mada: itikadi na ufundishaji wa nadharia za uhakiki wa

15
MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA FASIHI Richard Makhanu Wafula Department of Kiswahili Kenyatta University P. O.Box 43844, Nairobi, 00100 Februari 2015 Email: [email protected]

Upload: others

Post on 28-Oct-2021

10 views

Category:

Documents


0 download

TRANSCRIPT

Page 1: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA FASIHI

Richard Makhanu Wafula

Department of Kiswahili

Kenyatta University

P. O.Box 43844, Nairobi, 00100

Februari 2015

Email: [email protected]

Page 2: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

Itikadi na Ufundishaji wa Nadharia za Uhakiki wa Fasihi

Ikisiri

UFUNDISHAJIwa nadharia za uhakiki wa fasihi ulipoanza, ilifikiriwa kwamba hatimaye fasihiimefanikiwa kupata silaha za kiuhakiki na kiakademia za kutegemewa. Wahakiki nawananadharia wa Kimagharibi kama Wellek na Warren (1946) walifikiria kwamba nadharia yauhakiki wa fasihi ilikuwa moja popote fasihi iliposomwa. Hivi sasa katika kame ya 21, nadhariani nyingi na zinaendelea kuundwa kuendana na mazingira anuwai ambamo wahakikiwanapatikana. Makala haya yananuia kuonyesha kwamba wingi wa nadharia zilizopounaashiria mchomozo wa itikadi zinazoratibisha kuwepo kwa nadharia hizo . Japo Wellek naWarren walikuwa wakizungumzia kuhusu nadharia katika umoja wake, walikuwa wakiitikiamaswala ya kiitikadi. Jambo hili linahusu fasihi ya Kiswahili vilevile.

Maneno muhimu: nadharia, uhakiki, itikadi

Abstract

It was assumed that the teaching of theories of literary criticism ushered in an era whenliterature had begotten its ultimate critical and academic weapons. Western critics and theoristssuch as Wellek and Warren (1986) thought that theory was always singular and its rale uniformwherever it was applied. Now, in the zi" century, there a praliferation of many theories andwhat is more, others are being churned out and applied congruent to the home environments inwhich critics find themselves. The intention of this paper is to show that ideology in its variousguises has played and continues to playa crucial role in the formulation of those theories. Evenas Wellek and Warren were talking about the singularity of theory, they were in fact beingideological. This applies to Kiswahili literature as well.

Keywords: Theory, Criticism, Ideology.

1.1. Utangulizi

Lengo la makala haya ni kuonyesha dhima ya itikadi katika ufundishaji wa nadharia za

uhakiki wa fasihi. Itikadi kama inavyoeleweka sasa ina uwezo mkubwa wa kuifinyanga

nadharia ili nadharia hiyo ipondokee mtazamo maalumu na mahsusi. Kabla ya kuonyesha

jinsi itikadi inavyoweza kuathiri mwono wa nadharia, inajuzu kujifahamisha japo kwa kifupi

maana ya itikadi.

Page 3: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

1.2. Maana ya Itikadi

Itikadi ni istilahi ya kimsingi katika nyugo za kiutamaduni, za fasihi na taaluma zinazohusu

filamu. Maana ya istilahi 'itikadi' kiasilia inatokana na maandishi ya mwanafalsafa wa

Kijerumani, Karl Marx na mwenzake Friedrich Engels (Abdulla, Mansur na wenzake, 2014).

Katika uchanganuzi wao wa kimsingi wa jamii, walifafanua itikadi kama

dhana na imani za tabaka tawala katika kipindi maalumu. Dhana na imani za tabaka tawala

ndizo hutamalaki taratibu za kuunda fikra, mawazo na mielekeo ya wanajamii kwa ujumla.

Kwa hivyo, mfumo wote wa fikra za tabaka tawala ndio unajenga itikadi ya jamii fulani.

Kulingana na Marx na Engels, dhima ya itikadi ni kuhuisha upya zana za kuzalisha mali na

Kuhakikisha kwamba tabaka tawala linajiimarisha. Kwao,itikadi hupotosha na kuharamisha

ukweli. Ijapokuwa mgawanyo wa jamii kati ya watawala na watawaliwa umeundwa

na mtu kwa minajili ya kuhudumia mfumo wa kiuchumi, itikadi huhalalisha na huthibitisha

mgawanyo huo. Watawaliwa hukubali hali ya ukengeushi ambayo kwa kawaida wangeasi

dhidi yake. Hali hii ya ukengeushi imediriki kuitwa "ung'amuzi"potoshi"(Eagleton, 1991).

