hotuba ya mwenyekiti wa tume kwa wadau wa majimbo--
DESCRIPTION
Siasa za TanzaniaTRANSCRIPT
-
1
TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR
HOTUBA YA MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI MHE. JECHA
SALIM JECHA KATIKA MKUTANO NA WADAU WA UCHAGUZI KUHUSIANA NA KAZI YA UCHUNGUZI
WA IDADI, MAJINA NA MIPAKA YA MAJIMBO YA UCHAGUZI WA ZANZIBAR
Waheshimiwa Makamishna wa Tume ya Uchaguzi,
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Wakuu wa Vyombo vya Serikali;
Viongozi na Wawakilishi wa Vyama vya Siasa;
Viongozi wa Asasi za Kijamii;
Wawakilishi wa Vyombo vya Habari;
Maafisa wa Tume ya Uchaguzi;
Mabibi na Mabwana
Itifaki imezingatiwa
Asslam -Aleyikum
Nachukuwa nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha
kuwa pamoja tukiwa salama na wazima wa afya. Pili, nichukuwe nafasi hii
kutoa shukurani kwenu kwa kuupokea kwa mikono miwili mwaliko wetu na
-
2
kuhudhuria katika mkutano huu. Mwitikio huu unatupa imani kuwa mko na
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na mtaendelea kushirikiana nasi katika
utekelezaji wa majukumu yetu ya Kitaifa.
Waheshimiwa Viongozi, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeitisha mkutano
huu kwa madhumuni makuu matatu. Kwanza kabisa, kutoa shukurani kwa
msaada mnaoipatia Tume katika kutekeleza majukumu yake. Pili, kutoa taarifa
juu ya kazi kubwa ambayo imepangwa kutekelezwa na Tume katika kipindi
hiki na kuomba ushirikiano wenu katika kuifanikisha kazi hiyo. Na tatu, kutoa
maelezo ya namna ambavyo wadau tumewapangia utaratibu wa kutusaidia
kuifanya kazi hii mpaka kukamilika kwake. Na hatimaye tutatoa nafasi kwa
kuuliza maswali kwa pale ambapo panahitajia ufafanuzi juu ya kazi hii.
Katika mkutano huu hatukupanga kupokea maoni yenu, kwani tutakuwa na
muda mrefu wa kupokea maoni hayo kuhusiana na kazi hiyo baadaye.
Naomba tuusubiri muda huo na tuwe pamoja katika mkutano huu.
Waheshimiwa Viongozi, mwaka uliopita Wajumbe wote saba wa Tume ambao
wapo mbele yenu, mara tu baada ya kuapishwa kuwa Wajumbe wa Tume
tarehe 4 Mei 2013 walikutana nanyi katika mikutano ambayo lengo lake kuu
lilikuwa ni kujitambulisha kwenu na kuelezea majukumu ambayo
yatatekelezwa na Wajumbe hao katika kipindi cha miaka mitano ya utumishi
wao. Majukumu hayo kama vile:-
Usimamizi wa jumla wa mienendo ya uchaguzi wa Rais, Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wa Serikali za Mitaa;
Kuandikisha Wapiga Kura;
-
3
Kusimamia Daftari la Kudumu la Wapiga kura;
Kufanya mapitio ya mipaka ya Majimbo;
Kukuza na kuratibu Elimu ya Wapiga Kura; na
Kuendesha kura ya Maoni.
Waheshimiwa Viongozi, nachukua nafasi hii kuwajulisha kuwa Wajumbe wa
Tume kwa ushirikiano na msaada wa wadau wameanza kutekeleza majukumu
hayo. Katika kipindi cha mwaka mmoja cha utendaji wa Wajumbe hawa,
Tume imeendesha chaguzi ndogo tatu kujaza nafasi wazi Unguja na Pemba.
Chaguzi hizo ni uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ngombeni katika Baraza la Mji la
Mkoani uliofanyika tarehe 23 Juni 2013, Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la
Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi uliofanyika tarehe 02 Februari 2014 na
Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Kiboje Wilaya ya Kati uliofanyika tarehe 27 Aprili
2014.
Aidha, katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, Tume iliendesha jukumu la
Uandikishaji wa wapiga kura wapya na Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura. Kazi hii ilianza tarehe 29 Juni 2013 katika Wilaya ya Kaskazini
A na kumalizika tarehe 5 Novemba 2013, Wilaya ya Mkoani. Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar inatoa wingi wa shukurani kwa wadau wote vikiwemo
vyombo vya ulinzi na usalama, vyama vya siasa, vyombo vya habari, asasi za
kijamii na Viongozi wa Serikali katika ngazi ya Mikoa na Wilaya kwa
ushirikiano waliotupatia katika utekelezaji wa majukumu yetu kwa kipindi cha
mwaka mmoja uliopita. Ushirikiano huo kwa kweli umetuwezesha
kuyakamilisha baadhi ya majukumu niliyoyataja kwa mafanikio.
