hotuba ya mhe. dkt. jakaya mrisho kikwete, rais wa jamhuri ya muungano wa … · 2015. 6. 30. ·...
TRANSCRIPT
-
1
HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS
WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE
MAADHIMISHO YA KITAIFA YA SIKU YA KUPIGA VITA
DAWA ZA KULEVYA DUNIANI - BAGAMOYO, MKOANI
PWANI,TAREHE 26 JUNI 2015
Mheshimiwa Dkt. Seif Rashid, Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii;
Mheshimiwa Eng. Everist Ndikilo, Mkuu wa Mkoa wa
Pwani,
Ndugu Keneth Kaseke, Kamishna wa Tume ya Kuratibu
Udhibiti wa Dawa za Kulevya;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali;
Viongozi wa Vyama vya Siasa wakiongozwa na Chama
Tawala;
Dkt. Bwijo Bwijo, kutoka UNDP na Wawakilishi wa
Jumuiya na Taasisi za Kimataifa;
Viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia;
Wageni waalikwa;
-
2
Mabibi na Mabwana;
Ndugu wananchi;
Salamu na Shukrani
Nakushukuru sana Mheshimiwa Dkt. Seif Rashid,
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na waandazi wa
shughuli hii kwa kunialika na kunishirikisha katika Siku ya
Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani. Natoa pongezi
nyingi kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Pwani
wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Eng. Evarist Ndikilo
kwa kukubali kuwa wenyeji wa sherehe hizi. Baada ya
kuona mabango na kusikia kauli kadhaa kutoka wasanii
mmejidhihirishia ni jinsi gani mlivyojitayarisha kufanikisha
hafla ya leo. Nawapongeza kwa kushirikiana vyema na
Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya na
kufanikisha maadhimisho haya. Mwisho nitoe pongezi
zangu kwa TAYOA kutokana na ubunifu wao mzuri wa
mawasiliano miongoni mwa vijana. Hongereni sana! Hakika
mambo yamefana sana.
-
3
Aidha, nawashukuru kwa zawadi nzuri ya saa ambayo
itakuwa inanikumbusha wakati wa kulala na kuamka.
Kuadhimisha kupiga Vita Matumizi na Biashara
Haramu ya Dawa za Kulevya
Ndugu wananchi;
Kama alivyoeleza Mwakilishi kutoka UNDP, Dkt.
Bwijo Bwijo tarehe 26 Juni ya kila mwaka ni siku maalum ya
kuadhimisha kupiga vita matumizi na biashara haramu ya
dawa za kulevya duniani. Maadhimisho haya hutupa fursa
ya kutafakari hatua tunazopiga katika jitihada zetu za
kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya katika
jamii zetu na nchi yetu kwa jumla. Katika siku hii pia,
pamoja na kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto za
mapambano hayo tunapanga mikakati ya kukabiliana na
changamoto zilizopo kwa ufanisi zaidi.
Tujenge Jamii, Maisha na Utu wetu bila Dawa za Kulevya.
Ndugu wananchi;
-
4
Kila mwaka maadhimisho haya yanapofanyika
huwepo kauli mbiu ambayo hutoa ujumbe unaosisitiza
jambo lililokusudiwa wakati huo. Kauli mbiu ya mwaka huu
ya, “Tujenge jamii, maisha na utu wetu bila dawa za
kulevya” inatukumbusha sote kukaa mbali na matumizi na
biashara ya dawa za kulevya. Dawa za kulevya ni hatari
kwa maisha ya mwanadamu, utu wake na ustawi wa jamii
yake. Kauli mbiu hii inatutaka tujenge jamii, maisha na utu
wetu bila kujihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za
kulevya. Dawa za kulevya hazina manufaa yo yote bali
hasara tele. Mapambano haya dhidi ya biashara na
matumizi ya dawa za kulevya yanamhusu kila mmoja wetu
wadogo kwa wakubwa, viongozi na wananchi wa kawaida,
matajiri na maskini, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwani
athari zake humgusa kila mmoja wetu.
Madhara ya dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
-
5
Ni jambo lililo dhahiri kuwa dawa za kulevya zina
madhara makubwa sana. Matumizi na biashara ya dawa za
kulevya inaathiri ustawi wa binadamu. Hudhoofisha afya za
watumiaji, na huchochea kuenea kwa maambukizi ya virusi
vya UKIMWI, homa ya ini na mara nyingi husababisha vifo.