Dhana ya itikadi kama ilivyofikiriwa na kuwasilishwa na Marx na Engels imesailiwa na

Kupanuliwa ili itangamane na mabadiliko ambayo jamii imepitia tangu karne ya 19. Mabadiliko

makubwa ambayo yamefanyika ni kwamba uchumi kama kigeu imara kisichobadilika na

ambacho hutegemeza mgongano wa kitabaka umepoteza mashiko yake. Wahakiki wa

kiutamaduni hasa wale wanaohusishwa na mkondo wa kisasaleo wanasema kwamba vigeu

vya kukiritimba mamlaka na uchumi ni vingi vikiwemo jinsia, mfumo wa kuumeni na kukeni

rangi ya mtu, kabila lake na taifa anamotoka.

Naye mwanafalsafa wa Kitaliano anayeitwa Antonio Gramsci (1971) ameinyambua dhana ya

itikadi vingine. Kinyume na kutumia kishazi cha " ung'amuzi potoshi" kama walivyodai Marx na

Engels, anaunda na kutumia dhana ya hegemonia. Gramsci anadai kwamba itikadi hupata

mamlaka na uhalali kutokana ikibali ya hiari wala si kwa kutumia nguvu. Juu ya haya,

anafikiria kwamba itikadi ni seti ya mawazo na matendo wanayofanya wanajamii ili kuhalalisha

mfumo unaotawala. Miongoni mwa mawazo haya ni kaida zinazochukuliwa kuwa mazoea ya

kila siku ya mtu( Forgacs, 2000). Kwa hakika usuli wake ukisakwa, itabainika kwamba mawazo

hayo yaliundwa ili kuhudumia kikundi mahsusi. Mfaransa Louis Althusser aliyanyambulisha

Page 4: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

mawazo ya Gramsci na kung'amua kwamba kuna zana aina mbili za kuchipuza na kuendeleza

utawala; nazo ni zana nyamazishi na zana za itikadi za taifa(1971}. Zana nyamazishi au zana

gandamizi ni kama jeshi, polisi na jela. Kwa upande mwingine, zana za itikadi za taifa ni kama

vyombo vya habari, mfumo wa elimu, dini na familia. Itikadi na usemi (diskosi) ndio msingi wa

kuwasilisha dhana, imani na kaida.

1.3. Itikadi na Nadharia za Uhakiki wa Fasihi.

Baadhi ya mikondo ya kuelezea itikadi imeathiri jinsi nadharia zilivyoundwa na zinaendelea

kuundwa na kushughulikiwa kiusomi. Itikadi ni zana yenye mamlaka makubwa ya kuratibisha

usemaji wa kinadharia katika uhakiki wa fasihi. Maana mbalimbali za nadharia na viashiria

vingine vinavyohusishwa nazo vikichunguzwa kwa upekuzi, itagunduliwa kwamba nadharia

zimeingiliwa pakubwa na itikadi. Masuala kama nadharia ifikiriwe katika hali ya umoja au hali

ya wingi, nadharia kuwa mwongozo wa uhakiki, nadharia kuwa sheri a za uhakiki, nadharia

kuwa mikakati ya kusoma, nadharia kuwa usomaji unaozingatia ujarabati, nadharia kuwa

uhakiki wa kimfumo, nadharia kuwa muktadha wa kazi ya fasihi husika na nadharia kama

usemaji unaolenga kumiliki aina nyingine za usemaji yanategemea itikadi katika viwango

anuwai ambavyo watalaamu wameainisha. Tutaonyesha jinsi itikadi imeathiri ufasiri na

ufundishaji wa nadharia katika aya zifuatazo hivi karibuni.

1.4. Umoja na Wingi katika Ufasiri wa Maana ya Nadharia za Uhakiki

Wahakiki wa fasihi hasa wale walioandika katika miaka ya 1920 hadi miaka ya 1960 kama

Wellek na Warren walifikiria kwamba dhana ya nadharia ya uhakiki wa fasihi ni moja. Kwa

Mujibu wa mawazo yao, nadharia ilitazamiwa kueleza na kufafanua maana ya fasihi, dhima ya

fasihi na viwango mbalimbali vya ubora wa fasihi. Mtazamo wa Wellek na Warren ulifikia kilele

wakati wa umuundo, Uhakiki Mpya na umaumbo. Ijapokuwa nadharia ya Uhakiki Mpya

ilichipuka kipekee na kivyake inashabihiana kwa sifa nyingi na umuundo na umaumbo. Waasisi

na waitifaki wa nadharia hizi zote walifikiria kwamba lugha ya fasihi ina sheria mahsusi za

kipekee popote inapotumiwa. Lugha hiyo ya fasihi hujirejelea yenyewe kwa kuzitangaza sifa

zake. Wellek na Warren waliandika kitabu chao, Theory of Literature (1986) kuashiria

Page 5: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

mtazamo na mwelekeo huu. Kwao, nadharia ilikuwa moja tu. Dhamira yao ilikuwa kutafuta

msimbo wa kibia wa kuchanganulia fasihi. Isitoshe, kwao kazi za sanaa ni minara inayosifika

kwa vile imehifadhiwa kimaandishi. Fasihi simulizi haikuwa moja kati ya taaluma mashuhuri

katika mitaala yao. Hii ilikuwa itikadi ya kukiritimba uainisho na usomaji wa fasihi.

