ya kipato kushindikana na hivyo kila mtu anahitaji njia
mbadala ya kujiongezea kipato.
Na kwa hali ilivyo sasa, njia pekee ya uhakika ya kujitengenezea kipato ni
kupitia biashara na ujasiriamali. Kwa sababu kumekuwa na fursa nyingi za
kibiashara, sasa hivi karibu kila mtu anaweza kuingia kwenye biashara.
Mahitaji ya kuanza biashara kwa sasa ni rahisi kuliko kipindi cha nyuma. Fursa
za kibiashara ni nyingi na uzuri zaidi kuna biashara ambazo mtu anaweza
kuanza na mtaji kidogo sana na akaweza kuikuza. Pia mapinduzi ya kiteknolojia
pamoja na uwepo wa mtandao wa intaneti umerahisisha sana ufanyaji wa
biashara.
8
Changamoto kwa waajiriwa.
Pamoja na uhakika huu wa kuweza kutengeneza kipato kupitia biashara na
pamoja na fursa nyingi zilizopo kwa wanaotaka kuanza biashara, waajiriwa
bado wamekuwa na changamoto moja kubwa. Na changamoto hii inaanzia
kwenye swali hili;
Je niache kazi na kuingia kwenye biashara au nikae kwenye kazi na biashara
nifanye baadaye nikishapata mtaji?
Hili ni swali zito ambalo limewafanya wengi kuwa njia panda na kushindwa
kufanya maamuzi sahihi. Na pia wapo ambao wamefanya maamuzi ambayo
siyo sahihi na kujikuta kwenye wakati mgumu kuliko walivyokuwa wanafikiri
awali.
Maamuzi mabovu.
Kwa wale wanaochagua kuacha kazi na kuingia kwenye biashara moja kwa
moja, wengi wamekuwa wakikutana na changamoto kubwa sana. Hasa pale
ambapo mtu anakuwa na wategemezi wengi, anajikuta akishindwa kukuza
biashara na wakati huo akiwa hana kipato. Tutaona kwenye sura za mbele
hatari ya kuchoma meli moto na pia biashara inahitaji kukua.
Ni wachache wanaochagua njia hii na wakafanikiwa kwenye biashara, tena
hawa ni wale ambao wanafanya maamuzi haya wakiwa bado ni vijana na
hawana wategemezi wengi. Kwa wale ambao wameshakaa kwenye ajira kwa
muda mrefu na wana watu wengi wanaowategemea, maamuzi ya kuacha kazi
na kuingia kwenye biashara ni hatari sana na yanakutana na vikwazo vingi
mno, kuanzia kwa mtu mwenyewe mpaka kwa wale wanaowazunguka.
Kwa upande wa pili kuna wale ambao wanasema hawawezi kuacha kazi na
kuingia kwenye biashara. Wanasema ni bora waendelee kubaki kwenye kazi
huku wakikusanya mtaji na wakishapata mtaji wa kutosha basi wataondoka
kwenye kazi na kuingia kwenye biashara.
Hawa nao wanakuwa wamefanya maamuzi mabovu sana kwa sababu hii moja;
hakuna siku inafika wakaweza kusema sasa nimekusanya mtaji wa kutosha na
nipo tayari kuacha kazi na niingie kwenye biashara. Kila wanapokusanya mtaji
ukafika kiasi fulani inatokea jambo linahitaji fedha na wanajikuta
wameshatumia, wanaanza tena. Na kadiri muda unavyokwenda wakiwa bado
wapo kwenye ajira ndivyo zoezi la kukusanya mtaji linakuwa gumu kwa sababu
majukumu yanaongezeka na kipato hakiwatoshi.
9
Mwishowe wanaona kwa kuwa imeshindikana kupata mtaji wakiwa kazini, basi
ni heri wasubiri mpaka watakapostaafu ndipo watumie fedha yao ya kustaafu
kuanzisha biashara. Kwa sababu hapo watakuwa na fedha za kutosha. Kitu
ambacho wanakuwa hawajakijua ni kwamba hii ni hatari kubwa zaidi. Kwa
sababu ukichukua muda na kuwafuatilia wengi wa wanaostaafu, huishia
kufanya maamuzi mabovu sana ya kibiashara. Hujikuta wanawekeza kwenye
maeneo ambayo hawayajui vizuri na mwishowe kupata hasara.