Hali kadhalika, huchochea rushwa miongoni mwa
watumishi wa umma hasa wale wanaotegemewa kuongoza
mapambano dhidi yake. Kwa mujibu wa tamko la
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kudhibiti Uhalifu na Dawa za Kulevya alilolitoa tarehe 5
Juni, 2013 kwenye Mkutano wa mwaka wa Vyombo vya
Udhibiti wa Dawa za Kulevya uliofanyika Moscow, watu
wapatao 200,000 hupoteza maisha kila mwaka duniani
kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. Biashara ya
dawa za kulevya imeleta changamoto kubwa kwa jumuiya
ya kimataifa. Kwa baadhi ya nchi, biashara hii imekuwa ni
janga kubwa ambalo limesababisha kuharibika kwa mifumo
ya kiutawala na kisheria, uvunjifu wa amani na usalama,
-
6
kudorora kwa maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi.
Biashara hii huchochea kuwepo kwa magenge ya kihalifu
yanayojihusisha na mauaji, wizi na ujambazi. Hali
kadhalika, mapato yake yanafahamika kugharamia shughuli
za ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara ya
fedha haramu, biashara haramu ya silaha na uporaji wa
nyara za taifa - vitendo ambavyo ni tishio kwa usalama wa
dunia. Hivi basi kupiga vita biashara na matumizi ya dawa
za kulevya ni vita vya haki na ni wajibu kwa kila mtu
kushiriki. Lazima tushinde vita hii.
Juhudi za Mapambano Kimataifa
Ndugu wananchi;
Mataifa mengi duniani yametambua madhara ya
matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Pia watu
wengi wanauona umuhimu wa kufanya juhudi za pamoja
ndani ya nchi, kikanda na kimataifa kukabiliana na uhalifu
huu. Matokeo yake ni kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa
-
7
Mataifa la Kudhibiti Uhalifu na Dawa za Kulevya. Pia, ni
kufanyika kwa operesheni za pamoja za kupambana na
biashara ya dawa za kulevya zinazofanywa na mataifa
mbalimbali kikanda na kimataifa. Jambo lingine ni pamoja
na kuwepo kwa mikutano ya pamoja kimataifa na kikanda
kwa ajili kupanga mikakati ya pamoja.
Naungana na viongozi wenzangu wa nchi mbalimbali
duniani na mashirika wa kimataifa katika mapambano haya.
Nakemea vikali matumizi na biashara ya dawa za kulevya
na kuwaonya wananchi wajiepushe kabisa kujihusisha nazo.
Ni imani yangu kuwa, Watanzania wenzangu mtafanya kila
liwezekanalo kujiepusha na kuwaepusha watu wengine
hasa vijana na watoto kujihusisha na balaa hili. Watanzania
wenzangu tuongozwe na kauli mbiu ya TANU wakati wa
kudai uhuru na kujenga nchi inasema, “Umoja ni nguvu
utengano ni udhaifu”. Na kwa sasa kauli ya CCM isemayo,
”Umoja ni Ushindi”. Hakika umoja wetu ndio
utakaotuhakikishia ushindi katika mapambano haya.
-
8
Vyombo vyetu Viko Macho
Ndugu wananchi;
Naomba niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea
kutimiza wajibu wake katika mapambano dhidi ya biashara
na matumizi ya dawa ya kulevya bila kuchoka na bila
kigugumizi au ajizi yoyote. Lengo letu ni kudhibiti hali ili
kuzuia isizidi kuwa mbaya zaidi ya ilivyo sasa na kubadili
mwelekeo ili hatimaye tulikomeshe kabisa tatizo hili hapa
nchini. Kwa ajili hiyo, tumekuwa tunafanya mambo makuu
matatu.
Kwanza, kuimarisha vyombo vya dola vinavyoongoza
mapambano dhidi ya uhalifu huo. Tunayo Tume ya
Kudhibiti Dawa za Kulevya ambayo imefanya kazi kubwa
ya kuelimisha jamii kujiepusha na matumizi na biashara ya
dawa za kulevya. Tumeendelea kuijengea uwezo Tume
hiyo pamoja na Jeshi la Polisi ambalo ndilo linalokamata
wafanya biashara na watumiaji na kuwafikisha katika
-
9
vyombo vya Sheria. Pamoja na hayo nikaamua kuunda
Kikosi Kazi kilichojumuisha Polisi, Idara ya Usalama wa
Taifa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya. Kikosi Kazi
hicho kimefanya kazi kubwa na nzuri. Kimeongeza nguvu
na uwezo wa kupambana na uhalifu huu na wahalifu
wanaojihusisha na biashara hii haramu na wanaotumia
dawa za kulevya. Wafanya biashara wengi wadogo, wa kati
na wakubwa wamekamtwa na kufikishwa kwenye vyombo
vya sheria. Ukamataji wa Dawa za Kulevya nao
umeongezeka sana na hivyo kunusuru taifa na hata dunia
na madhara ambayo dawa hizo zingefanya. Tumezisikia
takwimu zilizotolewa na Ndugu Keneth Kaseke, Kamishna
wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya.