Ndio sababu wataalamu waliokulia kwa ziwa la Wellek na Warren walipoanza kutembea hasa

barani fasihi za kienyeji hazikuwashugulisha asilani ijapokuwa zilikuwa zimeimarika vya kutosha

katika vyuo vikuu vya Kimagharibi . Uamuzi wa kutofundisha sanaa za Kienyeji kifasihi ulikuwa

wa kiitikadi.

Hata hivyo, njia nyinginezo za kuudurusu ulimwengu zilipozuka wahakiki wengi hasa wa

pembezoni (Dunia ya Tatu) walikatikiwa Kung'amua kwamba maadamu kuna washindani

chekwachekwa katika medani ya kusoma, Kufikiria, na kutathmini, basi kuna njia nyingi za

kuzungumzia utaalamu tofauti tofauti. Nadharia za uhakiki ni kama njia nyingi teule za

kuzungumzia ujuzi wa kifasihi, zimo mashindanoni na zinazoshinda kidesturi ndizo huhesabiwa

kuwa teule zaidi kadamnasi ya nyinginezo. Nadharia zinazoshinda kwa kurejelewa mara kwa

mara na kutumiwa si lazima ziwe sahihi na kuhudumia wanajamii wote kwa mafanikio. Kwa

hivyo, hivi sasa nadharia ni nyingi na hutumika Kutegemea mahitaji mbalimbali vikundi anuwai

vya wanajamii.

1.5. Nadharia kama Mwongozo wa Kuhakikia

Nadharia inaweza kuchukuliwa kama mwongozo wa kumsaidia msomaji kufahamu kazi ya

sanaa vizuri zaidi. Nadharia ni mkataba usiokuwa rasmi kati ya msomaji na mtunzi. Mhakiki

kama msomaji anapoyaweka mawazo ya mtunzi katika utaratibu mahsusi ili yaweze

kutathminika pasi kuweka masharti maalum, basi nadharia yake itakuwa kama mwongozo.

Katika ushairi wa Kiswahili, wahariri na wahakiki kama Shihabuddin Chiraghdin na Abdilatif

Abdalla wanazungumzia ~itanzu vya mashairi kimaudhui pasi kuonyesha mipaka yake mahsusi.

Idadi ya vitanzu inategemea masuala yanayoendelea kuibuka. Katika utangulizi wake wa

Malenga wa Mvita (1970), tungo zilizosanifiwa na Juma Bhalo, Chiraghdin hazungumzii

muundo wa ushairi. Suala la muundo ni kaida na halimshughulishi asilani. Alipouandika

utangulizi wake, muundo tengemano wa shairi kama alivyofahamu hakukuwa umetishwa wala

kuvurugwa na yeyote. Alilirejelea tu pale alipowajibika kuwaonya na pengine kuwaelekeza

Page 6: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

washairi chipukizi. Kwa hivvo, Shihabuddin Chiraghdin alivaainisha mashairi va Ahmad Nassir

katika rnagawanvo manne: Mbinu za Lugha, Mawazo na Maliwazo, Baina va Mume na Mke, na

Majonzi na Makiwa. Uainisho huu ni ithibati tosha kuonvesha kwamba si lazima ushairi wa

Kiswahili ufikiriwe kimuundo kila mara mijadala va kinadharia inapozuka.

Diwani ya Ustadh Nyamaume navo iliandikiwa uhariri wake na Abdilatif Abdalla. Abdalla

anashabihianana Chiraghdin katika kubainisha ushairi wa Nvamaume kimaudhui. Hata hivvo,

rngawanvo wa Abdilatif haufanani sarafu kwa va pili na rngawanvo wa Shihabuddin Chiraghdin.

Ana mashairi vanavohusu: Kuusemea Ushairi, Malimwengu, Kushauri na Kunasihi, Kuimbana

Kishairi, Kufumba na Kupiga Mifano na Kutoa Heko. Kutokana na ukweli huu tunaweza

kuhitamidi kuwa uainisho wa ushairi wa Kiswahili kimaudhui ni rnnvumbufu kwa vile maudhui

rnapva vanawezakuibuka na kusababisha uundaji wa makundi rnapva va ushairi kimaudhui.