Na kinachoumiza zaidi katika wakati huo ni kwamba nguvu zinakuwa
zimepungua na hivyo ile mikiki mikiki ya biashara wanakuwa hawaiwezi. Na hii
inazidi kuwaweka kwenye hali mbaya kiuchumi na kujikuta hawana popote pa
kusimamia.
Maamuzi sahihi kuchukua.
Katika swali ambalo tumeona waajiriwa wengi hujiuliza, iwapo waache kazi na
kuingia kwenye biashara au waendelee na kazi kukusanya mtaji, yote ni
maamuzi mabovu, yaani kuacha kazi ni maamuzi mabovu na kuendelea na kazi
na kuacha biashara ni maamuzi mabovu. Hapa unaweza kubaki na mawazo
mengi, je ni kipi sahihi?
Maamuzi sahihi kwa mwajiriwa kuchukua ni kufanya vyote kwa
pamoja. Yaani kubaki kwenye ajira yake huku akianzisha
biashara yake kwa pembeni.
Ndiyo, haya ni maamuzi bora sana ambayo mwajiriwa yeyote anayetaka
kujiboresha kiuchumi anatakiwa awe ameshayafanya. Na kama mpaka sasa
hujayafanya basi unapomaliza kusoma kitabu hiki fanya maamuzi haya na anza
kuyafanyia kazi
Najua utaanza kupata mawazo kwamba lakini haiwezekani, kazi yangu
inanibana, sina muda, sina mtaji na sababu nyingine nyingi. Sasa sababu zote
hizi ndio zimenifanya nikuandikie kitabu hiki, hivyo endelea kusoma na utapata
majibu ya changamoto zote zinazokuzuia usifanye kazi na biashara kwa
pamoja.
Ajira ni sehemu sahihi kwako kuanzia biashara kwa sababu nyingi sana
utakazojifunza kwenye kitabu hiki. Lakini hapa nitakushirikisha chache za
kuanza kuzifikiria wakati unaendelea kusoma kitabu hiki.
10
1. Una uhakika wa kipato.
Japo ajira siyo za uhakika sana, na japo kipato cha ajira huwa hakitoshi, lakini
kuendelea kuwa na ajira wakati unaanza biashara yako ni nafasi nzuri sana
kwako. Hii ni kwa sababu unakuwa na uhakika wa kipato, kila mwezi unapata
mshahara. Biashara mwanzoni haina uhakika wa kipato, hivyo kuwa nacho
kutoka kwenye ajira, hata kama ni kidogo kinatosha kufanya mkono uende
kinywani, huku ukipambana kukuza biashara yako.
Hakuna kitu kibaya na kinachoweza kukurudisha nyuma kama kuendesha
biashara huku huna uhakika wa mkono kwenda kinywani, na hasa kama una
familia. Kuwa na kipato cha uhakika kunaifanya akili yako itulie na uweze
kufanya maamuzi bora.
2. Unaipa biashara nafasi ya kukua.
Kwa kuwa na kipato kutokana na mshahara wako, kunakufanya usiitegemee
biashara yako wakati wa mwanzoni. Na hii ni muhimu sana kwa sababu wakati
wa mwanzo biashara inakuwa haizalishi, na mbaya zaidi inakuwa inakuhitaji
wewe uweke fedha zaidi kwenye biashara hiyo. Hivyo unapokuwa na mshahara
unaipa biashara nafasi ya kukua bila ya wewe kuiingilia.
3. Una fursa kubwa ya kupata na kuongeza mtaji.
Unapokuwa kwenye ajira, nafasi yako ya kupata msaada wa kifedha hasa kwa
njia ya mkopo ni kubwa kuliko ambaye hayupo kwenye ajira. Kwa kuwa
kwenye ajira pekee ni dhamana ya wewe kupata mkopo hata kama huna
nyumba wala gari. Wakati ambaye hana ajira atahitaji kutafuta dhamani ndiyo
aweze kupata mkopo, kitu ambacho kinaweza kuwa kigumu sana kwake.
Kama upo kwenye ajira na bado hujaanza biashara unajipunja. Unajiweka
kwenye hali ya hatari sana kiuchumi, kama ambavyo tutaona kwenye sura
zijazo, kuwa na chanzo kimoja cha kipato ni hatari kubwa sana. Na kuna faida
nyingi sana za kuanza biashara ukiwa bado umeajiriwa kama tulivyoona hizi
tatu, tutaziangalia nyingine kwa undani kwenye sura za mbele.