Hiki ni kiwango kikubwa cha mafanikio hivyo vyombo
vinastahili pongezi nyingi kutoka kwetu sote. Takwimu hizi
zinatuonesha kuwa tatizo ni kubwa hivyo lazima tuwe
katika hali ya tahadhari wakati wote (saa 24 kwa siku zote
saba za wiki).
-
10
Pili, ili kuongeza nguvu, mbinu na maarifa ya
kupambana na uhalifu huu wa hatari na kutisha, tumetunga
Sheria (mpya) ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya ya Mwaka 2015. Sheria hii imejengeka juu ya hali
ilivyo sasa katika mapambano haya. Mafanikio na
changamoto zilizopo imezingatiwa hivyo ni Sheria
inayoimarisha mafanikio tuliyoyapata na kuyapatia
ufumbuzi matatizo yaliyopo. Sheria inaunda chombo
maalum cha kupambana na Dawa za Kulevya. Chombo hiki
kitakuwa na nguvu kubwa zaidi ya kuratibu udhibiti wa
dawa za kulevya nchini. Kimepewa mamlaka ya
kupeleleza, kupekua na kukamata wafanya biashara na
watumiaji wa dawa za kulevya. Nina imani kubwa kwamba
chombo hiki kitasaidia sana kupunguza tatizo hili nchini.
Natanguliza kuwaomba wananchi na vyombo vingine vyote
vya Serikali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa chombo hiki
mara kitakapoanza kazi ili tuweze kulinusuru taifa letu na
tatizo hili.
-
11
Huduma za Matibabu
Ndugu wananchi;
Kwa kuzingatia hekima na busara za usemi wa
Wahenga, ”Kinga ni bora kuliko tiba”, mkakati wa
kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya unasisitiza
sana kuelimisha jamii kuhusu kuepukana na kujihusisha na
biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Kwa wale
waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya, mkakati ni wa
Serikali kuendeleza jitihada za kuwapatia ushauri nasaha na
matibabu. Hilo ndilo jambo letu la tatu. Kwa sasa huduma
hizi zinapatikana katika vitengo vya magonjwa ya akili
katika hospitali za baadhi ya mikoa na wilaya hata nchini.
Hata hivyo, idadi ya watumiaji wanaopata nafasi ya kupata
huduma za tiba bado ni ndogo sana. Takwimu zinaonesha
kuwa kuna watumiaji wa heroin wanaokadiriwa kuwa kati
ya 200,000 na 425,000 nchini. Idadi ya watumiaji wa heroin
wanaopata matibabu kwa kutumia tiba ya methadone
-
12
mpaka kufikia Mei, 2015 ni 2,300 tu. Watu hawajitokezi kwa
wingi. Tafadhalini ndugu zangu jitokezeni mpate uponyaji.
Ninaiagiza mikoa yote hasa ile yenye matatizo
makubwa ya matumizi ya dawa za kulevya hususani Dar es
Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Pwani na
Shinyanga kuchukua hatua thabiti za kuanzisha na
kuendeleza huduma hizi. Lazima tutambue pia, kwamba
hakuna Mkoa ambao uko salama, tofauti ni kiwango cha
athari. Hivyo basi kila Mkoa ujiandae ipasavyo. Tahadhari
kabla ya hatari. Nawataka Viongozi wa Mikoa na Wilaya
kote nchini wafuatilie utekelezaji wa jambo hili. Kamati za
Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya ziliweke suala la
dawa za kuleya kuwa agenda ya kudumu katika vikao vyao.
Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wale wote
waliosaidia katika kuanzisha na kuendeleza huduma ya
methadone na huduma nyingine za matibabu nchini.
Niruhusuni nitoe shukrani maalum kwa Rais Barack Obama
-
13
na Serikali ya Watu wa Marekani kwa msaada mkubwa
wnaotupatia kwa upande wa matibabu.
Tusiharibu Taswira ya Nchi yetu
Ndugu wananchi;
Narudia kuelezea masikitiko kuhusu baadhi ya
Watanzania wenzetu wanaojihusisha na biashara ya dawa
za kulevya nje ya nchi. Hawa ni chachu ya kuendelea kwa
tatizo hapa nchini. Pia, wanaharibu taswira nzuri ya nchi
yetu kimataifa na kuhatarisha maisha yao. Zipo taarifa
kuwa kati ya Januari 2012 na Desemba 2014, kwa mfano,
jumla ya Watanzania 111 walikamatwa kwa kujihusisha
biashara hiyo katika nchi za Brazil na China. Hii ni fedheha
kubwa. Pia, naomba niwakumbushe na kuwatahadharisha
kuwa baadhi ya nchi hutoa adhabu kali ikiwemo ya kifo
kwa watu watakaokamatwa na kutiwa hatiani. Mfano
mmoja wapo ni wa yale yaliyotokea Indonesia kati ya
Januari na Aprili 2015 ilipowanyonga wasafirishaji wa dawa
-
14
za kulevya 12 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo za Afrika.