Kwa upande mwingine mijadala kuhusu muundo wa shairi la Kiswahili ilianza kudhihirika kwa

makali baada va kutungwa kwa diwani va Euphrase (1974), Kahigi na Mulokozi (1976) na

Mulokozi na Kahigi (1979). Shihabuddin Chiragdin alilihisi wimbi la watunzi hawa ambao kwa

wakati huo walikuwa wakereketwa kiasi na kusemezana na ushairi wao katika utangulizi wa

Malenga wa Mrima (1977). Sasa mashairi havakuainishwa kimaudhui kama ilivvofanvwa

kingaubaga katikaMalenga wa Mvita. Mhariri wa Malenga wa Mrima alijipa fursa va

kushambulia mashairi vasivofuata arudhi. Jambo hili Iilishadidiwa na Hassan Msami katika

tahakiki vake va Malenga wa Vumba (1982) . Katika tahakiki hivo, alitambua kueleza sifa za

bahari kumi na nne kimuundo. Bahari Hizo ni: kikai, msuko, sakarani, mtiririko, ukara,

ukaraguni, kikwamba, msuko wa kikai, tathlitha, tarbia, takhmisa, ukemi, pindu na utenzi.

Ulinganifu na tofauti zilizokuwepo kuhusiana na mgao wa ushairi katika makundi mbalimbali

ulisababishwa na itikadi va wasomi na wadau wengine waliohusika. Itikadi inatuwezesha

kuelezea utamaduni, elimu na aina nvlngine za usemaji uliozowewa ulioratibu uainisho wa

ushairi. Katika mazingira va sanaa za Kimagharibi nadharia kama mwongozo inadhihirika katika

matamshi va Aristotle katika tahakiki vake va Poetics (1965). Aristotle aliorodhesha na

kufafanua sifa na mazoea va Wavunani kuhusu utunzi wa tamthilia. Alifanva hivvo bila

kuwashinikiza watunzi na wahakiki kufuata alivovashuhudia. Aristotle aliishi katika demokrasia

kiasi na inawezekana kwamba ukosefu wa shinikizo katika tahakiki vake inadhihirisha itikadi hii.

Page 7: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

1.6. Nadharia kama Sheria ya Kutunga na Kuhakiki

Nadharia kama sheria za kutunga na kuhakiki kazi za fasihi zilipigiwa debe na mhakiki wa

kiroma, Horace Katika tahakiki yake Ars Poetica na kufufuka katika kipindi cha urasimi mpya wa

Kimagharibi. Katika wakati wa Horace, milki ya Uroma ilikuwa na nguvu nyingi za kisiasa. Lakini

Kwa upande wa utamaduni, milki ya Uyunani ambayo ilikuwa imedidimia na kuporomoka

iliendelea kukiritimba ushawishi mkuu. Yaani Uyunani iliendelea kuutawala ulimwengu wa

Kimagharibi kiutamaduni.

Katika mawanda ya fasihi, Waroma waliiga mitindo ya kiutunzi na kiuhakiki wa Kiyunani.

Katika kipindi chote ambacho Waroma waliutawala ulimwengu wa kale, lugha ya kiyunani

lIikuwa wa pili na ya lazima miongoni mwa Waroma walioelemika. Lakini kiitikadi, Waroma

Waliongozwa kwa amri. Juliasi Kaizari na watawala wote waliokuja baadaye walikuwa

madikteta. Jambo hili lilidhihirika katika mfumo wa elimu na wa kiusomi wa kipindi kile.

Alipokuwa akiwafundisha wanawe Piso katika Ars Poetica, Horace alionya:

nitamfundisha mshairi kazi yake na majukumu yake.Nitamfundisha mahali atakapopata malighafi ya kaziyake, yale yatakayokuza na kupapalia kipawa chakecha kutunga ushairi, yale ambayo anapaswa kufanyana yale asiyopaswa kufanya, mahali ambapo njia nzuriitamwelekeza na mahali ambapo njia mbaya itampeleka( Horace, Ars Poetica katika Dorsh, 89-90)

Horace anaendelea kuwaonya wanafunzi wake kwa kusema kwamba:

Ukitaka tamthilia yako kufurahiwa na kuigizwa maranyingine, tamthilia hiyo isiwe na matendo yanayozidiau yanayopungua matano. Matendo yanayosababishwana majaliwa au nguvu za kiungu yasiingizwe katikatamathilia isipokuwa hali ngumu itokee inayoshurutishamaingilio ya mkono wa kiujiza. Na usiwe na wahusikawanaozidi watatu kwenye jukwaa kwa wakati mmoja(Horace, Ars Poetica, katika Dorch, 85)

Ni bayana kwamba kauli hizi ni amri, ni sheria inayohusu namna ya kushughulikia sanaa

Page 8: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

va kutunga na kuihakiki tamthilia. Hizi ni sheria za Horace. Zinatofautiana pakubwa na jinsi

Aristotle alivvoonvesha mchakato wa kutunga na kuihakiki tamthilia. Mazingira va Horace

aliithiri jinsi alivvolurnba kauli zake. Yaani, itikadi va kutoa amri arnbavo ilikuwa imekolea katika

usemaji wa Makaizari uliingilia moja kwa moja kauli za Horace.