11
HATARI YA KUCHOMA MELI MOTO. “Choma meli moto ili usipate nafasi ya kurudi nyuma”. Huu ni usemi uliokuwa
maarufu sana siku za nyuma ambapo vuguvugu la watu kutoka kwenye ajira na
kuingia kwenye biashara lilipoanza kupamba moto.
Chanzo cha usemi wa kuchoma meli moto.
Usemi huu ulitokana na hadithi moja ya kivita. Ambapo kulikuwa na mapigano
baina ya pande mbili, na kiongozi wa upande mmoja akawachukua wapiganaji
wake kuelekea eneo la mapambano. Ili kufika walitakiwa kupanda meli maana
walitenganishwa na maji na usafiri pekee ulikuwa meli. Walipofika upande wa
pili na kutoa mizigo yao yote kwenye meli, kiongozi aliamuru meli zile
zichomwe moto.
Wapiganaji wake walishangaa sana kitendo kile, wakati meli zinaungua
akawageukia na kuwaambia, wote mnaona meli tulizokuja nazo zinatekelea
kwa moto. Hii ina maana kwamba kwenye hii vita tunatakiwa kuchagua moja
kati ya haya mawili, tushinde vita hii na kuishi, au tushindwe vita hii na
tuuwawe wote, hakuna njia ya kurudi nyuma.
Hii ni hadithi yenye hamasa kubwa sana, yenye kuweza kukusukuma uchukue
hatua, na uweze kufikia mafanikio? Si ndiyo? Ni kweli kwa upande mmoja,
lakini kwenye uhalisia wa maisha, kuna mambo mengi sana unahitaji
kuyafikiria kwa kina kabla hujachoma meli moto.
Kwenye hili la ajira au biashara, kuchoma meli moto itakuwa kuacha kazi mara
moja na kuingia kwenye ajira. Kwa kuwa umeshaacha kazi na huna tena kipato
kingine, basi utapambana kufa na kupona ili uweze kufanikiwa kwenye
biashara unayokwenda kuanzisha, hii ni kweli kwa upande mmoja, lakini kwa
hali ilivyo sasa, ni hatari kubwa sana kuchukua, hasa kama umeshakaa kwenye
ajira yako kwa muda mrefu.
Ni hatari sana kuchoma meli moto kwenye zama hizi kwa
sababu hali ya uchumi imekuwa haitabiriki, biashara zimekuwa
na changamoto kubwa na pia ushindani wa kibiashara
umekuwa mkubwa sana.
Uchumi wa sasa umekuwa hautabiriki, hata mambo yaonekane mazuri kiasi
gani, hakuna mwenye kuweza kujua kwa uhakika hali hiyo itakwenda mpaka
12
lini. Tumekuwa tunaona mtikisiko wa kiuchumi unavyoleta changamoto
kwenye biashara nyingi duniani. Unaweza kuweka juhudi zako kubwa kwenye
biashara yako, ukawa na wazo zuri la biashara ila sababu za kiuchumi ambazo
wewe huwezi kuziathiri zikazuia biashara yako kukua. Hivyo kwenye hali kama
hii kuchoma meli moto ni kujiweka kwenye hatari kubwa. Wote tunajua ya
kwamba bila ya hatari huwezi kupata faida kubwa, lakini pia ni lazima tupime
vizuri hatari tunazochukua, kama una njia mbili ambazo zote zinakufikisha
sehemu moja, ila moja ina simba na nyingine ina tembo, wote ni hatari, lakini
ni bora kupita kwenye tembo kuliko kupita kwenye simba. Kwa kuwa
inawezekana kuanza biashara yoyote ukiwa bado umeajiriwa, kwa nini ujiingize
kwenye hatari kubwa kwa kuacha kazi ndipo uingie kwenye biashara?