Nchi hiyo ilikataa maombi ya nchi zao kutaka adhabu hiyo
isitekelezwe dhidi ya raia wao.
Akitetea uamuzi wa nchi yake Mwanasheria Mkuu wa
Indonesia Muhammad Prasetyo baada ya hukumu
kutekelezwa alisema;
‘Tunapigana vita dhidi ya uhalifu wa kutisha wa dawa za kulevya
ambao unatishia mustakabali wa taifa letu. Napenda kusema
kwamba kuua si jambo jema, si jambo la kufurahisha. Lakini
lazima tufanye hivyo kwa ajili ya kuliokoa taifa na hatari ya dawa
za kulevya. Hatufanyi uadui na nchi ambazo raia wake
walihukumiwa kifo.’
Nawaasa Watanzania wenzangu watambue ukweli
huu na kuachana na biashara ya dawa za kulevya ndani na
nje ya nchi yetu. Ni hatari kwao na taifa pia. Ingawa hapa
nchini adhabu ya kifo haitolewi kwa kosa la kujihusisha na
dawa za kulevya, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na
-
15
Dawa za Kulevya ya 2015 ambayo itaanza kutumika hivi
karibuni inatoa adhabu kali hadi kifungo cha maisha.
Tahadhari Dhidi ya Matumizi ya Shisha
Ndugu wananchi;
Kwa masikitiko makubwa, Serikali imepokea malalamiko
mengi kuhusu matumizi ya shisha nchini. Matumizi haya
yameenea kwa haraka katika maeneo mengi ya starehe na
huwavutia vijana wengi wa kiume na wa kike. Watumiaji
wa kilevi hiki huonyesha dalili zinazofanana na za utumiaji
wa dawa za kulevya. Hivyo, kuna hofu kuwa kilevi hiki
kinachanganywa na dawa za kulevya. Kama hiyo ni kweli ni
jambo hili ni la kusikitisha sana, halikubaliki na kwamba
hatuna budi kuhakikisha kuwa haliachwi kuendelea.
Nichukue nafasi hii kuziagiza mamlaka husika kufanya
uchunguzi haraka iwezekanavyo ili kupata majibu
yatakayosaidia kutatua tatizo hili na hatimaye kuinusuru
jamii yetu.
-
16
Tusiruhusu Rushwa Ijipenyeze
Ndugu wananchi;
Mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za
kulevya si lelemama. Kuna changamoto kadhaa ikiwa ni
pamoja na vishawishi vya rushwa. Vitendo vya rushwa kwa
baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu vinachangia
sana katika kurudisha nyuma mapambano dhidi ya tatizo la
dawa za kulevya. Natoa agizo kwa mamlaka husika
kuhakikisha kuwa suala la rushwa linadhibitiwa kikamilifu
katika mapambano haya kwa kuwachukulia hatua stahiki
wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Mjitokeze kwa Wingi Kujiandikisha
Ndugu wananchi;
-
17
Wote mnatambua vema kuwa mwaka huu tutakuwa
na uchaguzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali katika
Taifa letu. Nawaasa wananchi wenzangu muendelee
kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha katika Daftari la
Kudumu la Mpiga Kura. Wakati wa kupiga kura
utakapofika, mtumie haki yenu ya kikatiba kuchagua
viongozi waadilifu ambao kwa namna yoyote ile
hawajihusishi na biashara au matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, nawaasa wazazi na walezi, viongozi wa dini,
viongozi wa asasi za kijamii, watambue kuwa hivi ni vita
vyetu sote. Tatizo la dawa za kulevya likiachiwa bila
kudhibitiwa kwa dhati litaleta maafa makubwa kwa kizazi
cha sasa na kijacho. Kwa sababu hiyo, tunao wajibu wa
kupambana kila mtu kwa nafasi yake. Tuwalee watoto wetu
kwa misingi ya maadili mema ili kujenga Taifa lisilokuwa na
matumizi wala biashara ya dawa za kulevya. Inawezekana
Timiza Wajibu wako.
Tujenge jamii, maisha na utu wetu bila dawa za kulevya
-
18
Asanteni kwa kunisikiliza.