1.7. Nadharia kama Mkakati wa Kusoma

Itikadi inaweza kuathiri nadharia na kuikabidhi nadharia hiyo sura va mkakati wa kusoma. Kazi

mbalimbali za sanaa zinaweza kuhakikiwa kwa kutumia nadharia ile ile moja. Lengo la kufanva

hivvo ni kutathmini uwezo wa nadharia moja katika ufafanuzi wa kazi mbalimbali za fasihi. Hali

alivorno msomaji katika kiwango hiki ni mathalan va maabara ambapo mikakati va kusoma

inajaribiwa na ile isivohitajika hudumazwa ilhali inavothaminiwa na msomaji hupewa

uchomozo zaidi. Mbali na havo, nadharia anuwai zinaweza kutumiwa kukisoma na

kukichanganua kitabu kimoja kwa nia va kuonvesha na ipi inavofaa zaidi katika usomaji wa

kitabu fulani na ni ipi haifai. Kaida hii va uhakiki inapotumiwa wachanganuzi watachukulia va

kuwa baadhi va nadharia zina ushawishi mkubwa hata kabla va kufanviwa majaribio katika

mazingira vovote.

Katika tasnifu nvlngi zilizoandikwa katika Chuo Kikuu cha Nairobi katika mwongo wa 7 na

mapema mwongo wa 8 wa karne ilivopita, nadharia llivotumlka zaidi kuhakikia kazi za fasihi

ilikuwa va uhalisia wa kijamaa au Umarx. Pamoja na hava, maswala valivohusu ubia na upekee

wa fasihi valitazamwa katika darubini va Uleninisti. Jambo hili halikufanvwa kwa kuzingatia

uwajibikaji wa uhakiki bali ulitilia maanani zaidi fahari ilivohusishwa na kufikiria kimaendeleo

au kimapinduzi. Wakati mwingine, watafiti walifanva uchanganuzi kwa kutumia silika zao

ijapokuwa walikuwa wametimiza masharti va mapendekezo kwa kupachika uhalisia wa kijamaa

au upembuzi wa kimarx katika sehemu ilivohitaji kujalizwa nadharia. Itikadi va ujamaa ilikuwa

njia sahihi va kufikiria na hakuna , hata asivekuwa mjuzi alivethubutu kuachwa nvurna wala nje

katika rnparanvo huu. Hili lilikuwa swala la kiitikadi.

Page 9: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

1.8. Usomaji unaozingatia Ujarabati

Huu ni usomaji ulioathiriwa na mielekeo na mitazamo ya kufikiria yenye mashiko katika sayansi

asili. Ujarabati ni ufafanuzi wa ujuzi unaozingatia tu mambo halisi yanayoonekana,

yanayoshikika na yanayohisika kwa fikra na mishipa ya fahamu ya mtu. Mhakiki anapotumia

nadharia zenye mwelekeo huu, huwa kama mchunguzi wa majaribio yanayojaribiwa kwenye

maabara. Nadharia za umaumbo na vipera fulani vya nadharia za kimtindo hasa zile

zinazotegemea uthibitisho wa kitakwimu ni za kijarabati. Marehemu Jay Kitsao (1982) alitumia

nadharia ya kimtindo na kitakwimu kiuchangamano kuandaa tasnifu yake ya uzamivu. Katika

muktadha huu, usanii unaainishwa kwa idadi ya jazanda na vipengele vingine vya uchomozo

alivyovitumia mwanasanaa. Isitoshe mwanasanaa bi nafsi anaweza kutambulika kwa matumizi

ya msamiati, urefu wa sentensi na hata uradidi wa kipekee. Mwelekeo kama huo ndio

uliwalifanya wahakiki kama Buffon( 1930) kung'amua kwamba mtindo ni mtu. Vilevile, hii

ilikuwa kaida ya kusoma fasihi kisayansi na wana-maumbo wa Kirusi.

Kigezo cha uchomozo kilisisitizwa zaidi na wana-maumbo wa Kirusi katika kubainisha tanzu za

fasihi. Ushairi ulihusishwa na usanii zaidi kuliko riwaya na tamthilia kwa kuwa una sifa bainifu

zaidi kama vina, mizani na wizani. Kuna dhana ya "uhuru wa kishairi" ambao hauhusu ushairi

peke yake bali tanzu zote za fasihi. Kwa mujibu wa wana-maumbo wa Kirusi ukiushi ulikuwa

ushahidi wa kuwepo kwa usanii na ulitambulika zaidi katika ushairi. Mambo haya yalitokea

kwa sababu za kiitikadi. Pengine wahakiki hao walikuwa wanajaribu kuepukana na maswala ya

kiharakati kwa sababu za kiusalama au walifikiria kwamba kuchopeka usayansi asilia katika

uhakiki wa fasihi kuuliiletea fasihi fahari na umashuhuri.