Kuchoma meli moto pia ni hatari sana kwa sababu wazo lako la biashara siyo
biashara yako. yaani wazo unalianza nalo, ambalo linakusukuma kuingia
kwenye biashara, siyo biashara utakayokuja kuifanya huko mbeleni. Kadiri
unavyofanyia kazi wazo lako, ndivyo utakavyozidi kuona ni vitu gani
hukuzingatia au hukujua na hivyo unahitaji kufanya mabadiliko. Sasa
mabadiliko kama haya ni vizuri kuyafanya ukiwa huna msukumo wa kupata
kipato, hivyo kuwa kwenye ajira kunakupa nafasi ya kukuza wazo lako la
biashara na kulijua vizuri. Unapokuwa unategemea biashara unayoanzisha
kama ndiyo njia kuu ya kipato, utashindwa kufanya mabadiliko kwa sababu
hutakuwa na uhakika kama mabadiliko hayo yataleta faida unayotegemea.
Haya ni maamuzi unayoweza kuyafanya kwa uhakika unapokuwa na chanzo
kingine cha kipato tofauti na biashara uliyoanzisha.
Changamoto pia zinaweza kukuondoa kabisa kwenye biashara kama
umechoma meli moto. Iko hivi, hata ujiandae vyema kiasi gani, hata ufanye
utafiti mkubwa kiasi gani, hata uandaliwe mchanganuo wa biashara na
mtaalamu wa biashara aliyebobea, bado utakutana na changamoto kwenye
biashara, pale unapoingia kufanya. Kwenye makaratasi biashara ni rahisi sana
kuipanga, ila unapoingia kuifanya biashara yenyewe, ndipo unapoona vitu
ambavyo hukutegemea kabisa. Na hata kama ulivipangilia bado kutakuwa na
mambo ambayo hukuzingatia. Sehemu ambayo unaweza kujifunza biashara
kwa uhakika ni kwa kufanya, je ungependa kujifunza biashara kwa akiba yako
pekee huku huna uhakika wa kupata faida, au ungependa kujifunza biashara
huku bado una kipato? Kwa hakika kujifunza biashara huku una kipato ni
chaguo sahihi, ndiyo maana nakushauri usichome meli moto kabla hujaisoma
biashara vizuri.
13
Kumekuwa na ushindani mkubwa sana wa kibiashara kwa sasa. Biashara
yoyote unayofanya kila mtu anaweza kuifanya. Na mara nyingi utaanza na
biashara ambayo tayari inafanyika. Au hata ukianza na biashara ya kipekee
kwako, kama itaonekana ni nzuri, kwa haraka sana wengi watakuiga. Hivyo kwa
vyovyote vile utajikuta kwenye ushindani mkali. Na njia pekee ya kushinda
kwenye ushindani huu ni kuboresha biashara yako na kutengeneza wateja
ambao wanaiamini biashara yako. zoezi hili linachukua muda, siyo kitu cha
muda mfupi. Kuna wakati utajikuta unaendesha biashara bila ya faida, ili tu
kujenga misingi ya biashara yako. Unaweza kufanya hili vizuri ukiwa bado una
ajira. Unapokuwa umetoka kwenye ajira na unaitegemea biashara kama
sehemu ya kipato, utalazimika kuingia kwenye ushindani wa moja kwa moja,
kitu ambacho kitazidi kuharibu biashara yako. Kuchoma meli moto ukiwa bado
hujajijengea uwezo wa kuzishinda biashara nyingine ni hatari kubwa sana
kwako.
Kazi unayofanya sasa inaweza kuwa sehemu sahihi kwako kukutana na wateja
wa biashara yako mpya. Au kuwepo kwenye kazi hiyo kunakukutanisha na
watu muhimu ambao wanaweza kuisaidia biashara yako kukua. Kuwepo
kwenye ajira pia kunaweza kukupa wewe upendeleo fulani ambao
wafanyabiashara wengine hawawezi kuupata. Kwa wewe kuwa kwenye ajira na
kuziona hizo nafasi vizuri kutakuwezesha kuikuza biashara yako vizuri. Kwa
kuchoma meli moto kunakuzuia wewe kupata fursa hizi nzuri ambazo
zingeiwezesha biashara yako kukua.