-
4
Kukamilika kwa chaguzi ndogo tatu na kukamilika kwa kazi za Uandikishaji wa
wapiga kura na Uendelezaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura
kusingewezekana kama mngeamua kuiachia Tume hii peke yake kuzifanya
kazi hizi. Lakini ushirikiano wenu nasi katika kila hatua umetuwezesha kufikia
malengo. Tunaomba muendelee kushirikiana nasi katika utekelezaji wa
majukumu haya.
Waheshimiwa Viongozi, baada ya shukurani hizo, sasa naomba kuchukua
nafasi hii kutoa taarifa juu ya kazi inayotarajiwa kufanywa na Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar katika kipindi cha miezi sita ijayo. Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar inakabiliwa na kazi ya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya
majimbo ya uchaguzi wa Zanzibar. Kazi hii inaendeshwa kwa matakwa ya
Katiba na inaelekeza kufanyika katika kipindi cha kila baada ya miaka 8 hadi
10. Mara ya mwisho kazi hii ilifanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
mwaka 2005.
Waheshimiwa Viongozi, historia ya Zanzibar inaonyesha kuwa kazi ya
uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi hapa
Zanzibar inafanywa kila baada ya kipindi maalum kama inavyoelekezwa
katika sheria. Jambo hili limetokea tangu miaka ya 1957, 1961 na 1963 wakati
visiwa vyetu vilipoanzisha utaratibu wa kuchagua viongozi wake kwa njia ya
uchaguzi. Aidha, kazi kama hizo zimeendeshwa mara mbili na Tume hii
mwaka 2000 na mwaka 2005.
-
5
Waheshimiwa Viongozi, hivi sasa ni miaka tisa tangu Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar ilipofanya uchunguzi wa idadi, mipaka na majina ya majimbo ya
uchaguzi ya Zanzibar na Sheria inatuelekeza kuwa kazi hiyo inaweza kufanyika
katika kipindi cha miaka minane hadi miaka kumi. Kwa maelekezo hayo,
hesabu zinatuonyesha kuwa hivi sasa tayari tumechelewa kuifanya kazi hiyo
kwa mwaka mmoja na tuna mwaka mmoja wa kuifanya kazi hii, vyenginevyo,
tutakuwa tumekiuka maelekezo ya Katiba. Kwa hivyo, uamuzi wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar kupanga kuifanya kazi ya uchunguzi wa idadi, majina na
mipaka ya majimbo ya uchaguzi katika kipindi hiki unatokana na matakwa ya
Katiba.
Waheshimiwa Viongozi, kazi ya kufanya uchunguzi wa idadi, majina na
mipaka ya majimbo ya uchaguzi tayari imepangiwa utaratibu wake na Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar na utekelezaji wake unaanza rasmi katika mwezi
huu wa Juni 2014 na inategemewa itaendelea mpaka mwanzoni mwa 2015.
Ripoti kamili ya kazi hii imeainishwa katika ratiba ambayo mtapatiwa baada ya
mkutano huu.
Waheshimiwa Viongozi, kazi hii pamoja na kuwa inasimamiwa na kutekelezwa
na Tume ya Uchaguzi kisheria, utendaji wake mpaka kufikia maamuzi
umepangwa kukushirikisheni nyote kila mmoja kwa nafasi yake katika jamii
ya Zanzibar. Tume ya Uchaguzi katika kuifanya kazi hii inategemea kwa kiasi
kikubwa kupata maoni yenu juu ya hali halisi ya majimbo ya uchaguzi ilivyo
hivi sasa katika Wilaya mbalimbali za Unguja na Pemba. Ili kupata maoni yenu
-
6
Tume imeandaa utaratibu wa kukusanya maoni juu ya majimbo kwa utaratibu
ufuatao:-
Kukutana na Wakuu wa Mikoa yote mitano,
Kukutana na Vyama vyote vilivyopata usajili wa kudumu,
Kukutana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali;
Kukutana na Idara ya Utawala Bora,
Kukutana na Uongozi wa Baraza la Wawakilishi,
Kukutana na Halmashauri za Wilaya,
Kukutana na Baraza la Manispaa la Zanzibar;
Kukutana na Mabaraza ya Miji ya Mkoani, Chake Chake na Wete,
Kukutana na Asasi za Kijamii;
Kufanya mikutano ya Wananchi kwa Wilaya zote, na
Kufanya ziara za kuyatembelea maeneo yote yatakayotajwa katika
mikutano ya kuchukua maoni.
Kwa taasisi au watu ambao hawatapata kutoa maoni ana kwa ana mbele
ya Tume ya Uchaguzi juu ya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya
majimbo ya uchaguzi wanaweza kutoa maoni hayo kwa maandishi.
Watendaji wa vyombo vya habari wanaombwa washiriki katika kazi hii kwa
kutoa taarifa mbalimbali za kuielimisha jamii juu ya kazi hii. Tume ya
Uchaguzi itakuwa tayari kutoa msaada wowote utakaohitajika ili
kufanikisha kazi hiyo ya kutoa elimu. Vyombo vya Ulinzi na Usalama navyo
kwa upande wao, vinaombwa vishirikiane na Tume ya Uchaguzi katika
jukumu hili.
Waheshimiwa Viongozi, naomba kuwasilisha.
-
7
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
JECHA SALIM JECHA
MWENYEKITI
TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR
ZANZIBAR