Page 10: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

1.9. Nadharia kama Usomaji Kimfumo

Kuna mwelekeo unaoshikilia kwamba ili kazi va fasihi ishughulikiwe katika vipengele vvake

vvote, inapaswa kuhakikiwa kimfumo. Mwelekeo huu unaongozwa na mtazamo kuwa mtunzi

anapotunga kazi va sanaa, kila neno, kishazi, sentensi na alama va uakifishaji ina lengo

maalumu. Kila kipashio kimewekwa katika kazi hivo kimaksudi. Hivvo basi, hakuna chochote

kinachostahili kuupuzwa. Moja kati va njia za zamani za kusoma kazi za fasihi na zilizosifika sana

ni ile inavogawa fasihi katika mawanda mawili; vallvorno na jinsi valivorno vanavvowasilishwa,

Nadharia inachukulia va kwamba shairi, tamthilia na shairi ni kazi za fasihi

ambazo zina vipengele mbalimbali. Kila kipengele kinapaswa kuelezwa katika muktadha wa

vipengele vingine. Bila kuwepo uhusiano huu wa kujengana na kukamilishana, kazi va fasihi

haitakuwa kamili. Mtazamo wa aina hii unapalilia wazo kwamba kazi va fasihi imejitosheleza na

haihitaji muktadha wa nje ili kuikamilisha.

Hatirnave dhana va ufu wa mwandishi imetokana na nadharia hii. Uhakiki unaornnvirna

mwandishi nafasi muhimu katika ufahamu wa kazi vake vilevile unaikengeusha hivo kazi

kutokana na muktadha ulioizalisha. Hapa itikadi inaikabidhi sanaa lengo la kiujumi bila

kuhusisha ule ujumi na maswala va kidhamira va mwandishi. Fikra kwamba lengo la kazi va

fasihi linaweza kutofautiana na dhamira va mwandishi wa kazi hivo inatokana na mtazamo huu.

UKweli ni kwamba ufasiri wa kutegemewa wa kazi ya fasihi utafafanua dhamira na mtindo wa

kazi inayohusika katika vipengele karibu vvote. Haiyumkiniki kuwa kati va vipengele hivvo,

mhakiki atakosa kutaja alivokusudla mtunzi asilia asilani. Kazi zote za fasihi ni aina fulani va

majazi vaani zinaweza kufahamika katika viwango mbalimbali vVa ufasiri. Kuna mkufu wa

kuashiria na kumaanisha kutegemea miktadha tofauti anavorejelea mhakiki. Miktadha hivo

inaning'inia kati va lugha dhahania na lugha tendakazi anavoiturnia mwandishi.

Nadharia va baada-ukoloni miongoni mwa nadharia nvingine za kisasaleo inathamini mwandishi

na muktadha uliomchipuza kwa arnbavvo inarejelea mitazamo va kiutamaduni na va kibinafsi

ambayo inapatikana nje va matini ilivoandikwa. Maana zinaweza kuwa nyingi na tofauti lakini

zitakuwa na dhima kubwa kwa waliokusudiwa kwa kufasiriwa kimkutadha.

Page 11: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

1.10. Nadharia kama Usemaji Unaolenga Kutawala Ujuzi

Katika mataifa mengi ya zama hizi, nadharia za uhakiki wa fasihi zimekuwa usemaji unaotumiwa

na wanajamii kuwatawala wanajamii wengine. Wananadharia kama Michel Foucault, Jacques

Derrida, Jacques Lacan, Homi Bhabha, Gaytri Spivak, Edward Said, Achilles Mbembe, Valentin

Mudimbe, Anthony Appiah (Werbner & Ranger, 1996L wanafikiria kwamba njia teule za

usemaji zikiwemo nadharia za uhakiki wa fasihi zimeumbwa ili zitumiwe kuutawala ulirnwengu,

Kama ambavyo watawawala hujiteua na kujitenga katika matabaka maalum, njia za

kuzungumzia ulirnwengu pia zimegawanywa katika matabaka maalum. Katika kazi za

wananadharia walioorodheshwa hapo awali, juhudi zinafanywa kutukuza usemaji ambao hapo

kabla ulikuwa umedhalilishwa, kudunishwa na kupuuzwa. Kwa kufanya hivyo, njia mbalimbali za

kufikiria (yaani nadharia) zimepewa nafasi sawa za kuwatetea wanajamii ambao kwa kawaida

hawana majukwaa ya kujitetea.