Kumekuwa na ushauri kwamba unaweza kuacha kazi kama umeshajiwekea
akiba ya angalau miezi sita ya kuishi bila ya kuitegemea biashara yako. huu nao
ni ushauri mzuri sana, lakini bado changamoto ni kubwa sana. Kama ambavyo
tumeshaona, hali ya uchumi haitabiriki. Unaweza kupanga kwamba kwa miezi
sita unahitaji kiasi fulani cha fedha kuishi, lakini unapokuwa tayari
umeshaondoka kwenye ajira mambo yakabadilika. Na pia bado kuna dharura
ambazo huwezi kujua zitakuja kwa kiasi gani na hivyo chochote unachopanga
kinaweza kisikutoshe kwa muda uliopanga. Hapo bado hujaangalia mwenendo
wa biashara yako kwa miezi hiyo sita, ni mara chache sana biashara inaweza
kuwa imeshaweza kujiendesha yenyewe ndani ya miezi sita. Biashara nyingi
zinahitaji muda mrefu zaidi ya hapo ili ziweze kujiendesha mwenyewe. Hivyo
hata kama unaweza kuweka pembeni kipato cha kukutosha kwa miezi sita,
usichome meli moto.
14
Unapokuwa kwenye njia panda ya kuacha kazi na kuingia kwenye biashara au
kuendelea na ajira na kuacha biashara, mimi nakushauri usichome meli moto.
Fanya vyote kwa pamoja na kazana sana kuhakikisha unaifanya biashara yako
kusimama kama kweli unachotaka ni kupata uhuru wa kipato. Kwa haya
tuliyojadili hapa kuhusu kutokuchoma meli moto unaweza kuona kama nakupa
woga wa kutokuondoka kwenye biashara, lakini ninachofanya hapa ni
kukuonesha ukweli halisi ni upi. Kwa sababu watu wengi wamekuwa wakifanya
maamuzi kwa mihemko au wakiwa na hisia kali na hivyo wanashindwa kufikiri
kwa kina. Baadaye wanapojikuta kwenye wakati mgumu ndiyo wanagundua ya
kwamba walifanya makosa makubwa. Usichome meli yako moto, badala yake
kaa kwenye meli hiyo na pambana ukiwa ndani ya meli mpaka uhakikishe
umeshinda vita ya kujijengea uchumi imara.
15
JIPATIE KITABU UENDELEE KUSOMA. Kama umependezwa na hizi sura mbili za kitabu ulizosoma, jipatie kitabu kamili
ili uweze kujifunza kwa undani zaidi na uweze kuchukua hatua.
Kwenye sura za mbele kuna biashara unazoweza kuanza kufanya ukiwa bado
umeajiriwa, uwekezaji unaotakiwa kufanya na pia kuna mifereji nane ya kipato
unayotakiwa kuanza kuitengeneza. Na katika kila mfereji kuna uzuri wake na
changamoto zake.
Pia kuna mbinu za kuilinda kazi yako dhidi ya mkataba wako wa ajira na hata
majungu ya wafanyakazi wenzako hasa pale biashara yako itakapoanza
kuonesha mafanikio.
JINSI YA KUPATA KITABU HIKI;
Kitabu kinatumwa kama nakala tete yaani softcopy kwenye mfumo wa pdf.
Kwa mfumo huu unaweza kusoma kitabu hiki kwenye simu yako kama ina
uwezo wa kusoma vitabu na pia unaweza kusoma kwa kutumia kompyuta.
Unatumiwa kitabu hiki kwa njia tatu, utachagua ile unayotaka wewe;
1. Kwa njia ya wasap, unaweza kutumiwa kwenye namba yako ya wasap na
ukapakua kusoma.
2. Kwa njia ya telegram, pia unaweza kutumiwa kwenye namba yako ya
telegram na ukapakua kusoma.
3. Kwa njia ya email, unaweza kutumiwa kitabu hiki moja kwa moja kwenye
email yako.
Gharama ya kitabu hiki ni shilingi za Kitanzania elfu kumi tu (tsh 10,000/=). Ili
kupata kitabu hiki tuma fedha kwenye namba zifuatazo;
1. Kama unatumia M- PESA tuma kwenda namba 0755 953 887 (jina AMANI
MAKIRITA)
2. Kama unatumia TIGO PESA au AIRTEL MONEY tuma kwenda namba 0717
396 253 (jina AMANI MAKIRITA)
3. Kama upo nje ya Tanzania tuwasiliane kwa wasap 0717 396 253 au email na
nitakupa utaratibu mzuri wa kulipia kulingana na ulipo.
16
Ukishatuma malipo ya kitabu, tuma ujumbe wa kawaida au wasap kwenda
namba 0717 396 253 wenye jina la kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA na
utatumiwa kitabu hiki kizuri.
Karibu sana rafiki yangu, ujipatie kitabu hiki ambacho kitakuwezesha kuanzisha
na kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.