Mfumo wa ukoloni ulitanguliwa na kuandamana na maandishi na masimulizi mengi kuhusu

maeneo yaliyolengwa kuwa makoloni. Waandishi kama Friedrich Hegel, Daniel Defoe na Conrad

waliandika maandishi yaliyosifu utu wa walionuia "kujitoa mhanga" na "kuyaokoa" maeneo

yaliyolaaniwa, maeneo yaliyokaliwa na II wana wa kambo" wa Mwenyezi Mungu. Wakati

huohuo, maandishi have yalionyesha uduni wa maisha ya waliolengwa kutawaliwa katika

mfumo wa ukoloni. Mwandishi na mhakiki anayepinga mtazamo kama huu anapaswa kujihami

na usemaji teule (nadharia) ambao utahalalisha kuwepo kwake na utu wake. Ngugi wa Thiong'o

(1998) na Chinua Achebe (1988) wamekuwa katika mstari wa mbele wa kuunda kauli

zinazotetea utu wa Mwafrika. Kwa kuunda kauli hizo wamejaribu kuratibisha usemaji

unaopaswa kutawala mtazamo wa maisha katika maeneo vallvotawaliwa chini ya mfumo wa

ukoloni na ambayo yanaendelea kuathiriwa na matokeo ya matendo yaliyofanywa wakati wa

ukoloni. Nadharia za kifeministi zinapatikana katika mkumbo huu wa kufikiria vilevile. Kwao

wafeministi, nadharia za uhakiki wa fasihi ni vichochoro vya mikabala ya kubainisha na kueleza

jinsi wanawake na wanaume wanavyohusiana katika jamii ambazo kwa muda mrefu

zimeongozwa kibabedume. Kama wanavyosema Belsey na Moore:

Page 12: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

Kwa mujibu wa wanachuo na wasomaji wa kifeministikila usomaji una mwelekeo maalum juu ya matini inayosomwa.Uchanganuzi wa aina yoyote una malengo na mielekeo ya kisiasa.Usomaji ama unashadidia mabadiliko katika kizazi cha mtu au kusitishamchapuko wa kutokea kwa mabadiliko hayo (1997:1).

Kama inavyodhihirika katika haya maelezo, nadharia za kileo hasa zile ambazo zinaelekeza

usomaji na uchanganuzi wa fasihi baada ya umuundo na umaumbo zinakusudia kuumbua

matamshi mateule ya kimapokeo kuhusu fasihi na maudhui yake. Baada-ukoloni na ufeministi

ni mifano michache ya nadharia hizi. Hata hivyo, isidhaniwe kwamba nadharia zinazojengua

uteule wa baadhi ya masimulizi kuhusu hali ya binadamu zinalingana katika vipengele vyake

vyote. Ijapokuwa uumbuzi unapiga mwangwi katika Baada-ukoloni na ufeministi, malengo ya

baada-ukoloni na ufeministi yanapiku uumbuzi. Hizi nadharia zina malengo ya kisiasa na

kiitikadi. Hivyo basi, waumbuzi hawakubaliani kwa kila jambo. Mawazo ya Belsey na Moore

kuhusu malengo ya kwanza ya udenguzi yanalishadidia jambo hili:

... tokea mwanzo, uhakiki wa kiumbuzi kuhusu jinsia ulikusudiakulikengeusha swala la uana kutokana na utamadunina ujumi au sanaa kwa ujumla (1997:9).

Maoni ya wahakiki hawa ni kuwa kwa kulipuuza swala la jinsia, uumbuzi ulikuwa unaendeleza

itikadi ya kibabedume. Ijapokuwa ufeministi unashirikisha na kutumia baadhi ya mihimili ya

uumbuzi, malengo yake ni tofauti kabisa kutokana na malengo ya uumbuzi. Uumbuzi unahusu

zaidi udenguzi wa lugha na mifumo wa uashiriaji wake bila kuzingatia amali mbalimbali

zinazobebwa na hiyo lugha. Kinyume na haya, ufeministi unatilia mkazo lugha kama kiashiria

kinachotumiwa kuelezea mahusiano ya wanajamii katika misingi ya jinsia. Maswala ya kisiasa na

ya kijamii hayawezi kuepukika katika usomaji wa kifeministi.

1.11. Nadharia Katika Siku za Halafu

Nadharia zitaendelea kuwepo na kuratibu na kuhamasisha usomaji na ufundishaji wa fasihi.

Hata hivyo zitabadilika kila kukicha endapo maswala mapya yatazuka ambayo yatahitaji

maelezo ya kipekee na kivyake kinadharia. Hayo maswala mapya yatakuwa ya kiitikadi

Hatimaye, ikidhihirika kwamba nadharia zilizopo hazina manufaa kiitikadi, zitalazimika kusalimu

Page 13: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

amri (kuhifadhiwa katika makavazi) ili nadharia nvlnglnezo zichipuke na kutimiza haja za

walimwengu waliopo.

Baadhi va nadharia zinazungumziwa na jamaa ambao wamekengeuka kutokana na jamii au

vikoa wanavvowakilisha. Wengi wa wananadharia wanaozungumzia Baada-ukoloni hawaishi

katika miji mikuu va maeneo vanavornilikiwa na ukoloni na athari zake na arnbavo

wavaendelea kunvonvwa na mfumo wa kibepari wa kimataifa. Nadharia hazitazungumziwa

kiakademia peke vake: zitapaswa kuhusishwa na hali thabiti wanamoishi watu. Kwa sababu va

tofauti za kiuchumi kati va watu na kwa sababu va maonevu va aina nvingi vanavcendelea

kuonveshwa na mtu dhidi va mtu mwingine, nadharia zinazotalii mahusiano kati va watu

zitaendelea kushamiri. Nazo nadharia ambazo hazijakita katika maisha va watu na kuathiri hali

halisi za maisha vao kama uumbuzi zitaendelea kufifia. Lakini baadhi va mikakati vake va

kuutazama ulimwengu haitafutika.

1.12. Tamati

Katika makala hava tumeonvesha va kwamba itikadi inaendelea kuathiri namna va kusoma na

kuchanganua kazi za fasihi. Matamshi mateule arnbavo wahakiki wametongoa kuhusu nadharia

za uhakiki vamefumbatwa katika itikadi kwa malengo vasivohusiana moja kwa moja na fasihi.

Page 14: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

Marejeleo

Abdalla, A. (1976). Utangulizi. Diwani ya Nyamaume. Nairobi: Shungwaya

Abdullah, M. na wengine (2014). "Dialectical Materialism". Ecyclopedia Britannica

(Mtandao)

Abedi, K. A. (1979). Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri. Nairobi:

Kenya Literature Bureau.

Achebe, Chinua (1988) Hopes and Impediments. London: Heinemann.

Althusser, Louis (1971). Lenin and Philosophy and Other Essays. Monthly Review.

Bakhtin, Mikhail (1989). The Dialogic Imagination: Four Essays. Trans. Michael Holquist &

Katerina Clark. Austin: University of Texas Press.

Belsey, Catherine & Jane Moore ed. (1997). The Feminist Reader. London: Macmillan.

Blamires, Harry (1990). A History of Criticism. London: Macmillan.

Bradford, Richard (1997). Stylistics. London: Routledge.Buffon, G (1930). Buffon's Discourse on Style. Paris: Librarie Hatier Publishers.Cohen, Ralph (1989). The Future of Literary Theory. New York &London: Routledge.

Daiches, David (1986). Critical Approaches to Literature. London: Longman.

Dorsch, S.T. (1965). Classical Literary Criticism: Aristotle/Longinus/ Horace.

Harmondsworth: Penguin.

Eagleton, Terry (1991). Ideology: An Introduction. London: Verso.

Forgacs, David (2000). The Gramsci Reader: Selected Writings 1916-1935. New York: NewYork University Press

Forster, Thomas (2003). How Read to Read Literature Like a Professor

New York: Harper Collins.

Foucault, Michel (1999). "Space, Power and Knowledge". The Cultural Studies Reader.

Ed. Simon During. London: Routledge

Gramsci, Antonio (1971). Selections from Prison Notebooks.

Page 15: MADA: ITIKADI NA UFUNDISHAJI WA NADHARIA ZA UHAKIKI WA

New York: International Publishers.

Harland, Richard (1999). Literary Theory: From Plato to Barthes: An Introductory History.

New York: St. Martins.

Keesey, D. (2003). Contexts for Criticism. London: Toronto Mayfield.

Kezilahabi, Euphrase (1974). Kichomi. Nairobi: Heinemann.

Kitsao, Jay (1982). An Investigation of Themes in Swahili Literature & the Application of

Stylostatistics to Chosen Texts. Unpublished PhD thesis, University of Nairobi.

Mulokozi, Mugybuso & Kahigi K. (1995). Malenga wa Bara. Dar es Salaam: Dar es Salaam

University Press.

Mulokozi, Mugyabuso & Kahigi K.(1979). Kunga za Ushairi na Diwani Yetu. Dar es Salaam:

Tanzania Publishing House.

Njogu, K. & R.M. Wafula (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi.

Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.

Shihabuddin, C. (1970). Utangulizi. Malenga wa Mvita. Nairobi: Oxford University Press.

Shihabuddin, C. (1977). Utangulizi. Malenga wa Mrima. Nairobi: Oxford University Press.

Wafula, R.M. (2014). Uhakiki Kama Mchakato wa Kutaalamisha Usomaji wa Fasihi. Journal of

Language Education and Linguistics Vol.8 Number 2. Dept. Of Foreign Languages:

University

of Dar es Salaam.

Wamitila, K. W. (2003) Kamusi ya Fasihi: Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus.

Wa Thiong'o, Ngugi (1998). Penpoints Gunpoints and Dreams. Oxford: Clarendon.

Wellek Rene & Austin Warren ( 1986). Theory of Literature. Harmondworth: Penguin.

Werbner, Richard & Terence Ranger ed. (1996) Postcolonial Identities in Africa.

London & New Jersey: Zed Books.

Kitawasifu

Dkt. Richard Makhanu Wafula ni mhadhiri katika Chuo kikuu cha Kenyatta ambapoanafundisha Nadharia za Uhakiki wa Fasihi, Fasihileo na Fasihi Linganishi.